1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Magazetini: Marekani yahamishia ubalozi wake Jerusalem

Sekione Kitojo
15 Mei 2018

Wahariri wa magazeti ya Ujerumani wamezungumzia kufunguliwa ubalozi wa Marekani mjini Jerusalem, na mjadala juu ya wachezaji wa timu ya taifa ya Ujerumani Ozil na Gundorgan kukutana na rais wa Uturuki Erdogan.

https://p.dw.com/p/2xk70
Gaza Israel Konflikt Jerusalem US Botschaft
Picha: Reuters/R. Zvulun

 

Gazeti la  Neue Osnabrueker Zeitung  likiandika  kuhusu  mzozo  wa mashariki  ya  kati, linasema:

"Kuutambua  mji  wa  Jerusalem  kama  mji  mkuu  wa  Israel kunaweza kuzungumziwa  tu kama  vile  mchezo wa karata, wakati rais Donald Trump akisubiriwa kuja  na  mpango  mahsusi  wa amani,  ambao  unaweza  kuwaleta  karibu  Wapalestina  na Waisrael  katika  suluhisho  la  mataifa  mawili. Iwapo  Israel itakuwa tayari kuonesha  maridhiano  na Palestina  baada  ya  zawadi  ya kidiplomasia  kutoka  Marekani, kwa mfano  katika  sera zake  za kujenga  makaazi  ya  Wayahudi, hilo lina  shaka. Uamuzi  wa  Trump kuhusu Jerusalem  na  kujitoa  katika  mkataba  wa  kinyuklia  na Iran  inaweza  kuwa ishara mbaya.  Moto unawaka katika  mashariki ya  kati. Kufikiria  kwamba  Umoja  wa  Ulaya  unaweza  kujitoa, si jambo  linalotarajiwa. Mbaya  zaidi , hakuna  mtu  ambaye  anaweza."

Israel Eröffnung der US-Botschaft in Jerusalem
Mshauri mwandamizi katika Ikulu ya Marekani White House Ivanka Trump akisimama karibu na maandishi ya ukutani yanayoonesha ubalozi wa Marekani mjini JerusalemPicha: Reuters/R. Zvulun

Mhariri  wa  gazaeti  la  Badische Zeitung  la  mjini  Freiburg akizungumzia  kuhusu  kuhamishwa  kwa  ubalozi  wa  Marekani kutoka  Tel Aviv kwenda  Jerusalem, anasema  kwamba  wakati Waisrael  wanashangilia  kufunguliwa  kwa  ubalozi  huo, Ukanda  wa Gaza  kunawaka  moto. Mhariri  anaendelea kwa  kusema:

"Ni  mara  chache  maandamano  yamekuwa  makubwa  na  ya hasira   kama  yalivyo  sasa, wakati  Marekani  inafanya  juhudi  za kuzipatanisha  Israel  na  Palestina. Haya  ni  matokeo  ya  uamuzi wa  Trump. Kila  mmoja  anafahamu, kwamba  gharama  iko juu mno. Na nani analazimika  kulipa ?"

Miaka  70  ni  historia  ya  mafanikio, anasema  mhariri  wa  gazeti la  Pforzheimer Zeitung  anapozungumzia Israel  kutimiza  miaka  70 tangu  kuundwa  taifa  hilo. Mhariri  anasema:

"Waisrael  wamelifanya  jangwa kuweza  kutumika  tena  kama sehemu  ya  kilimo, wamefanikiwa  kutatua  matatizo  yao  ya  maji kwa  teknolojia  ya kisasa  ya  kuchuja  maji  ya  chunvi  na  ni viongozi  duniani  wa  maeneo  mengi  katika  teknolojia  ya kompyuta. Mamilioni  ya  wahamiaji  wamejumuishwa  katika  jamii ya  Kiyahudi. Lakini kuanzia  jana  baada  ya  kusherehekea kuundwa  kwa  taifa  hilo  kuna  picha  nyingine  ya  kumbukumbu. Dazeni  kadha  za  Wapalestina  wameuwawa na  idadi  kubwa  ya wengine  wamejeruhiwa, wanajeshi  wa Israel wenye silaha, matairi yanayochomwa  moto, na  wingu  la  mabomu  ya  kutoa  machozi."

Nalo  gazeti  la  Stuttgarter Nachrichten  linazungumzia  kuhusu wachezaji  wawili  wa  timu  ya  taifa  ya  Ujerumani Mesut Ozil  na Ilkay Gundogan  waliokutana  na  rais  wa  Uturuki Tayyip Erdogan. Mhariri  anaandika  kwamba  ingekuwa  bora  zaidi  kandanda likatenganishwa na  masuala  ya  kisiasa:

Mhariri  anaandika:

Erdogan mit Özil und Gündogan
Wachezaji wawili wa Ujerumani Ilkay Gundogan na Mesut Ozil (wakwanza na wa pili kutoka kushoto)wakiwa pamoja na rais wa Uturuki Erdogan(watatu kutoka kushoto)Picha: picture-alliance/dpa/Uncredited/Presdential Press Service

"Katika  hali  hii Mesut Ozil na  Ilkay Gundogan wamefanya kinyume chake, na  hii  ni  ishara  mbaya  kabisa. Iwapo  wamefanya  hivi kutokana  na  ujinga , ama  walifanya  hivi  kwa  kujitambua  na makusudi kabisa, hilo halina umuhimu hapa. Ukweli  ni  kwamba hawakuvuruga  tu ushindani  kati  ya  chama  cha  soka  cha Ujerumani  kuwania  kuwa  mwenyeji  wa  fainali  za  kombe  la mataifa  ya  Ulaya  mwaka  2024 , dhidi  ya  Uturuki , lakini  pia  nchi yao, ambayo  kwa  miaka  kadhaa wachezaji hao wamefanikiwa kucheza  kandanda na pia Ujerumani kumzuwia  Erdogan  kutokana na  sababu  muhimu kufanya  kampeni  ya  uchaguzi  wa  rais  hapo Juni  24  nchini  Ujerumani. Ozil  na  Gundogan  hadi  sasa  ni  mfano mzuri  wa  ujumuisho  katika  timu  ya  taifa  ya  Ujerumani. Kutokana hayo  waliyofanya, mtu anaweza  kujiuliza  iwapo  wachezaji  hao wanastahili  kuwamo  katika   kikosi  cha  timu  ya  taifa kinachokwenda  katika  fainali  za  kombe  la  dunia?"

Mwandishi: Sekione Kitojo / inlandspresse

Mhariri: Iddi Ssessanga