1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mahakama yamsafishia njia Kagame muhula wa tatu

Mjahida8 Oktoba 2015

Mahakama ya juu nchini Rwanda imetupilia mbali kesi iliyonuiwa kuzuwiya rais Paul Kagame kurefusha hatamu yake ya urais kwa zaidi ya mihula miwili iliyokubaliwa kikatiba.

https://p.dw.com/p/1GkP5
Karikatur des DW-Zeichners Said Michael
Picha: DW/S. Michael

Mahakama hiyo imesema kesi iliyowasilishwa kwake na chama cha Democratic Green Party of Rwanda haikuwa na maana yoyote. Chama hicho kilitaka kulizuwiya bunge kubadilisha kipengee cha katiba nambari 101 kinachosema kwamba rais anapaswa kuchaguliwa kwa muhula wa miaka 7 na kipindi hicho kinapaswa kurefushwa mara moja tu.

"Hakuna sababu yoyote inayopaswa kumfanya mtu kushikilia hatamu ya uongozi katika ofisi ya jamhuri ya Rwanda kwa zaidi ya vipindi viwili," kama inavyosema katiba ya Rwanda.

Hata hivyo Jaji Mkuu Sam Rugege amesema katika uamuzi wake katika mahakama hiyo mjini Kigali kwamba mahakama imegundua kuwa kipengee nambari 193 cha katiba hiyo inaruhusu kipengee 101 kubadilishwa iwapo hilo litafanywa na wananchi kupitia kura ya maoni.

Rais Paul Kagame
Rais Paul KagamePicha: picture-alliance/dpa

Habineza kuendeleza harakati

Hata hivyo rais wa chama cha Democratic Green Party of Rwanda Frank Habineza amewaambia waandishi habari kuwa walitarajia kushinda keshi hiyo lakini mahakama imewavunja moyo. Habineza amesema chama hicho kitamuomba rais Kagame kutogombea.

Rais Paul Kagame anatarajia kurefusha kipindi chake cha miaka 15 madarakani iwapo katiba itabadilishwa. Amekuwa madarakani tangu mwaka wa 2000.

Kagame alishinda katika uchaguzi wa mwaka 2003 na 2010 -- na kila mara alipata ushindi wa zaidi ya asilimia 90 ya kura. Lakini ameiongoza Rwanda tangu jeshi lake la waasi lilipofanikiwa kusitisha mauaji ya halaiki mwaka 1994.

Zaidi ya watu milioni 3.7 zaidi ya asilimia 60 ya wapiga kura walitia saini ombi la kutaka mabadiliko ya katiba yafanyike ili kumkubali rais Kagame kugombea kwa muhula mwengine mwaka 2017.

Hapo jana Jaji Rugege alisema uamuzi wake unaendena na demokrasia pamoja na katiba ya nchi. Ameongeza kuwa kuna hatua muhimu zinazofuatwa kuhakikisha katiba haikiukwi.

Mwenyekiti wa chama cha Kijani Rwanda Frank Habineza.
Mwenyekiti wa chama cha Kijani Rwanda Frank Habineza.Picha: DW/A. Le Touzé

"Kuwanyima watu wa Rwanda haki ya namna wanayotaka kuongozwa sio demkorasia," alisema Jaji Rugege.

Aidha hatua hii imekuja wakati kukiwa na wasiwasi barani Afrika juu ya hatua ya viongozi kubadilisha katiba ili kuendelea kubakia madarakani.

Marekani mwezi uliopita ilirudia tamko lake la kupinga hatua ya rais Kagame kurefusha muhula wake madarakani.

Mwandishi: Amina Abubakar/AFP/dpa

Mhariri: Iddi Ssessanga