1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mahmaoud Abbas aikosoa Marekani

Isaac Gamba
15 Januari 2018

Rais wa  Mamlaka ya Wapalestina Mahmud Abbas amesema Marekani haiwezi tena kuwa msuluhishi kati ya Palestina na Israel, kufuatia hatua za ivi karibuni za utawala wa Rais Donald Trump.

https://p.dw.com/p/2qqgw
Palästina Israel Konflikt Versammlung PLO in Ramallah Mahmoud Abbas
Picha: Getty Images/AFP/A. Momani

Katika hotuba yake aliyoitoa katika baraza kuu la mamlaka ya ndani ya Palestina ambacho ni chombo chenye maamuzi  Mahmoud Abbas alimkosoa Trump pamoja na sera zake kuhusiana na Palestina  ikiwa ni pamoja na hatua yake ya kutambua Jerusalem kama mji mkuu wa Israrel.

Alisema Trump anapaswa kuona aibu kutokana na madai yake kuwa wapalestina  wanakataa kuzungumza kuhusiana na amani ya Masharikiya Kati na kusisitiza kuwa wapalestina  wanaheshimu mazungumzo ya amani  lakini pia wanayo haki ya kukataa kile ambacho hakiko katika maslahi yao.

Kauli yake inaashiria  kuzorota kwa mahusiano kati ya mamlaka ya ndani ya Palestina na utawala wa rais Donald Trump.

Wapalestina wanauona uamuzi wa Trump wa kutangaza Jerusalem kuwa mji mkuu wa Israel kuwa umeharibu hadhi yake ya kuwa mpatanishi wa amani ya Mashariki ya Kati.

Akifafanua zaidi Abbas alisema wanatambua kuwa mji wao mkuu ni Jerusalem  na kuwa hawatakubali pendekezo linalotajwa la  mji wa Abu Dis kuwa mji wao mkuu wa mamlaka ya ndani ya Palestina  badala ya mji wa Jerusalem kauli inayothibitisha taarifa za awali kuwa mji huo wa Abu Dis ulikuwa ukipendekezwa kutolewa kwa Wapalestina kama mbadala kwa Jerusalem.

Hadhi ya mji wa Jerusalem ni moja ya masuala muhimu na nyeti katika mgogoro uliochukua miongo kadhaa kati ya Israel na Palestina  na tangazo la Trump kuhusiana na hadhi ya mji huo  alilotoa Desemba 6, mwaka jana lilichochea maandamano maeneo mengi ulimwenguni.

Majadiliano ya kisiasa yatakiwa kuwa chini ya mpatanishi kimataifa

USA Donald Trump
Rais Donald Trump wa MarekaniPicha: picture alliance/dpa/AP Photo/E. Vucci

Abbas aliongeza kuwa  majadiliano ya kisiasa  yanapaswa kuwa  chini ya mpatanishi kimataifa na siyo Marekani pekee na kuwa hakubali Marekani kuwa mpatanishi kati yao na Israel.

Ama kwa upande mwingine  Abbas alisema wapalestina wamekataa hatua ya Marekani ya kusitisha malipo kwa ajili ya wapalestina waliojeruhiwa  kwa karibu familia 35,000 za wapalestina waliouawa na kujeruhiwa katika mgogoro kati yake na Israel.  Utawala wa Israel unasema kuwa hatua hiyo inashawishi vurugu.

Wakati huohuo utawala wa rais Donald Trump anapanga kuzuia mamilioni ya dola inazotoa kwa ajili ya wakimbizi wa kipalestina kwa mashirika ya Umoja wa Mataifa na kupunguza mchango wake huo katika mwaka wa kwanza kwa kiwango cha zaidi ya nusu ya fedha hizo.

Ingawa rais Donald Trump hajatoa uamuzi rasmi lakini anaonekana kutoa dola milioni 60 pekee kati ya dola milioni 125 zilizopangwa kutolewa kama fungu la kwanza kwa mashirika ya misaada ya kiutu ya Umoja wa Mataifa. Walisema maafisa  ambao hawakuwa tayari kutajwa majina kwa vile si wasemaji maalumu wa suala hilo. Maafisa hao wameongeza kuwa michango zaidi itategemea  shirika linalohusika na misaada hiyo ambalo linakosolewa na Israel ikitaka  lionyesha mabadiliko katika utendaji wake na pia moja ya kigezo ikiwa ni Palestina kukubali  kushiriki mazungumzo ya amani.

Mwandishi: Isaac Gamba/ape/dpae

Mhariri      : Gakuba, Daniel