1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Majivu ya volkano yavuruga safari za ndege

25 Mei 2011

Majivu ya volkano yanayosambaa angani kaskazini ya nchi za Ulaya na maambukizo ya bakteria, EHEC, yaliyowatia watu wasiwasi mkubwa, ni baadhi ya mada zilizoshughulikiwa na magazeti ya Ujerumani hii leo.

https://p.dw.com/p/RPtZ
In this photo taken on Saturday, May 21, 2011, smoke plumes from the Grimsvotn volcano, which lies under the Vatnajokull glacier, about 120 miles, (200 kilometers) east of the capital, Rejkjavik, which began erupting Saturday for the first time since 2004. Iceland closed its main international airport and canceled domestic flights Sunday as a powerful volcanic eruption sent a plume of ash, smoke and steam 12 miles (20 kilometers) into the air. (Foto:Jon Gustafsson/AP/dapd) ICELAND OUT
Wingu la majivu kutoka mlima wa volkano GrimsvotnPicha: dapd

Tukianza na wingu la majivu ya volkano linalosambaa kutoka Iceland hadi nchi za kaskazini ya Ulaya, gazeti la LÜBECKER NACHRICHTEN linakumbusha:

"Ni miezi 13 tangu mlima wa volkano uliporipuka nchini Iceland na kusababisha vurugu katika safari za anga barani Ulaya. Wakati huo, ilikubaliwa kuwa na mpango mmoja wa Ulaya kuhusu hatua za kuchukuliwa katika hali kama hiyo. Mwaka mmoja baadae, mtu anaweza kuona kuwa mlima mwingine wa volkano umeripuka; kuna kipimo kimoja kuhusu kiwango cha majivu: lakini kila nchi, imeachiwa kujiamulia yenyewe, kuhusu hatua za kuchukuliwa, kiwango hicho cha majivu kinapovukwa."

"Ugiriki na matatizo yake ya fedha ni mada inayoendelea kuwashughulisha wanasiasa na hata wahariri wa magazeti ya Ujerumani. Kwa maoni ya SÜDDEUTSCHE ZEITUNG, mwishowe kutakuwepo njia moja tu ya kuzuia matatizo ya fedha ya Ugiriki kuenea kwengineko: Nchi hiyo ipange upya madeni yake."

"Kwa maneno mengine, Ugiriki itangaze kuwa imefilisika. Hivi sasa, katika masoko ya fedha ya kimataifa, serikali ya Ugiriki inalazimika kulipa riba ya asilimia 17 kwa hisa zake. Ukweli ni kuwa serikali hiyo, haina uwezo huo. Mtu wala asijidanganye. Hata kupanga upya mfumo wake wa fedha na madeni, utaumiza. Vile vile upo uwezekano wa matatizo hayo ya fedha kuenea kwengineko. Lakini kwa hivi sasa, hakuna njia nyingine isipokuwa hiyo."

Tukigeukia mada ya maambukizo ya bakteria EHEC, gazeti la MITTELDEUTSCHE ZEITUNG linasema:

"Mripuko wa bakteria hizo unatisha. Kwani watu watatu wameshafariki dunia na wengine wako mahtuti. Wanasayansi wapo mbioni kuchunguza chanzo cha maambukizo hayo. Lakini moja ni hakika: bakteria hao huambukizwa kupitia chakula. Inadhaniwa kuwa hasi ni ukosefu wa usafi kamili majikoni. Hapa inafaa kukumbuka tena usafi wa kawaida, kama vile kuosha au kumenya mboga na matunda, pamoja na kuosha mikono vizuri, kabla ya kuanza kazi jikoni. Sasa imethibitishwa kuwa mito ya madaktari kwamba kanuni za zamani kuhusu usafi, zinapaswa kuzingatiwa kwa dhati. "

Na hatimae tunageukia mada yenye utata huku Ujerumani: mageuzi katika mfumo wa huduma za afya. Gazeti la RHEINPFALZ linasema:

"Mpaka sasa, mageuzi katika mfumo wa bima ya afya, kimsingi, yamesababisha gharama zaidi kwa huduma zilizopungua. Na wala isitazamiwe kuwa mambo yatakuwa tofauti safari hii. Vile vile, ni shida kuamini kuwa serikali ya muungano hivi sasa, ina nguvu ya kufanya mageuzi ya kimsingi, katika mifumo ya afya. Kwani ikiendelea na mpango wake, hiyo ni sawa na kujichimbia kaburi."

Mwandishi:Martin,Prema/dpa

Mhariri: Miraji Othman