1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Majeshi ya Kenya yaingia Somalia

Mohamed Dahman /AFP16 Oktoba 2011

Wanajeshi wa Kenya wamevuka mpaka na kuingia Somalia kuwashambulia waasi wa kundi la Al Shabaab, inaowatuhumu kwa kuhusika na utekaji nyara wa wananchi wa kigeni kadhaa, katika ardhi ya Kenya hivi karibuni.

https://p.dw.com/p/RrEn
Kundi la wanamgambo wa Al Shabaab (pichani)linaadamwa na wanajeshi wa Kenya walioingia SomaliaPicha: AP

Msemaji wa serikali Alfred Mutua ameliambia shirika la habari la AFP kwamba wamevuka mpaka na kuingia Somalia kuwasaka Al Shabaab ambao wanahusika na utekaji nyara na mashambulizi kwa Kenya.

Mwandishi wa AFP aliye karibu na mpaka huo, ameshuhudia kuwepo kwa idadi kubwa ya wanajeshi na ndege za kivita na helikopta zikiwa juu ya anga ya eneo hilo.

Hatua hiyo ya Kenya inakuja ikiwa ni siku moja tu baada ya Waziri wa Usalama wa Ndani nchini Kenya George Saitoti kuliita kundi la Al Shabaab lililoshajiishiwa na kundi la Al Qaeda kuwa ni adui na kuahidi kwamba watawashambulia popote pale watakapokuwepo.

Katika kipindi cha mwezi mmoja na kitu mwanamke wa Uingereza na mwanamke wa Ufaransa, wametekwa nyara kutoka maeneo ya pwani ya mapumziko ya kitalii katika matukio mawili tafauti na kutoa pigo kubwa kwa sekta ya utalii nchini Kenya.

Alhamisi iliyopita wafanyakazi wa kike wawili wa misaada wa Uhispania walitekwa nyara kutoka kambi ya wakimbizi ya Dadaab ambayo ni kambi kubwa kabisa iliyofurika wakimbizi duniani ikiwa na wakimbizi 450,000 wengi wao wakitokea Somalia.

Wakati Kenya ikililaumu kundi la itikadi kali za Kiislam la Al Shabaab kwa kuhusika na utekaji nyara huo, wataalamu wanasema utekaji nyara huo pia unaweza kuwa umefanywa na maharamia,majambazi na magenge ya uhalifu yenye tamaa.