1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mahakama Kuu ya Ujerumani yasema ni sahihi kisheria kwa serikali kuisaidia Ugiriki na nchi nyingine zenye madeni.

Abdu Said Mtullya7 Septemba 2011

Ni sahihi kisheria kwa Serikali ya Ujerumani kuzisaidia nchi zenye madeni katika Umoja wa sarafu ya Euro. Yasema Mahakama Kuu ya Ujerumani.

https://p.dw.com/p/12UKw
Mahakimu wa Mahakama Kuu ya Ujerumani mjini Karlsruhe.Picha: picture-alliance/dpa

Mahakama Kuu ya Ujerumani leo imeyakataa madai yaliyowasilishwa na wataalamu kadhaa wanaopinga kushiriki kwa serikali ya Ujerumani katika mpango wa kuziokoa nchi zenye madeni makubwa katika Umoja wa nchi zinatotumia sarafu ya Euro. Lakini Mahakama hiyo imesema kwamba serikali ya Ujerumani inapaswa kupata kibali cha Bunge.

Kushiriki kwa serikali ya Ujerumani katika mpango wa kuiokoa Ugiriki na nchi nyingine zilizotingwa na madeni ni hatua halali kisheria. Mahakama Kuu ya Ujerumani iliutoa uamuzi huo muda mfupi uliopita mjini Karlsruhe kusini magharibi mwa Ujerumani.

Kwa kuutoa umauzi huo Mahakama hiyo imeyakataa madai yaliyowasilishwa na jopo la wataalamu kadhaa wa Ujerumani kusaili uhalali wa hatua ya Ujerumani ya kushiriki katika kuziokoa nchi zenye matatizo ya madeni katika jumuiya ya sarafu ya Euro.

Akuitoa uamuzi huo mapema leo Hakimu Mkuu Andreas Voßkuhle alitamka kuwa sheria inayowezesha mpango wa kuisadia Ugiriki katika Umoja wa sarafu ya Euro ni halali na kwamba mpango wa kuziokoa nchi nyingine za Umoja huo haukiuki sheria ya uchaguzi inayotokana na ibara ya 38 ya kifungu cha kwanza cha sheria kuu.

Mahakama Kuu ya Ujerumani imeamua kwamba mchango wa Ujerumani katika kuzisaidia, Ugiriki na nchi nyingine na hasa Ireland na Ureno unawafiki na katiba ya Ujerumani. Hata hivyo Mahakama hiyo imesema kuwa Bunge la Ujerumani linapaswa kuwa na usemi mkubwa juu ya hatua zitakazochukuliwa na serikali katika siku za usoni. Uamuzi huo ulikuwa unasubiriwa na masoko yote ya fedha yaliyokuwa na wasi wasi mkubwa katika nchi 17 zinazotumia sarafu ya Euro.

Wataalamu wa sheria na wa uchumi nchini Ujerumani pamoja na watu wanaoutulia mashaka Umoja wa Ulaya waliyawasilisha madai yao kwenye Mahakama ya mjini Karlsruhe kuitaka itafakari iwapo ni halali kisheria kwa Ujerumani kushiriki katika mpango wa kuikoa Ugiriki na nchi nyingine zinazokabiliwa madeni makubwa barani Ulaya. Watu hao walisema katika mashtaka yao kwamba kushiriki kwa serikali ya Ujerumani katika kuiokoa Ugiriki na nchi nyingine zenye madeni ni kinyume na mikataba ya Ulaya na kunakiuka udhibiti wa bunge wa fedha za walipa kodi.

Miongoni mwa watu mashuhuri waliowasilisha mashtaka hayo ni mtaalamu wa uchumi ,Joachim Starbatty aliesema kuwa kuyaweka kando mamlaka ya Bunge juu ya bajeti ili kuweza kuepusha hatari inayoikabili sarafu ya Euro hakuwezi kuwa lengo la maendeleo ya Ulaya. Mtaalamu huyo amesema serikali ya Ujerumani iliipitisha bungeni kwa haraka sheria juu ya kuzisaidia nchi zenye madeni kiasi kwamba wabunge hawakuwa na muda wa kutosha wa kuitafakari sheria hiyo.

Mnamo mwezi wa mei bunge la Ujerumani liliridhia kiasi cha Euro Bilioni 22.4 kwa ajili ya kuidhamini Ugiriki. Ujerumani pia imeshiriki katika kuchangia katika mfuko wa kuziokoa nchi nyingine kwa kiasia cha Euro Bilioni 123.

Mwandishi/Mtullya Abdu/ZA/

RTRE/

Mhariri/ Othman Miraji