1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Magazetini Ujerumani

P.Martin8 Mei 2008

Miongoni mwa mada zilizogonga vichwa vya habari katika magazeti ya Ujerumani ni uamuzi wa Mahakama Kuu kuhusu wanajeshi wa Kijerumani na ndege za AWACS na sherehe za kuadhimisha miaka 60 tangu kuundwa taifa la Israel.

https://p.dw.com/p/DwdK

Tutaanza kwa maoni ya REUTLINGER GENERAL ANZEIGER kuhusu ndege za upelelezi-AWACS zilizotumwa na serikali iliyopita ya Ujerumani.

Gazeti hilo linasema,kimsingi wanajeshi wanaweza kupelekwa ko kote kushiriki vitani.Hasa katika vita kama ilivyokuwa hapo mwaka 2003,hata ikiwa ndege za AWACS wakati huo hazijaingia anga ya Iraq.Kufuatia uamuzi uliopitishwa na Mahakama Kuu ya Ujerumani,katika siku zijazo itakauwa vigumu sana kwa serikali ya Ujerumani kupeleka tena wanajeshi wake ko kote kule,bila ya kupata idhini ya Bunge.Serikali inaruhusiwa kuandaa mipango yake lakini hatua zingine zitakazofuta,zitahitaji kuidhinishwa na Bunge.

Tukiendelea na mada hiyo hiyo,gazeti la Thüringer Allgemeine linasema:

Uamuzi umepitishwa wakati ulio mwafaka hata ikiwa ulichukua muda mrefu.Kwani uamuzi huo utaathiri pendekezo lililotolewa hivi karibuni na serikali ya sasa kuhusu mfumo mpya wa usalama,ambao umezusha mabishano makali bungeni.

Kwa kweli,chama cha kiliberali cha FDP kiliposhtaki katika Mahakama ya Katiba miaka mitano iliyopita,kililenga serikali ya mseto ya wakati huo kati ya SPD na chama cha Kijani.Sababu ni kuwa hapo kabla serikali hiyo ilipinga vita vya Iraq vilivyoongozwa na Marekani lakini baadae wanajeshi wa Ujerumani walitumwa kushiriki katika ujumbe wa ndege za upelelezi za AWACS.Sasa ndio majaji wa Mahakama Kuu wameeleza waziwazi kuwa panapozuka hali ya kipekee,kimsingi ni Bunge na sio serikali inayoruhusiwa kufanya marekebisho.

Tukibadili mada ndio tunaligeukia MITTELDEUTSCHE ZEITUNG na sherehe za kuadhimisha miaka 60 tangu kuundwa kwa taifa la Israel.Gazeti hilo linasema:

"Kamwe hatutokuwa wahanga tena."Si taifa la Israel tu linalotamka maneno hayo bali Wayahudi wote duniani. Mananeo hayo si ukweli wa wale walionusurika maangamizi ya Wayahudi tu bali ni onyo na wajibu wa vizazi vyote vijavyo.Likiendelea gazeti hilo linasema,miaka 60 iliyopita kulikuwepo suala la kunusurika na leo hii ni kugombea kuona kuwa yale yaliyotokea kamwe hayatosahauliwa.

Kwa kumalizia tunalitupia jicho gazeti la GENERAL ANZEIGER la mjini Bonn:

Gazeti hilo likilalamika kuhusu vile serikali ya Myanmar inavyosita kuruhusu misaada ya kigeni kwa ajili ya watu walionasa sehemu za ndani linasema,hatua hiyo ya dharau waziwazi inaweza kuchochea kuangushwa kwa serikali hiyo ya kijeshi.Mateso makubwa ya umma hudhihirisha ile dharau ya serikali.

Uhaba wa misaada,kutotoa habari za kuwaonya wananchi mapema kuhusu kimbunga hicho kilichochukua maisha ya maelfu ya watu pamoja na kuzuia misaada ya kigeni katika sehemu za ndani,ni mambo yanayoonyesha jinsi serikali hiyo ya kijeshi ilivyoshindwa kuwahudumia wananchi wake.Hatimae,wananchi wa Myanmar watachoka kudharauliwa kama hivyo na serikali yao wenyewe lamalizia gaazeti la GENERAL ANZEIGER.