1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Magazetini Ujerumani

4 Januari 2010

Kama ilivyotarajiwa mada iliyotawala safu za mbele katika magazeti ya Ujerumani leo Jumatatu ni uamuzi wa serikali za Uingereza na Marekani kuisaidia Yemen kupambana na ugaidi nchini humo.

https://p.dw.com/p/LKjr

Vile vile mivutano katika serikali ya muungano ya Ujerumani kuhusu ahadi ya kupunguza kodi ya mapato inaendelea kugonga vichwa vya habari magazetini. Basi tutaanza na gazeti la NEUE OSNABRÜCKER linalouliza:

Je, Marekani inafungua uwanja mpya wa mapigano kukabiliana na ugaidi nchini Yemen? Je, kuna kitisho cha vita kwa sababu ya jaribio lililoshindwa kuiripua ndege ya Marekani? Ni wazi kabisa kuwa jawabu ni la. Hakuna haja ya kufungua uwanja mpya wa mapigano kwani tayari upo tangu miaka kadhaa. Kwa hivyo, wala haishangazi kuwa Mnigeria alietaka kuiripua ndege ya Marekani alipata mafunzo nchini Yemen. Vile vile si siri kuwa mtandao wa al-Qaeda una ngóme yake nchini Yemen. kwani hilo linajulikana tangu mwaka 2000 pale manowari ya Marekani USS Cole iliposhambuliwa katika bandari ya Aden - yaani kabla ya shambulio la Septemba 11 mwaka 2001 nchini Marekani.

Gazeti la SÄCHSISCHE ZEITUNG likiendelea na mada hiyo hiyo linasema:

Marekani ikifikiria kushambulia vituo vinavyosemekana kuwa ni vya al-Qaeda nchini Yemen, basi hiyo hufichua pia hali yake ya kufadhaika. Mabomu yanaweza kuteketeza kambi za mazoezi, lakini sio mawazo ya magaidi. Vile vile mashambulio ya anga daima huwaathiri wale wasiohusika. Bila shaka, hiyo husababisha baadhi ya umma kuwa na misimamo mikali na hukimbilia upande wa wachochezi wa itikadi kali.

Tukipindukia mada nyingine, gazeti la LANDESZEITUNG linagusia shambulio lililofanywa Aarhus nchini Denmark dhidi ya Westergaard ambae katika mwaka 2005 alichora katuni za Mtume Mohammad na kusababisha hasira kubwa miongoni mwa Waislamu katika nchi mbali mbali. Gazeti hilo linasema:

Shambulio lililofanywa dhidi ya Westergaard wala halishangazi. Kwani tangu alipochora katuni hizo miaka minne iliyopita, wachochezi wa chuki wametoa mwito wa kumuua raia huyo wa Denmark. Wakati huo, Waislamu wengi walihamakishwa na katunui hizo. Sasa nchi za Magharibi mara nyingine tena zinashuhudia kuwa wafuasi wa itikadi kali za Kiislamu wapo tayari kufanya cho chote kile katika vita vyao dhidi ya uhuru wa maoni katika ulimwengu wa Magharibi.

Mivutano ya kisiasa katika serikali ya muungano ya Ujerumani vile vile inaendelea kugonga vichwa vya habari magazetini na hasa kuhusu ahadi iliyotolewa na chama cha kiliberali FDP kinachoshiriki katika serikali hiyo ya muungano. NÜRNBERGER ZEITUNG linasema:

Waliberali wa chama cha FDP wamepania kutimiza ahadi yao kwa vyo vyote vile na hali serikali kuu,serikali za majimboni na mitaani zina madeni makubwa kwa sababu ya msukosuko wa uchumi na fedha. Lakini vyama shirika vya kihafidhina CDU na CSU vimegutuka - kwani kuambatana na katiba, serikali kuanzia mwaka 2011 inapaswa kupunguza madeni yake. Lakini ionekanavyo, chama cha FDP wala hakijali.

Kwa kumalizia NORDBAYERISCHE ZEITUNG linasema:

Katika kinyanganyiro cha madaraka, wanasiasa hawatambui jinsi walivyojitenga na shida za kila siku za wananchi. Chama cha CSU kikibishana kuhusu nyadhifa ya makamu wa kansela,umma unaohofia nafasi zao za ajira, unauliza iwapo wanasiasa hao hawana la kufanya?

Mwandishi:Martin,Prema/DPA

Mhariri: Othman,Miraji