1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Majadiliano kuhusu mustakabali wa Kosovo yameahirishwa

P.Martin9 Februari 2007

Mawaziri wa ulinzi wa shirika la kujihami-NATO hii leo wamekuwa na majadiliano pamoja na waziri mwenzao wa Urussi Sergei Ivanov katika mji wa Seville nchini Hispania.

https://p.dw.com/p/CHKQ

Ingawa mada kuu ya mkutano wa Seville ilihusika na mkakati wa kijeshi kuhusu Afghanistan,masuala mengine pia yalichomoza kama vile mustakabali wa Kosovo.

Kwa kweli,kwa mawaziri wa ulinzi wa NATO,Kosovo haikuwa mada kuu ya mkutano wao pamoja na waziri wa ulinzi wa Urussi Sergei Ivanow.Hata hivyo lakini,Ivanov aliitumia fursa hiyo kwa mara nyingine tena kueleza kinaganaga msimamo wa serikali ya Urussi kuhusu pendekezo la mjumbe wa Umoja wa Mataifa Martti Athisaari,kuwa Kosovo ipewe uhuru wa kiwango fulani.Waziri Ivanov amesema,Moscow itapigia kura azimio la Umoja wa Mataifa kuhusu Kosovo,ikiwa ni suluhisho linaloungwa mkono na Serbia.Kisheria,Kosovo ingali ni sehemu ya Serbia.

Akiendelea Ivanov alionya kuwa pindi Kosovo itapewa uhuru kamili,basi hatua hiyo itachochea wimbi la machafuko na akafafanua hivi:

“Tukichukulia,kuwa Kosovo,itapata uhuru wake,basi wakazi wa maeneo mengine,hasa kutoka zile sehemu zisizotambuliwa,watauliza kwanini wanatendewa vibaya zaidi ya wengine.”

Kwa upande mwingine,mjumbe wa Umoja wa Mataifa, Ahtisaari amesema,ni matumaini yake kuwa suala la mustakabali wa Kosovo litatenzuliwa kabla ya Ujerumani kumaliza zamu yake kama rais wa Umoja wa Ulaya mwishoni mwa mwezi wa Juni.Kuambatana na ombi la Serbia,Umoja wa Mataifa umekubali kuahirisha mazungumzo ya Kosovo hadi Februari 21.

Mazungumzo ya Kosovo tayari yaliahirishwa mara mbili kwa sababu ya kura ya maoni kuhusu katiba mpya ya Serbia iliyopigwa Oktoba mwaka jana na chaguzi za bunge zilizofanywa Januari 21.Katika kura ya maoni iliyopigwa,Waserb wengi waliunga mkono katiba mpya inayosema Kosovo ni sehemu ya nchi yao.

Kwa upande mwingine,waziri wa ulinzi wa Ujerumani,Franz-Josef Jung aliekutana na Ivanov mjini Seville aliwaambia waandishi wa habari kuwa pande zote zinapaswa kuyakubali mapendekezo yaliotolewa na Athisaari kuhusu uhuru wa kiwango fulani tu,ili kuhakikisha amani na utulivu katika kanda hiyo.

Itakumbukwa kuwa wakati wa vita vya mwaka 1999, majeshi ya NATO,yalivitimua vikosi vya Kiserb kutoka Kosovo.Tangu wakati huo,Kosovo inaongozwa na Umoja wa Mataifa kwa msaada wa walinzi wa amani wa NATO wapatao 16,000.