1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mahakama Afrika Kusini yalitaka bunge kumuwajibisha Zuma

29 Desemba 2017

 Mahakama ya Katiba imepigilia msumari wa mwisho kuhusu kashfa  inayomkabili Rais wa nchi hiyo, Jacob Zuma, ya kutumia fedha za umma kukarabati makazi yake kwa kulitaka bunge kumuwajibisha.

https://p.dw.com/p/2q6pm
Südafrika Kapstadt Jacob Zuma Präsident Anhörung Parlament
Rais Jacob Zuma, akijibu maswali ya wapinzani bungeni mnamo mwaka 2015. Picha: picture-alliance/dpa/N. Bothma

Mahakama ya Katiba ya Afrika Kusini, imetoa uamuzi  huo leo na kusema  kuwa bunge lilishindwa kumwajibisha Rais Jacob Zuma kutokana na kashfa ya kutumia fedha za umma, kukarabati makazi yake binafsi, ya Nkandla. Hivyo mahakama imetaka bunge kuanza mchakato wa kumtoa madarakani kiongozi huyo.

 Uamuzi huo ni pigo la mwisho  la kimahakama, katika kashfa  inayomkabili Zuma, ambaye pia anakabiliwa na shinikizo kubwa kutoka kwa umma akitakiwa kujiuzuliu wadhifa wake katika nchi hiyo iliyo na neema ya uchumi wa viwanda, kabla ya uchaguzi wa 2019.  Hata hivyo haikuwekwa wazi mara moja ni hatua gani bunge litachukua.

Akitoa uamuzi huo leo, Jaji Chris Jafta alisema wamejiridhisha kuwa bunge halikutimiza wajibu wake. Uamuzi huo uliungwa mkono na wengi mahakamani hapo na ulionyeshwa mubashara katika luninga.

"Kwa  mtazamo wetu, mchakato wa suala hilo haukuendana na kifungu cha 89. Bunge lilijadili  na kuchagua kupiga kura ya kutokuwa na imani.-halikujiridhisha kuwa uvunjwaji wa katiba, katika suala hilo, ulikuwa umejikita katika kutafakari   kifungu hicho. Hivyo basi, tunahitimisha kuwa bunge halikuweza kumwajibisha rais kutokana na makosa yake kama inavyotakiwa katika kifungu cha 89,``alisema

Südafrika Privatbesitz von Jacob Zuma Staatspräsident
Muonekano wa makazi ya Nkandla ya Rais wa Afrika Kusini, Jacob Zuma. Picha: Reuters/R. Ward

Jafta alisema imeelezwa vyema, katika kifungu cha 89 kinachodokeza wajibu wa bunge kutunga sheria hasa zile za kumuondoa rais madarakani.  Akaongeza kuwa kwa kushindwa kujumuisha sheria hizo,  bunge limeshindwa kutimiza wajibu wake.

Chama cha mrengo wa kushoto cha Economic Freedom Fighter, na vyama vidogo vya upinzani, ndivyo vilivyopeleka suala hilo katika mahakama ya katiba.

Zuma, yupo katika nafasi  mbaya kwa sasa, baada ya makamu wa rais  Cyril Ramaphosa, kupata ushindi mwembamba na kupata  nafasi ya kukiongoza chama tawala cha Zuma, ANC wiki iliyopita. Hata hivyo  bado Zuma ana nafasi muhimu katika chama hicho na tayari alishapenya katika kura za kutokuwa na imani naye.

 Wakati huo huo, ANC imetoa taarifa na kusema kuwa kitapitia uamuzi huo na kujadili  madhara yake katika kikao cha Kamati kuu ya chama hicho,   kitakachofanyika, Januari 10, 2018.

Tangu Ramaphosa achaguliwe, randi ya Afrika  Kusini imekuwa dhabiti  katika siku za mwisho za mwaka. Imepanda kwa zaidi ya asilimia 10 dhidi ya dola.

 Mwandishi: Florence Majani(Reuters)

Mhariri: Iddi Sessanga