1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Maharamia wa kisomali wadai dola millioni 20

Mwadzaya, Thelma29 Septemba 2008

Maharamia wa Kisomali walioteka meli ya Ukraine iliyosheheni zana za kijeshi wanadai dola milioni 20 ndipo wakiachie chombo hicho.Meli hiyo inaripotiwa kuzingirwa na meli tatu za kivita kutoka mataifa ya kigeni

https://p.dw.com/p/FQyp
Maharamia wa kisomali wakiwa katika moja ya meli walizowahi kuziteka, meli ya kifahari ya PonantPicha: picture-alliance/dpa

Kulingana na msemaji wa kundi hilo la maharamia wa Kisomali Sugule Ali meli hiyo ya Ukraine imezingirwa na meli tatu za kigeni na mabaharia wake wako salama.


Tayari baharia mmoja wa meli hiyo ya Ukraine anaripotiwa kufariki ila hakupigwa risasi.


MV Faina ilitekwa nyara Alhamisi iliyopita ilipokuwa ikielekea kwenye bandari ya Mombasa nchini Kenya.Meli hiyo inaripotiwa kuwa na shehena ya zana za kijeshi vikiwemo vifaru vilivyolengwa kutumiwa na jeshi la Kenya.


Awali mshauri wa rais wa eneo la Puntland lililojitenga alithibitisha kuwa meli hiyo imezingirwa na meli moja ya Marekani na mbili kutoka mataifa ya Ulaya ambayo hakuyataja.


Serikali za Uingereza,Ufaransa ,Ujerumani na Ugiriki zimesema kuwa mabaharia wao hawahusiki na operesheni hiyo.


Helikopta ya kijeshi ya Marekani inaripotiwa kuzunguka kwenye eneo hilo kwa minajili ya kuwatia hofu maharamia wengine wanaopanga kusaidia kundi hilo


Serikali ya Kenya kwa upande inaeleza kuwa haijawasiliana na maharamia hao ila juhudi za kuiokoa zinaendeleaa.


Hata hivyo bado kuna utata kuhusu nchi iliyoagiza shehena hiyo.


Tetesi zimezuka zinazoeleza kuwa silaha hizo ziliagizwa na serikali ya Kusini mwa Sudan.Itakumbukwa kuwa eneo hilo la Kusini mwa Sudan haliruhusiwi kununua silaha baada ya kutia saini makubaliano ya amani kati yake na serikali ya Khartoum.


Makubaliano hayo ya amani yalitiwa saini mwaka 2005 na kumaliza kipindi cha miaka 21 cha vita vya wenyewe kwa wenyewe.


Msemaji wa serikali ya Kenya Dr Alfred Mutua amekanusha taarifa hizo na kusisitiza kuwa shehena hiyo ni mali ya Kenya.


Mabaharia wa MV Faina wanajumuisha raia 17 wa Ukraine,watatu wa Urusi na mmoja wa Latvia.


Urusi kwa upande wake ilipeleka meli yake ya kivita ya Neustrashimy kufukuzia MV Faina.


Wizara ya Ulinzi ya Marekani nayo inafuatilia tukio hilo kwa karibu.Kwa mujibu wa Taasisi ya kimataifa kuhusu Masuala ya Ubaharia yapata meli 55 zimetekwa nyara na maharamia wa Kisomali kwenye Guba ya Aden na Bahari ya Hindi tangu mwanzoni mwa mwaka huu.


Somalia inazongwa na usalama duni na imekuwa bila ya serikali thabiti tangu mwaka 1991 baada ya rais Mohamed Siad Barre kungolewa madarakani.