1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

'Majeshi ya Syria yataka kuufuta mji wa Al Rastan'

Admin.WagnerD17 Mei 2012

Majeshi ya serikali nchini Syria yameanza mashambulizi mapya usiku wa kuamkia Alhamis, dhidi ya mkoa wenye upinzani mkubwa wa Homs ambayo yamelenga zaidi mji wa Al-Rastan ulioko mikononi mwa waasi.

https://p.dw.com/p/14wxc
Wanajeshi wa Syria waliyojiunga na waasi wakiwa juu ya kifaru pamoja na waasi mkoani Homs.
Wanajeshi wa Syria waliyojiunga na waasi wakiwa juu ya kifaru pamoja na waasi mkoani Homs.Picha: AP

Shirika la haki za binadamu la Syria lenye makao yake mjini London limesema majeshi ya serikali yanataka kuuharibu kabisa mji huo ambao ni kitovu cha harakati dhidi ya utawala wa rais Bashar al-Assad.

Mkuu wa Shirika hilo, Rami Abdul Rahman, alisema makombora yasiyopungua 30 yaliangushwa katika mji huo katika kipindi cha dakika 10. Mji wa Al-Rastan umeshuhudia mfululizo wa mashambulizi kwa miezi kadhaa kutoka kwa majeshi ya serikali yanayotaka kuurejesha kutoka mikononi mwa waasi.

Source News Feed: EMEA Picture Service ,Germany Picture Service Askari wa jeshi la Syria Huru akifurahia mbele ya kifaru kichoharibiwa wakati wa mapigano kati ya waasi na wanajeshi wa serikali.
Askari wa jeshi la Syria Huru akifurahia mbele ya kifaru kichoharibiwa wakati wa mapigano kati ya waasi na wanajeshi wa serikali.Picha: Reuters

Abdul Rahman amewataka waagalizi wa amani wa Umoja wa Mataifa kufika haraka katika Mji huo uliozingirwa na majeshi ya serikali. Siku ya Jumatatu, timu ya waagalizi hao iliripoti kuwepo mapigano makali karibu na al Rastan ambapo wanaharakati walisema wanajeshi wasiopungua 23 na raia 7 waliuawa katika makabiliano kati ya wasi na wanajeshi wa serikali.

Milipuko mingine imeripotiwa kutikisa vijiji vya Al-Jamila na Al-Furqan katika mkoa wa Aleppo na mingine imesikika sehemu mbalimbali za mji huo uliopo kaskazini mwa Syria. Hakukuwa na taarifa za maafa yaliyosababishwa na milipuko hiyo lakini katika mji wa Al-Qatifa, mapigano yalizuka usiku baada ya wanajeshi kadhaa kutoroka jeshi na kujiunga na waasi.

Umoja wa Mataifa walia na pande zote
Umoja wa Mataifa umezilaumu pande zote katika mgogoro huu kwa kukiuka makubaliano ya kusitisha mapigano, ambayo ni sehemu ya mpango wa amani uliopendekezwa na mjumbe maalumu wa umoja huo na umoja wa nchi za jumuiya ya kiarabu, Koffi Annan.

Katika mahojiano yake ya kwanza na chombo cha habari tangu Desemba mwaka jana, rais wa Syria Bashar Al-Assad alisisitza kuwa utawala wake unapambana na mamluki kutoka mataifa ya kigeni wanaotaka kumpindua, na si raia wasio na hatia wanaotaka demokrasia.

Licha ya kunyooshewa kidole na jamii ya kimataifa kuwa ndiyo chanzo cha mgogoro huu uliodumu kwa muda wa miezi 14 na kuua watu zaidi ya 12,000, Assad aliiambia Televisheni ya Urusi ya Channel Rossiya24 kuwa majeshi yake yamewateka mamluki kadhaa na kwamba watawaweka hadharani ulimwengu upate kuwaona.

Hivi ndivyo hali inavyokuwa Mkoani Homs.
Hivi ndivyo hali inavyokuwa Mkoani Homs.Picha: Reuters

Azionya Uturuki na Lubnan
Assad pia aliyaonya mataifa jirani ambayo anayashtumu kwa kuwapatia silaha waasi na kusema kuwa ukipanda mbegu za vurugu ndani ya Syria, zinaweza kukuathiri na wewe baadaye. Ingawa hakufafanua zaidi, lakini waasi na wanaharakati wanasema majeshi ya Syria yameweka mabomu ya ardhini katika njia zinazotumiwa kupitisha silaha hasa kutoka nchi za Uturuki na Lubnan.

Assad ambaye alirithi uongozi kutoka kwa baba yake, anaonekana kuendelea kujizatiti licha miezi 14 ya harakati za kumuondoa kutokana na mgawanyiko katika jamii ya kimataifa, hasa mataifa makubwa wanachama wa kudumu wa baraza la usalama la umoja wa Mataifa, akiungwa mkono na Urusi na China.

Lubnan nako hali inazidi kuchafuka
Wakati huo huo mtu mmoja ameripotiwa kuuawa na wengine saba kujeruhiwa siku ya Alhamis katika makabiliano mapya kati ya watu wa kabila la Alawite wanaomuunga mkono rais Bashar Assad na waumini wa madhehebu ya Sunni wanaounga mkono waasi.

Source News Feed: EMEA Picture Service ,Germany Picture Service Wanajeshi wa Lubnan wakijianda kukabiliana na vurugu mjini Tripoli ambako machafuko ya Syria yanaonekana kuhamia.
Wanajeshi wa Lubnan wakijianda kukabiliana na vurugu mjini Tripoli ambako machafuko ya Syria yanaonekana kuhamia.Picha: Reuters

Makabiliano ya hapa na pale yakihusisha pia mashambulizi ya roketi na silaha za rasharasha yalianza majira ya saa 10 usiku katika vijiji vya Bab al-Tebanneh na Jabal Mohsen kwa mujibu wa afisa moja aliyetaka jina lake lihifadhiwe.

Jabal Mohsen inakaliwa na watu wa kabila la Alawite na Bab al-Tebbaneh inakaliwa na watu wanaounga mkono waasi. Mapigano kati ya watu hao mwanzoni mwa wiki hii yalisababisha vifo vya watu 9 na kujeruhi 50 na kuzua hofu ya mgogoro wa Syria kusambaa katika mataifa jirani. Vurugu hizi zilisababishwa na kukamatwa kwa sheikh moja wa kisunni kwa madai kuwa alikuwa mwanachama wa genge la magaidi.

Mwandishi: Iddi Ismail Ssessanga\APE\DPAE\AFPE
Mhariri: Charo Josephat.