1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Magazeti ya Ujerumani

26 Julai 2010

Mada inayoendelea kugonga vichwa vya habari ni msiba uliotokea wakati wa tamasha la muziki Love Parade, jumamosi iliyopita katika mji wa Duisburg.Basi tutaanza na gazeti la VOLKSSTIMME linalosema:

https://p.dw.com/p/OUkC
Teilnehmer versuchen am Samstag, 24. Juli 2010, in Duisburg, Nordrhein-Westfalen, beim Techno-Musikfestival Loveparade 2010 nach einer Panik das gesperrte Gelaende zu verlassen. Vor dem Gelaende vor der Loveparade in Duisburg ist es am Samstag zu einer Massenpanik gekommen. Nach Angaben der Polizei wurden dabei zehn Menschen getoetet. (apn Photo/Hermann J. Knippertz) --- Collapsed people get first aid after a panic on this year's techno-music festival "Loveparade 2010" in Duisburg, Germany, on Saturday, July 24, 2010. (apn Photo/Hermann J. Knippertz)
Watu wakiparamia ukuta ili kukimbia eneo la tamasha la muziki "Love Parade" kufuatia mkanyagano uliotokea Jumamosi, 24 Julai 2010, mjini Duisburg, Ujerumani.Picha: AP

"Yaliyotokea Duisburg hayakuwa maafa ya kimaumbile. Vifo vya vijana waliokwenda kujifurahisha katika tamasha la muziki vingeweza kuzuiliwa. Kwa hivyo sababu za maafa hayo lazima zichunguzwe na wakosa watajwe. Hilo linastahili kutekelezwa kwa heshima ya wahanga."

Na gazeti la MÄRKISCHE ALLGEMEINE linaeleza hivi.

"Ni muhimu kujua nani anaewajibika kuhusu maafa yaliyotokea mjini Duisburg - lakini kwanza kabisa, ikumbukwe kuwa tamasha lililowahi kuvutia hadi watu milioni 1.5 katika miaka iliyopita, safari hii limefanywa katika eneo lililozingirwa ambalo lina uwezo wa kuchukua watu 300,000 tu. Na njia ya kuingilia ni moja tu."

Kwa hivyo, tangu mwanzoni, wataalamu wa usalama walionya kuwa mji wa Duisburg haufaii kwa tamasha kubwa kama hilo.Likiendelea MÄRKISCHE ALLGEMEINE linasema:

"Ionekanavyo faida ya kibiashara ndio iliyopewa kipaumbele na waandalizi wa tamasha na wakuu wa mji wa Duisburg.Kwa hivyo,tamasha ambalo kauli mbiu yake ni "amani na furaha" likaishia kwa vifo vya watu 19, zaidi ya majeruhi 340 na huzuni mkubwa kwa familia za wahanga."

"Vifo 19 na zaidi ya majeruhi 340 ni msiba mkubwa wa taifa, uliotokea katika mkanyagano na msukumano wakati wa tamasha la muziki la Love Parade" limeandika gazeti la OLDENBURGISCHE VOLKSZEITUNG.

"Kwa maoni ya gazeti hilo, hayo yote yangeweza kuepukwa. Kwani maelfu ya watu walikuwa na njia moja tu ya kuingilia uwanjani. Hapo wala uhitaji kuwa mtaalamu wa maandalizi ya tamasha, kugutuka na kuingiwa na mashaka - hata mtu mwenye akili ya kawaida angetambua hatari katika mpango huo."

Na gazeti la RHEIN-NECKAR ZEITUNG likiendelea na mada hiyo hiyo linaeleza hivi:

"Mji wa Bochum ni mfano mzuri, kwani mwaka jana mji huo ulikataa kabisa kuwa mwenyeji wa tamasha la Love Parade. Sababu ni wasiwasi kuhusu uwezo wake wa kuhakikisha usalama wakati wa sherehe hizo. Lakini, ionekanavyomwaka huu iliamuliwa kuandaa tamasha hilo kwa hali yo yote ile. Na wahanga ni watu 19 waliopoteza maisha yao."

"Maafa yaliyotokea pia ni kifo cha tamasha la Love Parade" ndio linavyosema gazeti la BERLINER ZEITUNG na kuongezea:

"Hapo kabla matatizo ya fedha ndio yaliyohatarisha tamasha hilo. Lakini sasa, msingi wa tamasha hilo umebomoka. Kwani tamasha hilo lilipofanywa kwa mara ya kwanza katika mwaka 1989, wito wake ulikuwa "Amani na Furaha" na kiasi ya watu 150 waliandamana kwa midundo ya muziki katika barabara kuu ya jiji la Berlin. Kila mwaka, idadi ya watu iliongezeka na kuweka rekodi ya watu milioni moja na nusu katika mwaka 1999."

"Lakini mji wa Duisburg, umeondoa pepo hiyo ya furaha" lamalizia BERLINER ZEITUNG.

Mwandishi:P.Martin/DPA

Mhariri:Josephat Charo