1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Magazeti ya Ujerumani yazungumzia kirusi cha Omicron

Josephat Charo
3 Desemba 2021

Wahariri wa magazeti ya Ujerumani wiki hii wamezungumzia athari zilizotokana na kirusi kipya cha corona na operesheni ya kuwakabili waasi wa ADF wa Uganda.

https://p.dw.com/p/43ocA
Südafrika Tourismus OR Tambo Flughafen in Johannesburg
Picha: Jerome Delay/AP Photo/picture alliance

Gazeti la Berliner Zeitung ambalo lilikuwa na kichwa ha habari kilichosema "Pigo kwa utalii kutokana na kirusi cha Omicron. Vizuizwi vipya vimeaiathiri Afrika Kusini na sekta yake ya usafiri". Mhariri anasema katika sehemu ya abiria wa kimataifa wanaowasili uwanja wa Cape Town Jumapili asubuhi, dereva mmoja tu wa teksi alionekana akiwa amekaa akisikiliza ibada ya kanisani katika simu yake ya mkononi. Kwa kawaida ndege kadhaa huwa zinatua wakati kama huu. Bango lenye maneno uwanja ulioshinda tuzo sasa unawakaribisha abiria milioni 10 linaning'inia kutoka darini. Ni la tangu siku za kabla ya janga la corona. Sasa mambo yamebadilika kabisa.

Gazeti la der Freitag linauliza je hii ndiyo shukurani tunayoipata? Afrika Kusini ilitoa onyo la awali kuhusu kirusi cha Omicron, lakini matokeo yake ikakabiliwa na maonyo ya watu kutosafiri kwenda nchini humo. Hatua ya serikali ya Afrika kusini kutangaza ugunduzi wa kitusi hicho ni mfano mzuri wa kuigwa na onyo la kwanza katika ngazi ya kimataifa. Inasaidai kuchukua hatua muafaka kuepusha kirusi hicho kuenea katika maeneo mengine na kufanya vipimo na kutoa matibabu. Hata hivyo vizuizi vya kusafiri vinatekelezwa kwa mataifa ya kusini mwa Afrika, lakini sio kwa nchi nyingine zilizoathiriwa. Mhariri anasema ni hatua ambazo zimechukuliwa kwa haraka na zinaathiri uchumi kwa kiwango kikubwa. Hii huenda ikazivunja moyo nchi kutoa onyo la mapema siku zijazo iwapo aina mpya ya kirusi itagunduliwa.

Mdahalo kuhusu chanjo

Gazeti la Frankfurter Allgemeine liliandika kuhusu mdahalo wa chanjo za lazima barani Afrika. Afrika Kusini na Kenya zinataka kuifanya chanjo kuwa ya lazima. Nchini Afrika Kusini watu walikuwa wanajiandaa kwa tangazao la kufungiwa tena majumbani na kufungwa kwa shughuli za kila siku. Mwishoni mwa wiki iliyopita foleni ndefu zilishuhudiwa katika maduka ya kuuza mvinyo, wateja wakijinunulia na kwenda kujiwekea majumbani. Huko nyuma vizuizi vikali dhidi ya uuzaji wa pombe vilifuatiwa na marufuku ya uuzaji wa pombe kwa lengo la kupunguza shinikizo kwa vyumba vya dharura vya kuwahudumia wagonjwa mahospitalini.

Nalo gazeti la Süddeutsche lilikuwa na kichwa cha habari kilichosema majanga mawili kwa mpigo. Kirusi cha corona kinakwamisha mapambano dhidi ya ugonjwa wa ukimwi na virusi vinavyosababisha ugonjwa huo vya HIV. Watu kama mshauri wa wanawake Alice Atieno kutoka Kenya sasa wanakabiliana na changamoto kadhaa za majanga mawili kwa wakati mmoja.

Uganda yawakabili waasi wa ADF

Gazeti la Tageszeitung liliandika kuhusu hatua ya Uganda kuwashambulia waasi wa kundi la Allied Democratic Force, ADF mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo. Uganda imechukua hatua hiyo kulipiza kisasi mashambulizi ya kigaidi kwa ushirikiano na serikali ya Congo, lakini serikali hiyo imenyamaa kimya kuhusu suala hilo. Mhariri wa gazeti hilo kutoka Uganda Simone Schlindwein aliandika "Mapema leo pamoja na washirika wetu wa Congo, tumefanya mashambulizi ya kutokea angani dhkdi ya kambi za ADF," lilitangaza jeshi la Uganda mnamo siku ya Jumanne.

Afrika Uganda Edward Katumba Wamala
Mnadhimu mkuu wa majeshi ya Uganda, Jenerali Edward Katumba Wamala, katikati, pamona mwenzake wa Congo, Luteni Jenerali Didier Etumba Longila, kushoto, na kamanda wa jeshi la Congo, Jenerali Leon Mushale, kulia, wakiwa Beni, Kivu Kaskazini Mei 7, 2014.Picha: AFP via Getty Images

Uingiliaji kati katika nchi jirani ya Congo ni hatua ya Uganda kufuatia mashambulizi ya kigaidi katika mji mkuu Kampala katikati ya mwezi Novemba, ambapo watu wanne waliuwawa. Waasi wa ADF kutoka Uganda, ambao wamekuwa wakiendesha shughuli zao katika eneo la mpakani na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, hufanya mauaji ya kiholela ya raia nchini Congo na wamejitangaza kuwa sehemu ya Dola la kiislamu ukanda wa Afrika ya Kati, ISCAP.

Jarida la der Spiegel lilikuwa na kichwa cha habari "Mkataba na shetani" likizungumzia hali ya machafuko nchini Sudan. Mhariri anasema nchi hiyo ilichukuliwa kama nchi ya matumaini kwa mapinduzi ya kiarabu, lakini kiasi wiki nne zilizopita, jeshi likafanya mapinduzi. Sasa vuguvugu hilo changa la demokrasia linapigania uhai wake.

Kitisho cha vita Afrika Kaskazini

Gazeti la die Welt lilizungumzia kitisho cha vita Afrika Kaskazini. Israel sasa pia inaipelekea Morocco silaha za kisiasa. Taifa jirani la Algeria linazungumzia usaliti wa waarabu na inachochoea mzozo na ufalme huo. Ulaya tayari inakabiliwa na athari. Wanajeshi walisimama katika gwaride wakati waziri wa ulinzi wa Israel Benny Ganzt alipowasili mji mkuu wa Morocco, Rabat wiki iliyopita kwa ziara ya kihistoria. Waziri huyo alisaini mkataba wa usalama, wa kwanza na taifa hilo la kiarabu. Gantz alielezea kuridhishwa kwake akisema makubaliano hayo yanaashira mabadilishano ya mitazamo, kuratibu miradi ya pamoja na kupata ridhaa ya kuuza bidhaa za Israel nchini humo.

Gazeti la neue Zürcher liliripoti juu ya kufunguliwa uchunguzi wa kisheria ukoo wa Kabila. Kanzi kubwa kabisa ya data barani Afrika inafichua jinsi watu wa karibu wa rais wa zamani wa Jamhuri ya Kiemokrasia ya Congo walivyochota fedha kutoka kwa makasha ya serikali. Kupitia kichwa cha habari Congo Hold Up - Congo Robbery yaani Unyang'anyi Congo - Wizi wa Congo - ndilo jina la mfululizo wa uchunguzi ambao umekuwa ukizua gumzo nchini Congo kwa zaidi ya wiki sasa. Uchunguzi huo unaofanywa na vyombo vya habari kadhaa vya kimataifa na mashirika ya kimataifa yasiyo ya kiserikali, unafichua jinsi rais mstaafu Joseph Kabila, familia yake na wapambe wake wa karibu kisiasa walivyofanya kila walichoweza kujitajirisha kifedha wakati walipokuwa mamlakani.

Vifaa vya tume ya amani vina mapungufu Mali

Gazeti la Suddeutsche lilibeba kichwa cha habari kilichosema "Hili halitakiwi kuruhusiwa kutokea" Kamishna wa ulinzi akosoa vifaa vinavyotumika katika tume za mataifa ya kigeni. Kamishna wa bunge la Ujerumani, Bundestag, anayeshughulikia masuala ya ulinzi, Eva Högl, ameelezea wasiwasi wake kuhusiana na taarifa kutoka kwa maafisa wanaume na wanawake wa jeshi kuhusu mapungufu ya vifaa katika tume walizohudumu kwenye nchi za kigeni.

Gazeti linasema wiki iliyopita, mwanasiasa huyo wa chama cha Social Democratic, SPD, aliwatembelea wanajeshi wa Ujerumani nchini Mali na nchi jirani ya Niger na akasikia ukosoaji. Gateti limemnukulu kamishna huyo akisema baada ya kurejea nchini "Inasemekana kila mara kwamba katika uwanja wa mapambano tuna kila kitu kilicho tayari. Nina mashaka yangu kuhusiana na hilo. Kiongozi huyo pia amesema alifahamishwa kwamba wanajeshi hawana vifaa vya kutosha wakati wanapokwenda katika uwanja wa mapambano na hilo halikubaliki.

http://iua.dwelle.de/typo3/index.php?id=322&no_cache=1