1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Iran kupinga vikwazo vya Marekani mahakama ya ICJ

Yusra Buwayhid
27 Agosti 2018

Iran Jumatatu itapinga vikwazo vipya ilivyowekewa na Marekani mbele ya Mahakama ya Kimataifa ya Haki. Marekani aliiwekea Iran vikwazo vipya licha ya kuondolewa kufuatia makubaliano ya nyuklia ya mwaka 2015.

https://p.dw.com/p/33otT
Symbolbild Kündigung Atomabkommen mit Iran durch USA
Picha: Imago/Ralph Peters

Wanasheria wanaoiwakilisha Iran wataitaka Mahakama ya Kimataifa ya Haki (ICJ) hii leo kuiamuru Marekani kuondoa vikwazo vilivyowekwa na serikali ya Rais Donald Trump dhidi ya Iran. Wanasheria wa upande wa Marekani wanatarajiwa kuwasilisha kesi yao mbele ya mahakama hiyo hapo kesho.

Trump aliyaeleza makubaliano ya nyuklia ya mwaka 2015 kati ya Iran na wajumbe watano wa kudumu wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa ikiwamo Ujerumani, kuwa ni ya kushtusha na yanayoelemea upande mmoja, na pia hayakufanikiwa kufikia lengo la msingi la kuzuia njia zote za kuiwezesha Iran kutengeneza bomu la nyuklia.

Amri ya rais Trump imesema kwamba vikwazo hivyo vitaiongezea shinikizo la kiuchumi Iran na kuifanya kuwa tayari kufikia suluhisho la kudumu juu ya shughuli zake ambazo jumuiya ya kimataifa haikuzitilia manani wakati wa makubaliabno yao, kama vile mpango wa Iran wa kutengeneza makombora ya msafa marefu na ufadhili wake kwa makundi ya kigaidi.

USA Donald Trump zum Atomdeal mit Iran
Rais wa Marekani Donald Trump akizungumza na maripota baada ya kusaini kujiondoa katika makubaliano ya nyuklia na Iran. Mei 8, 2018.Picha: Reuters/J. Ernst

Ingawa wajumbe wote waliosaini makubaliano hayo ya nyuklia na Iran waliishauri Marekani isijitoe, Trump hakuwasikiliza, alijitoa na kutangaza kuwa ataiwekea tena vikwazo Iran.

Duru ya pili ya vikwazo hivyo dhidi ya Iran inategemewa kutekelezwa na Marekani mapema mwezi Novemba, ambavyo vitalenga sekta zake muhimu za mafuta na nishati.

Marekani haina haki ya kuiwekea vikwazo Iran

Iran iliwasilisha kesi yake mbele ya Mahakama ya Kimataifa ya Haki (ICJ) mwishoni mwa mwezi Julai, ikiwataka majaji wa mahakama hiyo iliyopo mjini The Hague, Uholanzi kuamuru kuondolewa vikwazo hivyo mara moja.

Iran imeongeza kwamba Marekani haikuwa na haki ya kurejesha vikwazo hivyo, na imeomba kupewa fidia kwa uharibifu uliotokana na hatua hiyo ya Trump.

Mahakama ya ICJ iliyoanzishwa mwaka 1946 kutatua mizozo kati ya nchi, inatarajiwa kutumia miezi kadhaa ili kutoa uamuzi wa muda mfupi kuhusu madai ya Iran, wakati uamuzi wa mwisho wa kesi hiyo unaweza kuchukua miaka kadhaa.

Iran - ambayo inasema hatua hiyo inakiuka Mkataba wa 1955 wa Uhusiano wa Kiuchumi kati ya mataifa hayo mawili - inalalamika kuwa vikwazo hivyo vipya tayari vinaathiri uchumi wake. Sarafu ya Iran rial imepoteza nusu ya thamani yake tangu Aprili.

Mahakama ya ICJ mpaka sasa imesema mkataba wa 1955 bado ni halali, hata kama uliwekwa saini kabla ya Mapinduzi ya Kiislam ya mwaka 1979 ya nchini Iran yaliosababisha uhasama wa miongo kadhaa na Marekani.

Mwandishi: Yusra Buwayhid/afp/rtre

Mhariri: Josephat Charo