1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Maoni ya wahariri

Mtullya, Abdu Said27 Machi 2008

Katika maoni leo wahariri wa magazeti ya Ujerumani wanazungumzia juu ya pendekezo la kupunguza kodi ya mauzo ili bei ya nishati iwe nafuu.

https://p.dw.com/p/DVUq
Mwenyekiti wa chama cha waliberali FDP Ujerumani bwana Guido Westerwell.Picha: AP



Nishati ni miongoni mwa mahitaji ya msingi ya mwanadamu sawa na chakula na maji.

Na kutokana hayo nishati inapasa kupatikana kwa bei nafuu kwa wananchi wote. Hilo ndilo suala linalozingatiwa leo katika maoni ya wahariri wa magazeti ya Ujerumani.

Wahariri hao wanatoa maoni yao kufuatia pendekezo la mwenyekiti wa chama cha waliberali FDP bwana Guido Westerwelle juu ya  kupunguza kodi ya mauzo ili kuifanya  bei ya nishati iwe nafuu kwa wananchi wote.

Bwana Westerwelle amependekeza kupunguzwa kodi hiyo kutoka asiliamia 19  hadi asilimia 7.

Lakini  gazeti la KÖLNER STADT ANZEIGER halioni hilo kuwa wazo la kufaa sana.

Sababu  ni kwamba  haitachukua muda kwa makapuni ya nishati kupandisha bei kwa kisingizio cha kuongezeka bei  ya nishati kwenye  masoko ya kimataifa. Mhariri wa gazeti hilo KÖLNER STADT ANZEIGER anasema kitakachotokea baada ya kuteremsha  kodi ya mauzo(VAT) , ni kupungua mapato ya kodi kwenye mfuko wa  serikali.


Wazo la kupunguza  kodi ya mauzo linapingwa pia na mhariri  wa gazeti la WESTFÄLISCHE NACHRICHTEN kutoja mji wa Münster katika jimbo la kaskazini magharibi mwa Ujerumani.

Mhariri huyo anasema pendekezo la mwenyekiti wa chama cha waliberali bwana  Westerwelle ni mzaha. Gazeti linasema pendekzo la kupungza bei ya gesi na umeme linavutia lakini alietoa wazo hilo analenga shabaha ya kujijengea  umaaruf tu. Mhariri wa gazeti hilo   anauliza vipi itawezekana kuziba shimo  lililopo katika mfuko wa serikali, ikiwa  mapato ya kodi yatapungua?

Mhariri huyo anasema ipo jia moja tu ya kuweza kuondokana na bei za juu za mahitaji ya nishati. Nayo ni kufanya mageuzi kwenye masoko ya nishati hapa nchini Ujerumani.

Lakini mhariri wa gazeti la OFFENBACH POST  anasema mtu anaweza kudhihaki pendekezo  la mwenyekiti huyo wa chama cha FDP iwapo  ataliangalia kijuu juu,  lakini akiwa na wasaa wa kulichunguza  kwa undani atabaini kuwa,lina  maana. Mhariri huyo anauliza kwa nini kiwango cha chini cha kodi ya mauzo kinatozwa katika mapato yanayotokana na mbio za farasi,wakati kodi inayotokana na mauzo ya nepi za watoto ni ya juu. 

Gazeti linasema ikiwa kodi ya mauzo itapunguzwa katika gesi na umeme - jambo hilo litaingia akilini. Hatua hiyo ingeleta haki ya kijamii.

Mhariri wa gazeti la PFORZHEIMER anaunga mkono hoja hiyo kwa kusema kuwa bei ya nishati imethibiti kuwa kizingiti kirefu katika ustawi wa uchumi nchini  Ujerumani.

Mhariri huyo anasema kila mwananchi anapaswa kumudu kulipia mahitaji yake ya nishati, badala ya nishati kuleta manufaa  kwa serikali peke yake.