1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Maiti zaanza kuzikwa Haiti

Sekione Kitojo16 Januari 2010

Waziri wa Mambo ya Ndani wa Haiti amesema kuwa idadi ya watu waliofariki katika tetemeko la ardhi huenda ikafikia 200,000. Kwa mujibu wa serikali, hadi maiti 40,000 tayari zimezikwa.

https://p.dw.com/p/LXRu
Wafanyakazi wa shirika la kutoa misaada wakianza kugawa misaada na madawa kwa watu walioathirika na tetemeko la ardhi nchini Haiti.Picha: AP

Waziri wa Mambo ya Ndani wa Haiti amesema idadi ya watu waliouawa katika tetemeko la ardhi nchini humo huenda ikafikia 200,000. Katika mji mkuu Port-au-Prince, wasaidizi na waokoaji kutoka zaidi ya nchi 30 wanatoa misaada ya dharura huku maiti zikiendelea kurundikwa kando ya barabara .Maafisa wa Umoja wa Mataifa wanasema kuwa katika mji huo, hadi nusu ya majengo ama yamebomoka au yameteketezwa.

Rais wa Marekani Barack Obama amesema nchi yake inafanya kila kiwezekanacho kuwasaidia wakazi wa Haiti. Wanajeshi wa majini na nchi kavu wa Marekani wamekabidhiwa dhamana ya kusimamia uwanja wa ndege mjini Port-au-Prince na wameanza kuratibu ugavi wa misaada. Idadi ya wanajeshi wa Marekani nchini Haiti inatazamiwa kufikia hadi 10,000 . Baadhi yao wanatarajiwa kuwasili siku ya Jumatatu. Nae Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Hillary Clinton anatazamiwa kwenda Haiti leo Jumamosi.