1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Magazeti ya Ujerumani juu yanjaa, China na serikali ya Ujerumani

Dreyer, Maja30 Aprili 2008

suala muhimu magazetini hii leo ni hali ya serikali ya mseto ya Ujerumani baada ya mkutano wa kamati maalum ya muungano huo hapa jana.

https://p.dw.com/p/DrBi
Picha: dpa

Lakini kabla ya hapo tusikie kidogo kuhusu mada nyingine ambazo mara kwa mara tena zinazingatiwa na wahariri. Kwanza ni mzozo wa chakula na njaa duniani. Kuhusiana na hilo, gazeti la “Obermain-Tagblatt” limeandika hivi:


“Ghasia zilizoanza kutokea kwa sababu ya njaa ni kama dalili ya mzozo mkubwa ambao ulimwengu utakabiliwa nao. Na tunaweza kuona matokeo ya sera mbaya za kilimo yaani kwamba nchi tajiri zinazishinda nchi nyingine na kuongeza nguvu zao kwenye soko la kimataifa. Tena njaa ya watu maskini inazidi kuwapatia faida wafanyabiashara wa nchi za Magharibi. Bei zinapandishwa juu zaidi kwenye soko la hisa. Binadamu kweli amepoteza maadili na malengo yake.”


Mada nyingine inayobaki juu kwenye vichwa vya habari ni michezo ya Olimpiki itakaofanywa China siku 100 kutoka sasa. Gazeti la kila wiki la “Die Zeit” linaangalia vile mbinyo wa kutoka nje linazidi kuitishia China. Limeandika:


“Kweli, tishio ni la aina ya pekee. Kwanza kwa sababu maadamano dhidi ya sera za China kuelekea Tibet yalifanywa duniani kote na pili kwa sababu si tu watu wa kawaida wanaopinga sera hizo, bali pia serikali kadhaa. Ndiyo maana kuwepo kitisho kutoka pande hizo mbili ni jambo jipya. Viongozi wa nchi husika wanaweza kuvumilia maandamano barabarani, na vilevile wanaweza kuvumilia ukosoaji wa kidiplomasia kutoka kwa serikali nyingine. Lakini itakuwa vigumu sana ikiwa watu wa kawaida wanaandamana wakati ambapo viongozi wa nchi nyingine kama rais Sarkozy anatishia kususia sherehe ya kufunguliwa rasmi michezo ya Olimpiki. Na pia ni hatua kali kama Kansela wa Ujerumani, Angela Merkel anasema hatakubali kuelekezwa na China ikiwa Ujerumani inaruhusiwa kumkaribisha Dalai Lama au la.”


Naam, tuelekee sasa katika mada muhimu kwenye magazeti ya leo, yaani hali ya serikali ya mseto na tusikie yaliyoandiwa na “Ostthüringer Zeitung”:


“Muungano huu kati ya vyama vikubwa umepwaya. Bila ya kuwa na mawazo mapya, vyama vya CDU na SPD vinakaribia mwisho wa utawala wao wa pamoja. Mkataba wa serikali ya mseto umeweka malengo yao ambayo yanatekelezwa moja baada ya lingine. Lakini juu ya hayo, vyama hivi havina nguvu tena. Na Kansela Angela Merkel anapendelea sera za siasa za kimataifa kuliko kuongoza sera za siasa za ndani.”


Uongozi wa Kansela Merkel unakosolewa pia na gazeti la “Rhein-Zeitung” katika uchambuzi wake.


“Angela Merkel anasubiri wanaoshindana katika ngazi za chini wadhoofishane ili yeye aweze kushinda. Hataki mzozo katika serikali yake, anapendelea ukimya kama ule wa kwenye kaburi. Hata huwezi kusema, Kansela huyu anaongoza kwa utulivu. Kusema ukweli, Bi Merkel anazuia Ujerumani kuendelea mbali. Hata ikiwa mambo mengi yanazungumziwa na mikutano inafanyika, hakuna maendeleo. Inaonekana kama magari haya makubwa ya kiserikali yanatumika bila ya maana huko mjini Berlin.”