1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Majeshi ya NATO yazidisha mashambulizi

Sekione Kitojo10 Mei 2011

Majeshi ya NATO yameshambulia tena maeneo ya mji mkuu wa Libya , Tripoli leo Jumanne. Taarifa zinaashiria kuwa mashambulio hayo yamemlenga kiongozi wa nchi hiyo Kanali Muammar Gaddafi.

https://p.dw.com/p/11DGx
Moja ya vyumba vya kulala katika nyumba iliyoharibiwa na makombora ya jeshi la NATO mjini Tripoli Libya.Picha: picture-alliance/dpa

Majeshi ya NATO yameshambulia tena maeneo katika mji mkuu wa Libya, Tripoli leo Jumanne. Taarifa zinaashiria kuwa mashambulio hayo yanamlenga kiongozi wa nchi hiyo Kanali Muammar Gaddafi . Wakati huo huo mashirika ya umoja wa mataifa yametoa wito kwa umoja wa Ulaya na NATO leo, kuziimarisha juhudi zao za uokozi kwa wakimbizi ambao wanasafiri kuelekea mataifa ya magharibi kupitia bahari ya Mediterranean kutoka Libya.

Gaddafi hajajitokeza hadharani tangu Aprili 30 wakati shambulio la anga la majeshi ya NATO liliposhambulia nyumba anamoishi katika mji mkuu wa nchi hiyo Tripoli na kumuua mtoto wake wa kiume pamoja na wajukuu wake watatu.Maafisa wa Libya wamesema kuwa mashambulio ya NATO katika eneo la Tripoli usiku wa jana limewajeruhi watoto wanne na wawili kati yao wako katika hali mbaya kutokana na majeraha waliyoyapata baada ya kukatwa na vioo vya madirisha.

Taasisi za umoja wa mataifa zimetoa wito wa kuwasaidia wakimbizi haraka baharini , baada ya ripoti kuwa boti lililokuwa na watu 600 limezama nje ya pwani ya Libya siku ya Ijumaa. Watu kadha wanahofiwa kuwa wamefariki katika tukio hilo. Huu ndio ujumbe wetu: Msisubiri kupata ishara ya kuomba msaada. Lifuateni boti, angalieni iwapo wanahitaji msaada , na waokoeni, amesema Melissa Fleming, msemaji wa shirika la umoja wa mataifa la kuwahudumia wakimbizi, UNHCR mjini Geneva.

Jean-Philippe Chauzy wa shirika la umoja wa mataifa la wahamiaji, IOM, amesema kuwa shirika lake pia limepata ushahidi kuwa wengi wa waliokuwamo katika boti hilo wakikimbia kutoka Libya wamelazimishwa kuingia katika boti hilo na wanajeshi wa Libya baada ya kuwapora mali zao walizokuwana nazo.

UNHCR imesema kuwa imewasiliana na mataifa ya umoja wa Ulaya na NATO kuwataka watoe msaada wa kijeshi baharini.

Fleming amesema kuwa kiasi cha watu 800 wamekufa maji katika meli ambazo zimekumbwa na dhoruba na kuvunjika tangu March 25 mwaka huu. Hali ya chakula na mahitaji mengine imeendelea hata hivyo kuwa mbaya amesema mratibu wa umoja wa mataifa anayehusika na masuala ya kiutu, Valerie Amos. Ameyasema hayo wakati akitoa taarifa kwa baraza la usalama la umoja wa mataifa.

Tuna wasi wasi mkubwa kuhusiana na watu wanaoishi katika maeneo ya vita. Eneo la kwanza ni eneo la Misrata, ambalo tangu miezi miwili iliyopita limekuwa likishambuliwa. Bado kipo kiasi cha kutosha cha chakula na madawa, lakini pia kuna baadhi ya watu ambao wana kiasi kidogo sana cha chakula na maji.

Libyen Ukraine Krankenschwester von Muammar al Gaddafi Galina Kolotnizkaja sucht in Norwegen Asyl
Muuguzi mkuu wa kiongozi wa Libya Moammar Gadhafi , Halyna Kolotnytska ambaye amekataliwa hifadhi ya kisiasa nchini Norway.Picha: AP

Wakati huo huo muuguzi maalum wa Muammar Gaddafi ambaye ni raia wa Ukraine amekataliwa ruhusa ya hifadhi ya kisiasa nchini Norway katika uamuzi ambao unaweza kupitiwa upya na maafisa wa ngazi ya juu wa wizara ya sheria, vimeeleza vyombo vya habari vya nchi hiyo leo.

Tunesien Libyen Flüchtlinge aus Bangladesch an der Grenze Koffer
Wakimbizi wakijaribu kuvuka mpaka wa Libya na Tunisia hivi karibuni.Picha: DW

Nayo Misri imeongeza muda kwa Walibya wanaotaka kuingia nchini humo kwa kuwaruhusu kuingia bila visa.

Misri ililazimika kuweka sharti la kuwa na visa siku ya Jumapili, na kuwalazimisha Walibya kadha ambao walikuwa wanajaribu kukimbia mapigano nchini kwao kutaharuki.

Maafisa katika viwanja vya ndege, mipakani na bandari wameanza kutekeleza sheria hiyo mara moja.

Maandamano yaliyozuka nchini Libya February 15 yamesambaa na kuwa mapigano ya silaha ambayo yamesababisha maelfu ya watu kupoteza maisha na wengi kukimbilia katika nchi jirani za Tunisia na Misri.

Mwandishi : Sekione Kitojo / rtre/afpe

Mhariri : Mohammed Abdul-Rahman