1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Magazetini Ujerumani

27 Julai 2010

Maafa yaliyotokea kwenye tamasha la muziki "Love Parade" mjini Duisburg ni mada inayoendelea kugonga vichwa vya habari katika magazeti ya Ujerumani, huku masuala mengi yakingojea jawabu.

https://p.dw.com/p/OVc3

Basi tutaanza na gazeti la MAIN POST linalouliza:

"Kwanini wakuu wa mji huo waliruhusu tamasha hilo kuandaliwa, na hali kulikuwepo wasiwasi kuhusu utaratibu wa usalama kama inavyodaiwa? Uwazi na ukweli, ndio kinachotarajiwa hivi sasa kutoka kwa waandalizi wa tamasha hilo wanaokosolewa. Wao wanawajibika kufanywa hivyo, sio kwa ajili ya wahanga pekee."

Na CELLESCHE ZEITUNG likiendelea na mada hiyo hiyo linasema:

"Wataalamu wa masuala ya usalama wanaeleza kuwa kwenye tamasha kubwa huwepo uwezekano wa kuzuka hali ya hatari.Hiyo haiwezikuepukwa, hata kama zimechukuliwa hatua madhubuti za usalama. Lakini wakati huo huo, umma unaohudhuria tamasha la muziki kama vile Love Parade, mahubiri ya kanisa au mashindano ya kandanda, una haki ya kuhakikishiwa usalama wao."

Kwa maoni ya WESTDEUTSCHE ZEITUNG, Meya Mkuu wa Duisburg, Adolf Sauerland hana tena cha kufikiria - kilichobaki ni kuondoka madarakani. Linaongezea:

"Hiyo ndio hatua pekee ya kuchukuliwa, kufuatia maafa yaliyosababisha vifo vya watu 20 katika mji wake. Hilo ni suala la maadili, kwani hata kabla ya waendesha mashtaka kueleza nani anaewajibika kisheria kuhusu maafa yaliyotokea, kuna kile kinachoitwa udailifu wa kisiasa. Na anaewajibika kisiasa ni mkuu wa maafisa wanaowajibika na maafa yaliyotokea."

Nyaraka za siri kuhusu Afghanistan, zilizovuja katika mtandao wa Wikileaks ni mada nyingine iliyoshughulikiwa na magazeti ya Ujerumani leo Jumanne. Gazeti la DER NEUE TAG linasema:

"Maelfu kwa maelfu ya nyaraka zilizovuja, hazitobadili mtazamo kuhusu vita vya Afghanistan. Lakini umma wa Ujerumani uliokuwa na mashaka yake kuhusu vita hivyo kwa sababu ya taarifa mbali mbali, sasa utazidi kuwa na picha tofauti. Yaani, vita vya Afghanistan vinazidi kumuaga damu ya washirika na maadui; na itazidi kuwa hatari kwa wanajeshi wa Ujerumani. Sasa itakuwa vigumu zaidi kwa serikali za nchi zinazoshiriki katika vya Afghanistan kuikanusha hali hiyo."

Kwa maoni ya gazeti la BADISCHE ZEITUNG:

"Hakuna haja ya kuiandika upya historia ya vita vya Afghanistan. Kwani habari za kugongana zilizopatikana hadi hivi sasa, hazikufichuliwa na jarida la Spiegel au magazeti ya New York Times na Guardian. Juu ya hivyo ionekanavyo hali ni mbaya kuliko ilivyodhaniwa. Kuna operesheni nyingi zaidi za siri: wahanga zaidi wa kiraia, kuna udhaifu mkubwa na maendeleo madogo."

Lakini kinachoshtusha zaidi ni kuwa Wataliban wamejizatiti vizuri sana kwa silaha na wanasaidiwa na idara ya ujasusi ya Pakistan lamalizia BADISCHE ZEITUNG:

Mwandishi: P.Martin/DPA

Mhariri: Charo,Josephat