1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Magazetini Ujerumani

19 Julai 2010

Mada iliyoshughulikiwa zaidi na wahariri wa magazeti ya Ujerumani leo Jumatatu, inahusika na kujiuzulu kwa Meya Ole von Beust wa Hamburg, kaskazini ya Ujerumani.

https://p.dw.com/p/OOpV
Hamburg's Buergermeister Ole von Beust gibt am Sonntag, 18. Juli 2010, im Rathaus in Hamburg seinen Ruecktritt bekannt. Er wird sein Amt zum 25. August 2010 nach neun Jahren niederlegen.(apn Photo/Joerg Sarbach) --- Hamburg's mayor Ole von Beust gives a statement in the town hall of Hamburg, Germany, July 18, 2010. Von Beust resigns after nine years as mayor.(apn Photo/Joerg Sarbach)
Meya wa Hamburg, Ole von Beust.Picha: AP

Basi tutaanza na gazeti la FRANKFURTER RUNDSCHAU linalosema:

"Ole von Beust hakuingilia hivyo sera za serikali kuu mjini Berlin. Lakini kuondoka kwake kutaleta athari zake kwa Kansela Angela Merkel. Kwani kujizulu kwa mwanasiasa huyo ni ishara kuwa sio msingi pekee, bali hata mtazamo wa sera za Merkel unasambaratika."

Kwa maoni ya FRANKFURTER RUNDSCHAU:

"Hakuna mwanasiasa ye yote yule anaeweza kulinganishwa na mhafidhina huyo wa kimamboleo, alieweza kuwavutia wapiga kura wengi katika jiji la Hamburg. Meya huyo alikiri kuwa siku za hivi karibuni ameelekea mrengo wa kushoto na anazingatia zaidi mazingira.Huo ni mkondo wa kimamboleo unaotakiwa na Merkel kwa chama chake."

Mhariri wa gazeti la BERLINER ZEITUNG akiendelea na mada hiyo hiyo anasema:

"Chama cha kihafidhina cha CDU na chama cha Kijani cha walinzi wa mazingira, vilipounda serikali ya muungano katika jiji la Hamburg, jaribio hilo lilifungua njia mpya, badala ya muungano wenye mvutano pamoja na chama cha kiliberali cha FDP. Hata hivyo ,serikali hiyo yenye muundo mpya, ilipoteza umaarufu wake kufuatia matukio mbalimbali.

Kwa mfano, kashfa iliyozuka wakati wa majira ya baridi kali na kusababisha matatizo makubwa kwa wakaazi, kuongezwa kwa ada katika vituo vya kuwatazama watoto,migomo ya shule, na gharama kubwa za kujenga jumba la utamaduni, ni baadhi ya mambo yaliyopunguza umaarufu wa serikali. Na sasa, waziri mkuu wa Hamburg amejiuzulu. Si rahisi hivyo kuwaleta pamoja wahafidhina na waliberali wanaotetea mazingira. Huo ni ujumbe wa kutisha unaokwenda kwa Kansela Merkel."

Gazeti la NÜRNBERGER NACHRICHTEN linaaandika hivi:

"Mawaziri wakuu sita wa chama kimoja, wameondoka katika kipindi cha mwaka mmoja - wengine hawakuchaguliwa na wengine wameacha kazi wenyewe. Hiyo, haijawahi kutokea katika historia ya Shirikisho la Jamhuri ya Ujerumani. Na eti, hakuna kinachoweza kufanywa na Kansela Merkel. Hiyo si sahihi, kwani yeye ni mwenyekiti wa chama cha CDU kwa hivyo, anawajibika kwa yote yanayotokea katika chama hicho, hata kuhusu viongozi wanaokimbia madaraka yao kiholela."

Kwa kumalizia tunabadilisha mada na tunatupia jicho uhariri wa gazeti la MAIN POST linalosikitika hivi:

"Kinachohuzunisha zaidi ni kuwa sio tu habari kuhusu matatizo ya kupambana na ukimwi zinazopungua kupewa kipaumbele na vyombo vya habari, bali hata jitahada za jumuiya ya kimataifa kupiga vita ugonjwa huo zinapungua. Lengo la Umoja wa Mataifa kuwapatia matibabu wagonjwa wote wa ukimwi ifikapo mwaka 2010 halikutekelezwa. Bado watu milioni 10 walioambukizwa virusi vya ukimwi wangali wakingojea kupata dawa zinazoweza kuokoa maisha yao.

Mwandishi: P.Martin/DPA

Mhariri:Charo,Josephat