1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

140610 Langzeitwirkungen der Ölpest

Josephat Nyiro Charo14 Juni 2010

Maafa yaliyoikumba ghuba ya Mexico kutokana na kuendelea kuvuja kwa mafuta hayana kifani. Sasa inaingia wiki ya saba tokea mafuta hayo yaanze kuvuja na hakuna anaejua ni lini hali itaweza kudhibitiwa tena

https://p.dw.com/p/Nq8N
Mafuta yakivuja kutoka kisima kilicho ghuba ya MexicoPicha: AP

Wahusika wanajaribu kutumia njia ya kuleta nafuu kwa kuchimba tena. Labda suluhisho litapatikana kwa njia hiyo. Hata hivyo ni katika mwezi wa Agosti tu ambapo njia hiyo itaweza kutumika.

Lakini kwa sasa keundelea kuvuja mafuta hayo kunazidi kuleta madhara. Afya za binadamu pia zinaathirika kutokana na maafa ya mafuta. Watu wapatao 70 sasa wanatibiwa kutokana na maradhi ya udhia, maumivu ya kichwa, uvimbe wa macho na shida za kupumua. Na wanane ya hao wamelazwa hospitalini. Na hadi sasa baada ya wiki kadhaa za kumwagika mafuta na kuingia baharini hakuna anayejua uhakika ni kiasi gani kimeshaingia baharini.

Tokea wiki jana yamefanyika makadirio mengine yanayoonyesha kwamba kiasi cha lita milioni 6.4 za mafuta zinaingia baharini kila siku kutoka kwenye kisima ambapo mafuta hayo yalikuwa yanachimbwa chini ya bahari. Makadirio hayo ni mara mbili ya kiasi ambacho kimekuwa kinafikiriwa hadi sasa.

Mkuu wa asasi ya kimataifa ya uhifadhi wa mazingira Carl Gustaf Lundin amesema maafa yanayotokea kwenye Ghuba ya Mexiko ni miongoni mwa makubwa aliyowahi kuyashuhudia.

Maafa haya yanaathiri kila kitu kuanzia chini ya bahari, juu ya bahari na mfumo wote wa ikolojia kuanzia mita 50 hadi alfu moja chini ya bahari. Pia yanaathiri sehemu za juu ya bahari hadi kwenye fukwe. Viumbe vya baharini vinakunywa mafuta. Fukwe, sehemu za unyevunyevu na maeneo ya mikoko pia yanazama chini ya mafuta.

Mtaalamu huyo amesema mafuta hayo hayaelei juu ya bahari tu. Pia chini ya bahari, matabaka yamejijenga ambapo matone ya mafuta yanaganda.

Kiwango cha maafa kama hayo yanayotokea chini bahari hakijawahi kuonekana. Na ndiyo sababu mtaalamu huyo Carl Gustaf lundin amesema ni vigumu kukadiria madhara yake. Kwa sasa mtaalamu huyo na wenzake wanatayarisha kemikali zitakazolikata tope la mafuta na hivyo kuaylinda mazingira kwenye fukwe.

Lakini tatizo ni kwamba dawa hizo zina kiwango cha sumu cha juu na madhara yake kwa mazingira hayawezi kupimika. Mtaalamu mwengine Ron Kendal amesema maafa yaliyosababishwa na kuvuja kwa mafuta yanaikumba kila sehemu ya Ghuba ya Mexico. Kwa hiyo amesema sumu inatapakaa pote na kuleta madhara kwa binadamu, wanyama, na mimea.

Mwandishi/ Röhrlich, Dagmar/ZAR/

Tafsiri/Mtullya, Abdu

Mhariri/ Josephat Charo