1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mahakama yamzuwia Zuma kujiondoa ICC

Mohammed Khelef
22 Februari 2017

Mahakama nchini Afrika Kusini imeuzuia mpango wa serikali kujiondoa kwenye Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC) ikisema ni mpango "ulio kinyume na katiba na usiofaa".

https://p.dw.com/p/2Y1g4
Jacob Zuma und Omar al-Bashir
Picha: picture alliance/dpa/E.Hamid

Uamuzi huu uliotolewa Jumatano (22 Februari) na Jaji Phineas Mojapelo wa Mahakama Kuu ya North Gauteng ni pigo kubwa kwa juhudi za Rais Jacob Zuma anayetaka kuiondoa nchi yake kutoka ICC. 

"Uamuzi wa baraza la mawaziri kutuma hati ya kujiondoa kwa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa bila ya kwanza kuidhinishwa na bunge ni kinyume na katiba na haufai kabisa," alisema Jaji Mojalepo.

Hukumu hiyo inamtaka Rais Zuma na mawaziri wake "kuiondoa mara moja hati hiyo".

ICC imekuwa ikikabiliwa na vitisho vikubwa vya mataifa wanachama kujiondoa katika miezi ya hivi karibuni, ambapo serikali za mataifa hayo zinalalamikia ukandamizaji wa ICC dhidi ya Afrika.

Mnamo mwezi Oktoba, serikali ya Zuma ilitangaza kuwa ilishatuma tamko lake la kujiondoa kwenye mahakama hiyo katika Umoja wa Mataifa, kufuatia mzozo uliozuka baada ya kushindwa kumkamata Rais Omar al-Bashir wa Sudan aliyekuwa akiitembelea nchi hiyo kuhudhuria mkutano wa kilele wa Umoja wa Afrika.

Bashir amekwepa kukamatwa tangu ulipotolewa waraka wa ICC mwaka 2009 kutokana na tuhuma za uhalifu wa kivita katika jimbo la Darfur, ambapo watu 300,000 waliuawa na wengine milioni mbili kulazimishwa kuyahama makaazi yao.

Baada ya kuchaguliwa kwa Rais Adama Barrow nchini Gambia, serikali ya nchi hiyo iliuomba Umoja wa Mataifa kusitisha mchakato wake wa kujiondoa ICC, ikifuta ombi lililotumwa na mtangulizi wake, Yahya Jammeh.

Burundi pia imejiandikisha kwenye orodha ya mataifa yanayoondoka ICC, huku Kenya ikitajwa kufikiria kuchukuwa uamuzi kama huo.

Mwandishi: Mohammed Khelef/AFP
Mhariri: Saumu Yussuf