1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mageuzi ya Ugawaji wa Ardhi Kusini mwa Afrika

P.Martin18 Agosti 2008

Kinyume na Zimbabwe inayokabiliwa na matatizo katika utaratibu wa ugawaji wa ardhi,huko Afrika Kusini na Nambia kuna ishara zinazotoa matumaini.

https://p.dw.com/p/F018

Changamoto ya hivi sasa katika nchi hizo ni kujifunza njia ya kuhakikisha kuwa wakulima waliogaiwa ardhi, watajipatia rizki yao.

Nchini Zimbabwe,mashamba 150,000 madogo na mashamba makubwa ya kibiashara 15,000 yalipata wamiliki wapya kufuatia maguezi ya kugawa upya ardhi kwa haraka.Mageuzi hayo yalifanywa bila ya mpangilio na mara nyingi kulitumiwa nguvu.Wakulima wengi wa kizungu walilazimika kuondoka kwa sababu ya kuhofia maisha yao.

Lakini nchini Afrika Kusini na Nambia ugawaji upya wa ardhi unafuata utaratibu maalum.Kwa mfano Afrika Kusini watu wanapeleka maombi ya kurejeshewa ardhi yao ikiwa wana madai ya kihistoria kwa sababu walifukuzwa miongo au karne kadhaa zilizopita.Njia nyingine ni kuomba msaada wa serikali kuwapatia ardhi.

Hata hivyo Afrika Kusini pia kuna mifano ambako sera ya mageuzi ya ardhi haikufanikiwa.Kwani kuna watu walionunua ardhi lakini walipoona hawafanikiwa moja kwa moja walijiamulia kuondoka na ni wachache tu waliobakia mashambani.Hata miongoni mwa wakulima hao wapya wengine wameshindwa kupanda cho chote na wamekaa na mashamba yao.Sababu ni gharama kubwa za ukulima na vile vile matatizo tofauti ya kilimo ambayo hawakutazamia.Wengine ndio walipoteza kabisa hamu ya kulima kwa sababu ya kukosa msaada wa serikali.

Kwa maoni ya Ben Cousins alie mkurugenzi wa mipango ya utafiti wa ardhi na kilimo kwenye Chuo Kikuu cha Western Cape Afrika Kusini,kuna sababu nyingi zilizosababisha hali hiyo.Kama vile uhaba wa uandalizi na kutokuwepo mipango ya kuendeleza ujuzi au kuwasaidia wakulima kununua mbolea,mbegu na kumwagilia maji mashamba.Vile vile hakuna miundombinu inayoweza kutumiwa kusafirisha mazao sokoni.

Nchini Namibia pia wakulima waliofanikiwa ni wachache mno kulinganishwa na wale walioshindwa. Muda mfupi tu baada ya nchi hiyo kujipatia uhuru wake mwaka 1990,kulifanywa mkutano wa kitaifa kuhusu mageuzi ya ardhi.Mkutano huo uliweka msingi wa utaratibu wa amani wa mageuzi ya ardhi. Lakini kwa maoni ya mtaalamu wa mageuzi ya ardhi Willem Odendaal,utaratibu huo unakwenda pole pole mno kwa wengi.Namibia ni nchi kame kwa hivyo wakulima wengi hupendelea kuwa na mifugo.

Lakini ruzuku za wakulima zimepunguka na wakati huo huo mashindano yanazidi kuwa makubwa katika masoko ya duniani.Kwa hivyo sasa,hata wakulima wa zamani wamevunjika moyo na hawaoni sababu ya kuendelea na kilimo.Kwa mujibu wa Odendaal,serikali ina mipango michache mno kuwasaidia wakulima wapya.Licha ya matatizo yote kuna wengi waliofanikiwa kuanzisha maisha mapya.Kwao,kilicho muhimu ni kuwa sasa wana uhuru wa kujifanyia kazi wenyewe.