1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Maiti za wanajeshi wa Kijerumani zarejeshwa nyumbani

5 Aprili 2010

Maiti za wanajeshi watatu wa Kijerumani waliouliwa na Wataliban huko Kundus, Afghanistan, katika siku ya ijumaa kuu zimewasili jana jioni mjini Kolon

https://p.dw.com/p/MnS2
Waziri wa ulinzi wa Ujerumani, Karl-Theodor zu GuttenbergPicha: AP
Maiti za wanajeshi watatu wa Kijerumani waliouliwa na Wataliban huko Kundus, Afghanistan, katika siku ya ijumaa kuu zimewasili jana jioni mjini Kolon zikisafirishwa na ndege ya serekali. Ndani ya ndege hiyo alikuwemo pia waziri wa misaada ya maendeleo, Dirk Niebel, na ujumbe wake ambao walirejea kutoka ziara yao ya Afghanistan. Kuzipipokea maiti hizo katika uwanja wa ndege alikuweko pia waziri wa ulinzi, Karl-Theodor zu Guttenberg. Zaidi anayo Othman Miraji...

Ilikuwa siku ngumu kwa wanasiasa hao wawili wa Kijerumani, waziri wa ulinzi, Karl-Theordor zu Guttenberg aliyepokea majeneza ya wanajeshi hao katika kiwanja cha ndege cha Kolon, na waziri wa misaada ya maendeleo, Dirk Niebel, aliyesindikiza majeneza hayo kutokea Kundus, Afghanisatn. Mwenywe waziri Guttenberg alisema: haiamininiki, kuuwawa kwa wanajeshi hao kumeugusa sana moyo wake.

Baada ya kutokea mapigano hayo makali, ambapo wanajeshi wa Kijerumani walihusika, serekali ya Ujerumani inabidi sasa ijiulize masuala mengi ya kiuhakiki juu ya operesheni zake na pia mpango wa kubadilisha mikakati. Hali ya mambo imezidi kufanya masuali hayo kubidi kupatiwa majibu, hasa kwa vile kutokana na baada ya mkasa huo, jeshi la Ujerumani liliwauwa, kwa makosa, wanajeshi sita wa Ki-Afghanistan. Waziri Guttenberg, ambaye aliivunja likizo yake huko Afrika Kusini, alisema katika mkutano wa waandishi wa habari ulioitishwa kwa haraka katika ofisi ya wizara yake mjini Bonn kwamba kuuliwa kwa wanajeshi hao wa Ujerumani ijumaa iliopita kumeweka wazi tena hali halisi ya mambo ilivyo huko Afghanistan na vipi inavoweza kuwa katika siku za mbele. Alisema kwa waasi wa huko Afghanistan kuichagua siku ya ijumaa kuu kufanya mashambulio hayo ni kubeza tamaduni za watu wengine na utamaduni wao pia.

Waziri huyo alisema shambulio hilo la Wataliban lilikuwa kweli la usaliti, lilikuwa la uwiano wa hali ya juu na gumu.

Wanajeshi wa Kijerumani, waliokuwa wanapiga doria ya kawaida katika eneo lilokuwa sio tulivu, wilaya ya Schahar Dara, walishambuliwa na kukatokea mapigano ya saa kumi na Wataliban. Wanajeshi watatu wa Kijerumani walikufa na wanane walijeruhiwa, baadhi yao vibaya.

Vifo hivyo vilikuwa vya mwanzo tangu  Karl-Theodor zu Guttenberg akamate wadhifa wa uwaziri wa ulinzi, lakini  mwanasiasa huyo, kinyume na mtangulizi wake, Franz-Josef Jung, hajatafuna maneno, na alitumia lile neno linalotisha, akisema kwamba mtu anaweza kusema kwamba kuna vita huko Afghanistan.

"Kila kitu tutafanya, na tutafanya kila kitu kuepusha haya, lakini hali ambayo mtu anaweza kuiita karibu ya kivita au, kwa lugha ya kawaida, mtu atapenda kuita ya kivita, hali kama hiyo isiotakiwa haiwezi kukatalika kwamba haitokuja."

Hadi sasa wameshakufa katika operesheni za Afghanitan wanajeshi 39 wa Kijerumani, 22 katika mashambulio na mapigano.

Mara kadhaa katika matamshi yake ya jana, waziri Guttenberg, alielezea masikitiko yake kwa wanajeshi wa Ki-Afghanistan ambao waliuliwa kwa makosa. Wanajeshi hao waliendesha gari za kiraia na kutokana na ripoti za jeshi la Ujerumani, licha ya kanuni za usalama na kujitambulisha, gari yao haijasimama.

Akizungumzia juu ya vifo hivyo vya Wa-Afghanistan, waziri Guttenberg alisema:

"Kutokana na hali ya sasa, tunafahamu kwamba wameuwawa wanajeshi sita ambao walipoteza maisha kutokana na wanajeshi wa Kijerumani kufyetua risasi."

Waziri huyo wa Ujerumani ameomba radhi kwa waziri mwenzake wa Afghanistan, na Ujerumani itafanya uchunguzi juu ya mkasa huo .

Kwa hivyo, baada ya Pasaka hii, waziri huyo wa ulinzi wa Ujerumani itambidi aitete kwa nguvu siasa ya serekali ya Ujerumani ya kuendeleza operesheni zake za kijeshi huko Afghanistan, jambo ambalo linazidi kutopendwa na raia wengi. Waziri huyo amesema atabakia na mkakati ule ule, nao ni kwamba katika siku za mbele wanajeshi watakwenda katika maeneo mapana zaidi, na hatua kwa hatua kuonesha kwamba wako katika eneo hilo. Hivyo itawafanya Wataliban watengwe na watu ambao watapata himaya ya  wanajeshi wa Kijerumani. Mkakati huo mpya utatekelezwa hadi majira ya kiangazi na machipuko, lakini una hatari zake; lakini. ikumbukwe, ule wa zamani ulikuwa wa hatari pia. Waziri alisema operesheni za kijeshi  huko Afghanistan ziko na zitabaki kuwa za hatari.

Mwandishi:Othman Miraji /AFP

Mpitiaji:Mohammed Abdul-Rahman