1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mahakama ya juu ya Ujerumani yahakikisha juuya uhuru wa magazeti hapa nchini.

27 Februari 2007

Jarida linalotoka kila mwezi hapa Ujerumani, Cicero, mwezi April mwaka 2005 lilichapisha makala kuhusu gaidi aliyekuwa anafuata siasa za itikadi kali za Kiislamu, Abu Musab al-Zarkawi. Ndani ya makala hayo ilinukuliwa kwa undani taarifa iliokuwemo ndani ya mafaili ya idara ya upelelezi ya hapa jerumani, BKA.

https://p.dw.com/p/CHJF
Jarida la Der Spigel la Ujerumani
Jarida la Der Spigel la Ujerumani

Matokeo ya kitendo hicho ni kwamba idara ya uhariri wa jarida hilo pamoja na nyumba ya kibinafsi ya mwandishi wa makala hayo, Bruno Schirra, zilisachiwa. Sababu iliotajwa ya kufanywa upekuzi huo ni kwamba kwa kuchapishwa taarifa hiyo ya siri, mwandishi alisaidia katika uhaini wa kutoa hadharani siri za serekali. Lakini mahakama ya kikatiba ya hapa Ujerumani mjini Karlsruhe, korti ya juu kabisa hapa nchini, ilitangaza jana kwamba upekuzi huo ulikuwa ni kinyume na katiba. Uamuzi huo sio tu umeimarisha uhuru wa magazeti.

Ulrike Mast-Kirschning ameandika yafuatayo; maoni yake yanasomwa studioni na Othman Miraji…

Hapa Ujerumani uhuru wa magazeti ni nguzo ya demokrasia. Kama njia ya kutolewa jando, jamhuri changa ya Shirikisho la Ujerumani ilipitia miaka 41 iliopita ile iliokuja kuitwa kashfa ya Jarida la SPIEGEL, ambapo muasisi na mchapishaji wa gazeti hilo, Rudolf Augstein, alikaa kwa muda gerezani kwa ati kile kilichodaiwa kuwa ni kitendo cha uhaini dhidi ya nchi yake. Kitendo hicho kilikuwa sio cha haki, hivyo tuhuma hiyo dhidi ya jarida la SPIEGEL ilitupiliwa mbali. Pia wakati huo mahakama ya kikatiba ya Ujerumani ililishughulikia suala hilo. Wakati huo uhuru wa magazeti ulionekana kuwa ni msingi wa dola ilio huru. Kwa hivyo, uhuru wa magazeti ukapata nguvu hapa Ujerumani. Jana, mahakama hiyo ya katiba ilibidi ifanye vivyo hivyo. Haijafanya hivyo kwa vile kadhia hii ya sasa ina umuhimu sawa na ule wa ile kashfa ya SPIEGEL, lakini kwa vile uhuru wa magazeti baina ya wakati huo na sasa umekuwa kidogokidogo na polepole ukiendewa kichinichini.

Kusachiwa majumba na kutwaaliwa vitu, kama ilivofanyika katika mkasa wa jarida la Cicero, kumezidi katika miaka iliopita. Visa 187 vimesajiliwa na jumuiya ya waandishi wa habari tangu mwaka 1987, na tuhuma maisha zimekuwa ati waandishi hao wa habari wamechochea au wameshiriki katika uhaini wa kutoa siri za serekali. Licha ya kwamba mwishowe mwandishi wa habari anaweza kutozwa faini ndogo, lakini jambo hilo linamuaibisha na kumtia hofu mwandishi huyo. Na hali hiyo inawakuta mashushushu na pia waandishi wa habari. Mwishowe, baada ya kutwaliwa mafaili yake, mwandishi huyo wa habari kwa wiki kadhaa anabakia hawezi kufanya kazi, hivyo maisha yake yanaingia katika shida. Hapo tena mwandishi huyo atafikiri mara mbili kama mara nyingine alaumu namna dola inavotenda na vipi wale wanaotawala wanavofanya kazi zao; na hasa pale kutokana na msingi wa kutaka kile anachoandika kiaminike inamlazimu anukulu hati za siri.

Na huo ndio mkakati wa polisi. Waandishi wa habari wanaochunguza visa na kashfa mara nyinghi hukabiliana na mafaili ya idara za serekali ambayo bila ya sababu hupigwa tu mhuri kwamba ni ya siri. Mfano ni kadhia ya yule aliyekuwa zamani mfungwa wa gereza la Guantanamo, Murat Kurnaz. Yule ambaye kama mwandishi wa habari atanukulu mambo kutoka faili lake , basi itambidi ahofie kuandamwa.

Katika mkasa huu na pia mengine, wananchi wana haki ya kupewa uwazi na habari. Raia wana haki ya kujulishwa vipi walio na dhamana serekalini na kwenye utawala, kwa mfano, wanavoyashughulikia kikweli masuala yanayohusiana na haki za binadamu. Ni tu aliye na habari ndiye anayeweza kulalamika juu ya ukorofi na vipi dola inavokosea katika kutimiza wajibu wake. Ni jukumu la waandishi wa habari katika demokrasia kukusanya habari kama hizo na kuzisamnbaza kwa wananchi. Mazungumzo ya hadharani yatakayofuata kuhusu habari kama hizo zilizo wazi yanahakikisha kuweko mazingira ya kidimokrasia.

Duniani kote, jumuiya za kupigania haki za binadamu zinaripoti juu ya kushambuliwa uhuru wa magazeti, kuandamwa na kutishwa waandishi wa habari ambao wanataka kuchapishwa habari zinazohitajiwa na wananchi. Hapa Ujerumani mahakama ya juu kabisa imeweka wazi tena kwamba uhuru wa magazeti ni hazina ilio ya thamani ya juu. Peke yake kuchapisha siri za serekali hakutoshi siku za baadae kuwa ni sababu ya kusachiwa ofisi za wahariri au wafanya kazi wa magazeti. Pia njia, tuseme ya kutafuta uwezekano wa kuvuja habari za taasisi za utawala, hakuwezi kuwa ni sababu ya kusachiwa maofisi ya magazeti.

Kwa mara nyingine tena sio tu waandishi wa habari waliozusha kesi hii wameshinda, lakini hasa demokrasia na raia ndio walioshinda.