1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Maharamia wa kisomali wagonga vichwa vya habari

Oumilkher Hamidou20 Novemba 2008

Umoja wa ulaya waajiandaa kutuma vikosi kupambana na maharamia

https://p.dw.com/p/Fya0
Meli ya mafuta ya Saud Arabia Sirius Star imetekwa nyara na maharamia wa kisomaliPicha: AP




Wahariri wa magazeti ya Ujerumani wamejishughulisha zaidi na mpango wa umoja wa ulaya wa kutuma vikosi vya kupambana na maharamia wa kisomali na kuvunjwa bunge la jimbo la Hesse .


Tuanzie bahari ya Hindi ambako walimwengu wanazidi kuingiwa na wahka kutokana na kuongezeka hujuma za maharamia katika mwambao wa Afrika Mashariki,linahisi gazeti la NEUE OSNABRÜCKER ZEITUNG,na kuendelea kuandika:


"Inaeleleweka.Kwasababu visa hivyo vya utekaji nyara vinatishia kuvuruga njia mojawapo muhimu kabisa kwa shughuli za kiuchumi za mataifa ya magharibi.Kwa mtazamo wa muda mfupi,hakuna njia nyengine isipokua opereshini za kijeshi.Lakini watu wasitegemee miujiza.Opereshini hizo zitazuwia kidogo tuu ,chanzo halisi lakini cha uhalifu huo wa baharini kitasalia pale pale.Kimesababishwa hasa na ile hali ya shida na usumbufu iliyozagaa Somalia-nchi isiyokua na serikali wala kanuni tangu miaka 20 iliyopita.Imegeuka kua uwanja ambako wageni wanapigania masilahi yao.Wanadai wanataka kupambana na wanaamgambo wa kiislam na magaidi.Lakini ushawishi wao unazidi kupaalilia msimamo mkali.


Gazeti la LAUSITZER RUNDSCHAU la mjini Cottbus lina maoni sawa na hayo na linaandika.


Anaetaka kukomesha utovu katika pembe ya Afrika,atabidi kwanza aiokoe Somalia.Mpango wa umoja wa ulaya wa kupambana na maharamia utakaoanza december ni hatua ya mwanzo tuu.Utaleta tija ikiwa mpango huo utakua wa muda mrefu na kutumwa pia vikosi vya nchi kavu.Hakuna lakini anaeonyesha daalili ya kutaka kuchangia katika mpango kama huo,-


linalalamika gazeti la LAUSITZER ZEITUNG.Nini muhimu zaidi,bidhaa au maisha ya binaadam?linajiuliza gazeti la FRANKFURTER RUNDSCHAU


Ni suala linalostahiki kuulizwa hilo.Jumuia ya kimataifa inajiandaa kuamua:Hivi karibuni tuu manuari za mataifa ya Umoja wa Ulaya zitaelekea katika bahari ya hindi kulinda ujia wa kibiashara dhidi ya balaa linalosababishwa na uharamia wa kimambo leo.Maelfu ya watoto wasiojiweza,wakinamama na wakinababa katika eneo la mashariki la jamahuri ya kidemokrasi ya Kongo,wanaachiwa wao waendelee kusubiri hadi jumuia ya kiuchumi na maadili ya Ulaya itakapoamua kuwahami dhidi ya ghadhabu za wanajeshi makatili.Frankfurter RUNDSCHAU linasema binaadam katika eneo la mashariki la Kongo wanastahiki kushughulikiwa sawa na zinavyoshughulikiwa meli za mafuta."


Na hatimae wahariri wa magazeti ya Ujerumani wametupia jicho pia kuvunujwa bunge la jimbo la Hesse.Gazeti la SÜDDEUTSCHE ZEITUNG linaandika:


Kwamba uchaguzi unaitishwa upya Hesse baada ya kupita miezi kumi tuu,wakulaumiwa sio peke yake Andrea Yipsilanti aliyekwenda kinyume na ahadi aliyotoa.Ni sawa kwamba sababu kubwa ya kuitishwa uchaguzi ni jaribio lake la kutaka kuunda serikali ya wachache ambayo ingevumiliwa na waafuasi wa siasa kali za mrengo wa shoto Die Linke.Ushupavau wake umewakera na kulaumiwa hata na wafuasi wa chama chake mwenyewe cha SPD.Lakini kuna sababu nyengine pia kwanini uchaguzi unaitishwa,nayo inatokana na kupooza nyendo za kisiasa katika jimbo hilo.Kulikua na njia nyengine pia za kuunda serikali ya muungano,lakini kila upande ulipinga kuregeza kamba.