1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mahmoud Abbas kuikashifu Marekani katika Umoja wa Mataifa

John Juma
20 Februari 2018

Rais wa Wapalestina Mahmud Abbas atarajiwa kutoa wito wa kupewa uanachama kamili katika Umoja wa Mataifa na atalihimiza Baraza la Usalama la UN kupinga uamuzi wa Marekani wa kuutambua Jerusalem kama mji mkuu wa Israel

https://p.dw.com/p/2t0QP
UN-Sicherheitsrat in New York zu Situation in Nahost
Picha: Reuters/B. McDermid

Rais Mahmoud Abbas wa Palestina anatarajiwa kulihimiza Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kupinga uamuzi wa Marekani wa kuutambua mji wa Jerusalem kama mji mkuu wa Israel na lianzishe mchakato madhubuti wa kutafuta amani. Aidha kiongozi huyo anatarajiwa kutaka uanachama kamili katika Umoja wa Mataifa.

Akilihutubia Baraza la Usalama kwa mara ya kwanza tangu mwaka 2009 mjini NewYork, kiongozi huyo wa Wapalestina Mahmud Abbas anatarajiwa kutoa wito wa kupewa uanachama kamili katika Umoja wa Mataifa. Umoja wa Mataifa uliitambua Palestina kama mwangalizi mnamo mwaka 2012 licha ya pingamizi kutoka Marekani.

Mnamo mwaka 2011, Marekani na washirika wake walipinga juhudi za awali za Palestina kutaka kupewa uanachama kamili katika Umoja huo. Swali la ikiwa Palestina itakubaliwa uanachama kamili katika Umoja wa Mataifa linahusiana moja kwa moja na mkwamo katika kutafuta suluhisho la pande mbili kuhusu mzozo wa muda mrefu kati ya Israel na Palestina. Israel pia itakuwa katika mkutano huo wa Baraza la Usalama.

Kunusuru mchakato wa kutafuta amani ya mzozo wa Israel na Palestina

Rais wa Wapalestina Mahmud Abbas
Rais wa Wapalestina Mahmud AbbasPicha: picture-alliance/dpa/Str.

Kadhalika, Abbas atatoa wito mpya wa pamoja wa kunusuru mchakato wa amani katika mzozo wa pande mbili Israel na Palestina. Hayo ni kwa mujibu wa balozi wa Palestina kwenye Umoja wa Mataifa, Riyad Mansour. Mansour ameliambia shirika la habari la AFP kuwa Abbas atasema kuwa kuhusiana na Jerusalem, baada ya Disemba 6 sasa ni wakati wa juhudi za pamoja.

Hiyo inaweza kusababisha wanachama wengine wanne wa kudumu - Uingereza, Ufaransa, China na Urusi kuimarisha juhudi zao au inaweza kutanua diplomasia baina ya nchi hizo na nchi za kiarabu na nyinginezo.

Kwa sasa pande zinazohusika na mzozo wa Mashariki ya Kati kando ya Israel na Palestina zenyewe ni Marekani, Umoja wa Mataifa, Umoja wa Ulaya na Urusi.

Mansour amesema maadamu Baraza la Usalama ni mamlaka ya juu zaidi katika masuala ya amani na usalama kimataifa, linapaswa kuja na mpango mpya wa kimataifa na kwamba Marekani haitatengwa.

Ameongeza kuwa katika mpango huo mpya, Marekani haitakuwa mshirika pekee mwenye udhibiti bali itakuwa sehemu ya mchakato wa pamoja.

Balozi wa Marekani katika Umoja wa Mataifa Nikki Haley
Balozi wa Marekani katika Umoja wa Mataifa Nikki HaleyPicha: Reuters/B. McDermid

Ghadhabu kuhusu hatua ya Trump

Uamuzi wa Rais Donald Trump wa Marekani kuuhamisha ubalozi wa Marekani hadi Jerusalem uliwaghadhabisha Wapalestina na wakaamua kwamba Marekani haiwezi tena kuongoza mchakato wa amani ya Mashariki ya Kati

Wiki chache baada ya balozi wa Marekani katika Umoja wa Mataifa, Nikki Haley, kuanzisha mashambulizi makali dhidi ya Rais Abbas, na kumtaja kuwa mtu aliyekosa ujasiri unaohitajika kwa amani, viongozi hao wanatarajiwa kukutana katika mkutano wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa

Israel, ambayo mara kwa mara huulaumu Umoja wa Ulaya na Umoja wa Mataifa kwa kutoipendelea, imerejea mara kadhaa kusema kuwa haitakuwa tayari kupokea mpatanishi mwengine tofauti na Marekani. Balozi wa Israe,l Danny Danon, pia anatarajiwa kuhutubia Baraza la Usalama.

Mwandishi: John Juma/AFPE/DPAE

Mhariri: Mohammed Khelef