1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mahasimu wa zamani wa Marekani wampongeza Obama

14 Aprili 2009
https://p.dw.com/p/HWhS
Rais Barack Obama.Picha: AP

Hatua ya Rais Barack Obama wa Marekani sera ilio wazi kuhusiana na hali ya Mashariki ya kati, sasa yaelekea kuwafurahisha hata wale waliokua mahasimu wa Marekani wakati tawala za marais waliomtangulia. Miongoni mwa wanaompongeza kiongozi huyo wa Marekani ni Rais wa Libya Muammar Gaddafi ambaye amemtaja Obama kuwa ishara ya matumaini. Jee mtazamo huu mpya unaweza kweli kusaidia kuufufua utaratibu wa kusaka amani ya mashariki ya kati ?

Afrika-Gipfel der Afrikanischen Union der libysche Revolutionsführer Muammar el Gaddafi
Muammar Gaddafi wa Libya.Picha: AP

Kiongozi wa Libya ambaye wakati mmoja alikua ni mwiba wa mchongoma kwa Marekani, ni mtu aliyetajwa kuwa " mbwa mwenye kichaa," na rais wa zamani wa Marekani Ronald Reagan miaka ya 1980. Lakini tangu 2003 ameuboresha uhusiano wake na Marekani.

Katika sifa alizomwagia Obama wakati wa mkutano wa hadhara wiki iliopita, Gaddafi alisema kiongozi huyo mpya wa Marekani anazungumza mambo ya maana na hakuna kiburi katika mtazamo na muelekeo wa Marekani, ambao awali ulikua wa kuziamrisha nchi nyengine duniani zifuate kile inachotaka.

Obama pia amepongezwa na Rais wa Syria Bashar al-Assad, Kiongozi wa chama cha wapalestina cha Hamas Khaled Meshaal na Ayatollah mkuu wa Lebanon Sayed Mohammed Hussein Fadlallah, watu ambao Marekani wakati fulani iliwahusisha na ugaidi.

Si hayo tu lakini hata kiongozi wa nchi isiyokua ya kiarabu-Iran, Mahmoud Ahmedinejad ametambua kwamba Obama anaweza kuleta kitu fulani kipya. Katika mahojiano na jarida la Ujerumani Der Spiegel, Ahmedinejad alisema " Tunazungumza tukiwa na heshima kubwa kwa Obama. Lakini tunaiangalia hali kwa makini na tunataka kuona mabadiliko ya kweli." Tunahisi sasa Obama anapaswa kuyambatanisha maneno yake na vitendo."

Präsident Bashar Assad Mahmoud Ahmadinejad
Rais wa Syria Bashar al-Assad (kushoto) na Mahmoud Ahmadinejad wa Iran.Picha: AP

Lakini wakati wale waliokua mahasimu wa Marekani hapo zamani wakitamka hayo, baadhi ya washirika wa jadi wa Marekani wamekaa kimya. mmoja wapo ni rais wa Misri Husni Mubarak.Huenda viongozi wahafidhina katika ulimwengu wakiarabu hawakufurahishwa na sera ya Obama kuwajongelea mahasimu wao wao Iran na Syria, na wana wasi wasi pia kwamba muda si mrefu anaweza pia akarejea upya shinikizo la Marekani kutaka nchi hizo za kiarabu ziheshimu haki za binaadamu na kuleta mageuzi ya kidemokrasi katika mifumo yao wenyewe ya kiimla.

Pia Saudi Arabia na Misri zimekua zikionya mnamo miezi ya karaibuni kuhusu kuzidi kwa ushawishi wa Iran katika eneo hilo, wakati huo huo zikijaribu kuivuta karibu Iran badala mfarakano

Hata hivyo wakati Obama akionyesha kuwa na mtazamo mpya kuhusu Mashariki ya kati, utawala mpya nchini Israel chini ya Waziri mkuu Benjamin Netanyahu umegeuka kikwazo katika juhudi za kuleta amani. Netanyahu anayeongoza serikali ya mseto ambamo vyama vya siasa kali za mrengo wa kulia vina usemi mkubwa, haungi mkono suala la kuwa na mataifa mawili- Israel na Palestina kama suluhisho. Waziri wake wa kigeni Avgidor Lieberman ametamka wazi akisema mazungumzo ya amani yanayoungwa mkono na Marekani sasa "yamekufa."

Chini ya mtazamo wa yote hayo, kile ambacho nchi za kiarabu zinakisubuiri kwa hamu, ni kuona vipi utawala wa Obama utaweza kukabiliana na serikali ya siasa akali za mrengo wa kulia nchini Israel. Wachambuzi kwa upande mwengine wanasema, Israel ina historia ya wanasiasa wa misimamo mikali ambao baadae wamekubaliana na ukweli wa mambo ulivyo.

Kwa mfano Menahem Begin aliyewahi kukataa kabisa kuzungumza na waarabu, lakini hatimae akafikia makubaliano ya amani na rais wa zamani wa Misri Anuwar Sadat. Israel ikasaini pia mkataba wa amani na Jordan. halikadhalika mwanasiasa mwengine Ariel Sharon alipiga hatua moja mbele baada ya miaka mingi ya msimamo mkali, na kuyakongoa makaazi ya walowezi wa kiyahudi katika ukingo wa magharibi , kabla ya kuondoka madarakani kutokana na hali mbaya ya afya.

Kwa mtazamo huo, huenda serikali mpya nchini Israel inatumia mbinu ya kupoteza wakati, na hatimae inaweza kurudi tena katika meza ya mazungumzo na Wapalestina na waarabu kwa jumla, bila shaka kwa shinikizo la Marekani.

Mwandishi:M.Abdul-Rahman

Mhariri:Saumu Mwasimba