1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mahasimu wa Sudan Kusini wasaini makubaliano ya amani

2 Februari 2015

Rais wa Sudan Kusini, Salva Kiir na kiongozi wa waasi, Riek Machar leo (02.02.2015) wamesaini makubaliano mapya ya kumaliza vita vya wenyewe kwa wenyewe vilivyodumu kwa zaidi ya miezi 13.

https://p.dw.com/p/1EUFZ
Riek Machar na Rais Salva Kiir
Riek Machar na Rais Salva KiirPicha: Getty Images/Zacharias Abubeker/Ashraf Shazly/Montage

Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Mashariki na Pembe ya Afrika-IGAD, imethibitisha leo kuwa makubaliano hayo yamesainiwa, mjini Addis Ababa, Ethiopia baada ya siku nne za mazungumzo muhimu na kwamba hatua imepigwa kuelekea kumaliza vita vya Sudan Kusini. Mpatanishi mkuu wa IGAD, Seyoum Mesfin amesema viongozi hao hasimu wamekubaliana kuhusu mkataba mpya wa kumaliza mapigano, lakini wameshindwa kufikia makubaliano ya kugawana madaraka, yaliyopendekezwa na IGAD, kwa lengo la kumaliza kabisa mzozo uliosababisha mauwaji ya maelfu ya watu.

Kwa mujibu wa mapendekezo ya IGAD yaliyofikiwa Addis Ababa, Salva Kiir ataendelea kuwa rais, huku Riek Machar akiwa makamu wake, nafasi aliyokuwa nayo hadi Julai mwaka 2013, alipofukuzwa na hivyo kusababisha vita vilivyoibuka miezi mitano baadaye. Akizungumza baada ya makubaliano hayo kusainiwa, Waziri Mkuu wa Ethiopia, Hailemariam Dessalegn, ambaye pia ni Mwenyekiti wa IGAD, amesema ana uhakika viongozi hao wawili wataheshimu kile walichosaini leo.

Mpatanishi mkuu wa IGAD, Seyoum Mesfin
Mpatanishi mkuu wa IGAD, Seyoum MesfinPicha: AP Photo/Ed Bailey

''Katika siku zijazo za mwezi Februari tutashuhudia makubaliano ya kueleweka yakisainiwa. Hilo ndilo jambo ambalo watu wa Sudan Kusini wanalitarajia, na watu wa eneo hili pamoja na jumuiya ya kimataifa wanatarajia kutoka kwa viongozi hao. Kushindwa kufanya hivyo itakuwa ni matokeo mabaya sana kwetu sote na hasa kwa viongozi wa Sudan Kusini'', alisema Dessalegn.

Makubaliano kamili kufikiwa Februari 20

Hata hivyo, Mesfin amesema utiaji saini wa makubaliano hayo ya kumaliza kabisa uhasama, unatarajiwa kukamilika katika mazungumzo ya mwisho yatakayofanyika tarehe 20 ya mwezi huu wa Februari. Balozi wa Umoja wa Ulaya anayeshiriki kwenye mazungumzo hayo amesema matumaini ya kupatikana mkataba wa kudumu wa amani yanafifia.

Mesfin amesema IGAD itamchukulia hatua kali kiongozi yeyote atakayekiuka makubaliano hayo na taarifa zake zitafikishwa katika Umoja wa Afrika na Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa. Umoja wa Afrika na Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kwa pamoja zimetishia kuweka vikwazo dhidi ya wale wanaokwamisha mpango wa amani Sudan Kusini. Kiir na Machar tayari wameshasaini karibu mikataba sita, ingawa mikataba hiyo ilikiukwa na kuvunjwa.

Watoto wasio na makaazi kutokana na vita
Watoto wasio na makaazi kutokana na vitaPicha: Reuters/Kate Holt/UNICEF

Pande hizo mbili zinahitaji kuwa na serikali ya mpito ifikapo mwezi Julai, wakati ambapo Rais Kiir atakuwa amemaliza muda wake madarakani. Mapigano nchini Sudan Kusini yalianza Disemba mwaka 2013, baada ya Kiir kumtuhumu Machar kwa kufanya jaribio la mapinduzi. Mashirika ya kutetea haki za binaadamu yanasema kuwa pande hizo mbili zinahusika na mauaji ya kikabila na ukiukwaji mwingine, hatua iliyolisababisha taifa hilo changa kutumbukia katika njaa kubwa.

Mwandishi: Grace Patricia Kabogo/AFPE,RTRE,APE
Mhariri:Josephat Charo