1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Magazeti ya Ujerumani-06.09.2016

Admin.WagnerD6 Septemba 2016

Wahariri wa Ujerumani wameandika zaidi kuhusu uchaguzi wa jimbo la uzawala la Merkel uliompa matokeo mabaya Kansela huyo na Chama chake

https://p.dw.com/p/1JwRE
Merkel akiwa Bad Doberan
Merkel akiwa Bad DoberanPicha: picture-alliance/dpa/B. Wüstneck

Badische Nueste Nachrichten
Mhariri anasema kwamba kwa chama cha CDU, matokeo ya uchaguzi huo ni ujumbe wa tahadhari kwamba muda wa ziada wa kuwepo madarakani kansela huyo umemalizika. Kansela Merkel, ambaye katika kipindi cha miaka mitatu ya nyuma alikuwa ni mtu pekee anayeuhakikisha ushindi wa chama chake cha CDU katika uchaguzi mkuu, sasa ni mwanasiasa anayeonekana kuwapa nguvu tu wapinzani wake ambao wanaonekana kuongezeka na wenye mizizi kutoka chama chake cha CDU na chama ndugu CSU. Mhariri wa gazeti hilo anamalizia maoni yake kwa kujiuliza, je Angela Merkel amekuwa mzigo kwa chama chake?

Mitteldeutsche Zeitung

Uchaguzi wa Mecklenburg -Vorpommern unakumbusha juu ya janga la kushindwa vibaya kwa chama cha Social Democratic, SPD, mwaka 2005 katika jimbo la NorthRhine-Westphalia.Wakati huo aliyekuwa Kansela Gerhard Schroeder alishindwa vibaya na chama chake kutokana na mageuzi ya kijamii aliyoyaanzisha, ambayo lengo lake lilikuwa kuwapa msaada wasiokuwa na ajira, katika kile kinachoitwa mpango wa Hartz V, mageuzi yaliyokosa umaarufu miongoni mwa jamii ya Wajerumani. Sasa ni zamu ya Kansela Merkel ambaye anakabiliwa na kishindo kutokana na sera yake kuhusu wahamiaji. Kama Mfalme Belsazar wa Babilon alivyoandika maandishi yake mashuhuri ukutani, sasa alama za mikasi kwenye kura ilizopata chama kisichopendelea wageni cha AfD, ni ishara kwamba muda wa Kansela Merkel nao umemalizika.

Volksstimme :
Mikutano kama hii ya G20 imekuwa na sifa ya kuwa mikusanyiko isiyokuwa na maana wala tija yoyote. Hata katika mji wa Hangzhou hayo yameonekana. Kilichofanyika ni kuwepo majadiliano baina ya viongozi na mara nyingine vikao hivyo kuchukua muda mrefu zaidi kuliko ilivyopangwa. Kwa haraka haraka inaweza kuonekana kwamba makubaliano yamefikiwa kama ilivyo mfano katika suala la Syria. Marais wa Marekani na Urusi, Barack Obama na Vladmir Putin, walijaribu kutafuta makubaliano ya kufikia usitishaji mapigano katika nchi hiyo yenye vita,ingawa juhudi za mwanzo hazikufanikiwa lakini baada ya miezi kadhaa matumaini yanaonekana kukaribia. Kadhalika mgogoro wa Ukraine limekuwa suala gumu kupatiwa ufumbuzi. Alau lakini katika mji wa Hangzou pande nne zilidiriki kukutana kuujadili mgogoro huo,Urusi Ufaransa,Ujerumani na Ukraine yenyewe. Kwa siku kadhaa rais wa Urusi alikuwa akiupinga mkutano huo akisema jumuiya ya Kimataifa haiwezi kuutatua mgogoro huo. Kilicho dhihirika kwahivyo migogoro ya kimataifa haiwezi kutatutiliwa katika mikusanyiko ya aina hii.Isipokuwa mikutano ya aina hii inasaidia katika kupiga hatua ndogo ya kufanyika vikao muhimu vya kubadilishana mawazo.

Rhein Zeitung

Mhariri wa gazeti la Rhein Zeitung linalochapishwa mjini Koblenz anajaribu kutoa ushauri kwa viongozi wa Ulaya kuelekea mkutano ujao wa kundi hilo la G20 utakaofanyika Hamburg Ujerumani.Mhariri huyo anasema Ulaya itapaswa kuitumia nafasi hiyo kikamilfu kusukuma malengo yake. Mwaka ujao wa 2017 Ulaya itakuwa katika nafasi bora zaidi kuzungumzia malengo yao katika mkutano wa G20 utakaoongozwa na Kansela Angela Merkel.Katika mkutano wa Hangzou viongozi wa Ulaya hawakuonesha kufanikiwa badala yake ilikuwa dhahiri kwamba wameshindwa kuonesha ni kwa jinsi gani walivyojipanga kuendelea baada ya Uingereza kujitoa katika taasisi hiyo. Si hivyo tu lakini Ulaya imeonekana pia kuburuzwa na China na Marekani katika kuyapitisha makubaliano ya tabia nchi. Juu ya hilo bado suala la wakimbizi limebakia kuwa tatizo la Ulaya.Kwa hali hiyo Ujerumani itakapochukua uwenyekiti wa G20 mwaka 2017 inabidi katika mkutano utakaofanyika mwezi Julai mjini Hamburg iweke wazi mipango madhubuti ya kuchukua hatua kulipatia ufumbuzi suala la mgogoro wa kimataifa wa wakimbizi.Si hilo tu lakini Kansela Merkel atapaswa kuufanikisha mpango huo na hasa kwa kutilia maanani kwamba suala hilo litahodhi nafasi kubwa katika uchaguzi mkuu.

Mwandishi: Saumu Mwasimba/Deutsche Zeitungen
Mhariri: Mohammed Khelef