1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mahakama ya Juu Kenya yamzuwia rais kubadili katiba

Mohammed Khelef
14 Mei 2021

Mahakama ya Juu nchini Kenya imeamua kwamba mageuzi ya kikatiba yanayopigiwa debe na Rais Uhuru Kenyatta na kiongozi mkuu wa upinzani, Raila Odinga ni kinyume na sheria, uamuzi unaompa nguvu Naibu Rais William Ruto.

https://p.dw.com/p/3tMk1
Kenia Präsident Uhuru Kenyatta und Oppositionsführer Raila Odinga in Nairobi
Picha: Reuters/T. Mukoya

Kwenye uamuzi wake wa Alkhamis (Mei 13), Mahakama hiyo ilisema rasimu ya sheria ya mabadiliko ya katiba, maarufu kama Building Bridge Initiatives (BBI), ni hatua binafsi ya Rais Kenyatta ambaye hana mamlaka ya kisheria kuanzisha mchakato wa mabadiliko yoyote ya kikatiba kupitia uhamasishaji wa umma. 

Mpango huo ambao umeligawa taifa hilo la Afrika Mashariki kisiasa, unapendekeza kuuondowa mfumo wa mshindi wa uchaguzi kuchukuwa kila kitu, jambo ambalo Rais Kenyatta anasema limechochea migogoro ya kila baada ya uchaguzi. 

Tayari bunge la taifa lilishayapitisha marekebisho yaliyopendekezwa ambayo yanaashiria mabadiliko makubwa kabisa kwenye mfumo wa serikali tangu katiba mpya kupitishwa mwaka 2010.

Lakini wakitowa uamuzi kutokana na mapingamizi kadhaa yaliyowekwa na makundi mbalimbali nchini Kenya, majaji watano wa Mahakama hiyo ya Juu walisema "Kenyatta alitumia kipengele cha katiba kilichowekwa kwa ajili ya raia kuanzisha mabadiliko hayo", na hilo linaifanya hatua yake kutokuwa na uhalali wa kisheria. 

"Rais hawezi kuwa mchezaji na muamuzi kwa wakati mmoja." Alisema Jaji Jairus Ngaah akisoma uamuzi huo

Serikali, ambayo inataka kuitisha kura ya maoni baada ya Kenyatta kuusaini muswaada huo kuwa sheria, ilisema ingeliukatia rufaa uamuzi huo wa Mahakama ya Juu.

Ushindi kwa Ruto?

Kenia Uhuru Kenyatta  William Ruto
Rais Uhuru Kenyatta (kushoto) na naibu wake, William Ruto, ambaye anapingana vikali na mabadiliko ya katiba.Picha: Getty Images/AFP/T. Karumba

Kenyatta anasema muswaada huo unapigania mfumo wa ugawanaji madaraka kati ya makundi ya kikabila yenye uhasimu mkubwa wa kisiasa ili kupunguza kurejelewa kwa ghasia za uchaguzi na anakanusha kwamba unamlenga mtu mmoja mahsusi.

Kama ukiwa sheria, utaunda majimbo mapya 70 ya uchaguzi, kurejesha jukumu la mawaziri kwa wabunge wa kuchaguliwa na kuunda nyadhifa kadhaa za juu na zenye nguvu: akiwemo waziri mkuu, manaibu wake wawili na kiongozi rasmi wa upinzani bungeni.

Kenyatta alianzisha mabadiliko hayo akiungwa mkono na Waziri Mkuu wa zamani, Raila Odinga, baada ya wawili hao kupatana mwezi Januari 2018 kufuatia uchaguzi uliokuwa na ushindani mkali, ambao Kenyatta alimshinda tena Odinga.

Hata hivyo, mchakato mzima ulionekana kumtenga Naibu Rais William Ruto, ambaye anataka kumrithi bosi wake atakapostaafu mwakani baada ya kuhudumu vipindi viwili vya miaka mitano mitano.

Mmoja wa wapinzani wa rasimu hiyo, John Githongo, ameliambia shirika la habari la Reuters kwamba mageuzi hayo ya katiba kwa sehemu yamefanywa ili kuivunja ndoto ya kisiasa ya Ruto, kwa kufanya iwe rahisi kuunda muungano wa kisiasa dhidi yake.

Wafuasi wa Ruto wamekuwa wakiyapinga waziwawi mabadiliko hayo ya katiba ndani na nje ya bunge, wakisema kuwa "Kenya haina tatizo la kikatiba, bali la kiuchumi."