1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Magazetini Ujerumani

17 Februari 2010

Mzozo wa madeni ya Ugiriki,mjadala mpya uliozuka kuhusu Hartz 4 yaani mpango wa serikali kuwasaidia watu wasio na ajira ni miongoni mwa mada zilizoshughulikiwa na wahariri wa magazeti ya Ujerumani leo Jumatano.

https://p.dw.com/p/M3kJ
Tutaanza na gazeti la SÄCHSISCHE ZEITUNG. Likiandika kuhusu mzozo wa Ugiriki inayokabiliwa na nakisi kubwa katika bajeti yake linasema: "Ugiriki hazukingilia tu uchumi wa Umoja wa Ulaya kwa sera zake za fedha bali kwa miaka imekuwa ikituma hesabu za uongo kuhusu hali halisi ya uchumi wake. Hata hivyo moja lijulikane : si Wagiriki waliofanya hayo bali ni serikali zilizokuwepo madarakani nchini Ugiriki. Lakini wanaoathirika na kulazimika kubeba mzigo wa madeni hayo ni Wagiriki wote. Hadi sasa maslahi ya Ugiriki yalikuwa yakizingatiwa na Umoja wa Ulaya. Lakini sasa Athens haina budi kuuzingatia Umoja wa Ulaya na hasa sarafu ya Euro. Na gazeti la NÜRNBERGER NACHRICHTEN likiendelea na mada hiyo hiyo linaandika: "Mkasa wa Ugiriki umedhihirisha kuwa umoja wa sarafu hautokamilika ilimradi Ulaya haitofanikiwa kuiachilia sera moja ya sarafu hatimae kuwa sera moja ya kifedha na kiuchumi. Sasa nchi za Ulaya hazina budi ila kuchukua hatua zinazohitajiwa kukabiliana na hali hiyo." Matamshi ya mwenyekiti wa chama cha kiliberali cha FDP Guido Westerwelle kuhusu Hartz 4 yaani malipo ya kuwasaidia watu wasio na ajira kwa muda mrefu, yamekosolewa vikali lakini yamezusha mdahalo muhimu linasema gazeti la RHEINZEITUNG na kuongezea: "Suala si kuwa mfanyakazi wa kawaida anapaswa kulipwa fedha zaidi kuliko yule anaepokea msaada wa Hartz 4 bali ni muhimu pia kuhakikisha kuwa walipa kodi hawatoathirika hata gharama za huduma za kijamii zinapoongezeka. Kwani gharama za Hartz 4 zikiendelea kuongezeka basi ni wazi kabisa kuwa haitowezekana kufanya hata mageuzi madogo katika mfumo wa malipo ya kodi. Chama cha FDP kinafahamu hilo vizuri, kwa hivyo linazidi kuhofia mradi wake unaotaka mageuzi katika sekta ya kodi na huduma za afya. Mtu anaweza kubishana kuhusu mradi huo wa FDP lakini ijulikane pia kuwa taifa linalozingatia maslahi ya jamii sasa linastahili kudurusiwa." Na kwa kumalizia, gazeti la TRIERISCHE VOLKSFREUND linaandika kuhusu wale wanaokwepa kulipa kodi ya mapato. "Hali ya wasiwasi imechomoza miongoni mwa watoro wa kodi nchini Ujerumani. Mamia kati yao wameanza wenyewe kuripoti katika taasisi husika ili hatimae wairejeshee serikali kodi na riba yake. Lakini huo si uadilifu - huo ni uoga tu wasije wakajulikana katika CD iliyo na majina ya wakwepa kodi" lamalizia TRIERISCHE VOLKSFREUND. Mwandishi:Martin,Prema/DPA Mhariri: Abdul-Rahman, Mohammed