1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Magoli mengi yafungwa katika hatua ya makundi

27 Juni 2014

Ni wazi kuwa wachezaji mahiri wa soka ulimwenguni walibeba njumu zao za kufunga magoli wakati wakielekea Brazil kwa Kombe la Dunia. Jumla ya magoli 136 yametiwa kimyani katika mechi 48 za awamu ya makundi

https://p.dw.com/p/1CRXq
Fußball WM 2014 Honduras Schweiz
Picha: Getty Images

Tekenlojia ya kubainisha kama mpira umevuka mstari wa lango imetumiwa kuthibitisha matukio kadhaa kufikia sasa, lakini lazima tukubali kuwa nyavu katika viwanja mbalimbali vya Brazil zimekuwa zikiraruliwa katika kipindi cha wiki mbili zilizopita.

Washindani 32 wa Kombe la Dunia walifunga karibu magoli matatu katika kila mchezo kwa kiwango cha wastani katika duru ya kwanza, ikilinganishwa na kiasi cha chini ya magoli mawili kwa kila mchezo (jumla ya 93) katika awamu hiyo nchini Afrika Kusini miaka minne iliyopita.

Rekodi za ufungaji mabao zimevunjwa. Algeria ndio timu ya kwanza ya Afrika kufunga manne, Asamoah Gyan ndiye mfungaji bora barani Afrika kwa kufunga magolo sita katika Kombe la Dunia, wakati Miroslav Klose wa Ujerumani ametoshana na Ronaldo wa Brazil kwa kufunga magoli 15.

Fußball WM 2014 Brasilien Kamerun Neymar
Mshambuliaji wa Brazil Neymar anaendelea kutikisa nyavuPicha: Reuters

Lakini juhudi za Klose kujaribu kuipiku rekodi ya Ronaldo huenda ikawa kibarua kigumu, ukilinganisha na kiwango cha mwenzake chipukizi Thomas Müller. Mjerumani huyo mwenye umri wa miaka 24 ambaye alifunga goli la ushindi dhidi ya Ujerumani, na mabao matatu dhidi ya Ureno, ana magoli tisa ya Kombe la Dunia. Müller hivyo basi alimpiku Diego Maradona wa Argentina na Mjerumani mwenzake Rudi Völler katika mechi ya Alhamisi.

Lionel Messi, Neymar na Arjen Robben ambao wanatamba sana katika timu za Argentina, Brazil na Uholanzi, wamezibeba timu zao kwa kufunga magoli manne kila mmoja. Xherdan Shaqiri wa Uswisi, Robin Van Persi wa Uholanzi, James Rodriguez wa Colombia wana matatu kila mmoja na wana kila dalili za kuendelea kutikisa nyavu za wapinzani.

Na dimba hili kufikia sasa halijakosa kuwashangaza wengi na nampisha mwenzangu Anuary Mkama akueleze namna ambavyo vigogo wa Ulaya walivyofunga virago vyao mapema kuelekea makwao baada ya majahazi yao kuzama..

Mwandishi: Bruce Amani/AFP/DPA
Mhariri:Mohammed Abdul-Rahman