1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Majadiliano Mapya Kati ya Israel na Syria

P.Martin7 Mei 2008

Wakati ikihofiwa kuwa kuna uwezekano wa vita kuzuka kati ya Israel na Syria,ukweli ni kwamba nchi hizo mbili huenda ikawa zinakaribia kuafikiana.

https://p.dw.com/p/Duum
Pope John Paul II and a child release two white pigeons after the Angelus Prayer in Vatican City, Sunday 26 January 2003. Fotograf: Alessandro Bianchi dpa Bashar Assad (Syrien) #884690: Bashar Assad headshot, as Syria President, Damascus, Syria, graphic element on black Ehud Olmert (Israel) #985104: Ehud Olmert headshot, as Israel Prime Minister, graphic element on black
Waziri Mkuu wa Israel Ehud Olmert(kushoto)na Rais wa Syria Bashar al-Assad.Picha: AP / picture-alliance / dpa/dpaweb / Fotomontage DW

Kwani hata matamashi ya hivi karibuni ya Rais George W.Bush kuwa Syria na Korea ya Kaskazini zilishirikiana kinyuklia,hayakuathiri jitahada za kutafuta amani au angalao kupunguza mivutano kati ya nchi hizo mbili.

Zaidi anayo Prema Martin.

Mapema mwezi huu,Syria na Israel zilithibitisha hadharani kuwa zilikuwa na mazungumzo yasio rasmi chini ya upatanishi wa wajumbe waandamizi wa Uturuki.Gazeti la Al-Watan nchini Qatar limemnukulu Rais wa Syria Bashar al-Assad akisema kuwa amearifiwa na Waziri Mkuu wa Uturuki kuwa Israel ipo tayari kuondoka Milima ya Golan na badala yake kuwepo amani pamoja na Syria-dai hilo wala halijakanushwa na Waziri Mkuu wa Israel Ehud Olmert.

Lakini maendeleo yaliyopatikana katika juhudi hizo za Uturuki kufufua amani,hayakupokewa kwa shangwe na viongozi wa Marekani.Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Condoleezza Rice alipohotubia mkutano wa mwaka wa Halmashauri ya Kiyahudi ya Marekani hapo mwishoni mwa mwezi Aprili alisema,Marekani haipingi amani,ikiwa Syria na Israel zinatafuta amani.Akaongezea kuwa tatizo ni kwamba vitendo vya hivi sasa vya Syria haviashirii kuleta utulivu katika kanda hiyo bali ni kinyume kabisa.

Lakini aliekuwa mpatanishi wa amani wa Israel Daniel Levy anasema,msimamo wa serikali ya Bush unanga´ngania sharti kuwa Syria ibadili mwenendo wake kabla ya mazungumzo kuweza kuanzishwa.Kwa maoni ya Levy,inaonekana kana kwamba hali ya majadiliano ya amani kati ya Israel na Syria inafungamanishwa na matakwa ya Washington kuzitenganisha Syria na Iran;sera ambayo kwa kweli inapuza maslahi ya Syria ya hivi sasa kama kurejeshewa Milima ya Golan,usemi wake katika siasa za ndani za Lebanon na kuunga mkono makundi ya Hamas na Hezbollah,huku Bush akigombea kudhibiti kanda hiyo na kukomesha ushawishi wa Iran unaozidi kuenea.

Kwa maoni ya Uturuki,uvamizi wa Marekani nchini Iraq umesababisha machafuko zaidi na kuimarisha kitisho cha Wakurd kujitenga na vile vile Iran huenda ikawa imechomoza kama taifa lenye uwezo wa kukabiliana na Uturuki katika kanda hiyo.

Ikiwa Uturuki itafanikiwa katika juhudi zake kuleta amani kati ya Israel na Syria,basi Ankara itaweza kurejea katika uwanja wa kisiasa na kujiimarisha kwenye jukwaa la kimataifa.Uturuki ikisaidia kuanzisha mazungumzo kwa matumaini ya kupata amani,pande hizo tatu husika kwa kweli,zinatayarisha msingi wa makubaliano ambayo hatimae yatahitaji kuungwa mkono na serikali mpya ya Marekani.Lakini Rais Bush akibakiwa na chini ya mwaka mmoja kabla ya kuondoka madarakani,anashughulikia zaidi mchakato wa Annapolis ulioanzishwa na Marekani.Bush anataka kupata uamuzi wa mwisho wa amani kati ya Israel na Wapalestina kabla ya kumaliza awamu yake.Lakini kuendelea kutengwa kwa chama cha Hamas pamoja na mzozo wa kibinadamu katika Gaza na vivle vile harakati za Israel kuzidi kujenga makaazi ya walowezi wa Kiyahudi katika ardhi ya Wapalestina,ni mambo yanayohatarisha mchakato wa Annapolis.