1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Makabiliano yazuka Gabon

1 Septemba 2016

Kumezuka makabiliano Gabon Jumatano (31.08.2016) kufuatia kuchaguliwa tena kwa Rais Ali Bongo ambapo vikosi vya usalama vimewatawanya waandamanaji kwa kutumia gesi ya kutowa machozi na maji ya kuwasha.

https://p.dw.com/p/1JtWo
Picha: Getty Images/AFP/M. Longari

Wanaharakati wa upinzani waliingia katika eneo lenye kuzunguka jengo la bunge mjini Brazaville na kulitia moto. Makaazi ya Waziri Mkuu Paul Biyoghe -Mba pia yametiwa moto.

Ghasia hizo zimezuka baada ya Bongo kuchaguliwa tena kwa ushindi wa kura chache na hiyo kurefusha utawala wa familia yake wa miaka 49. Tume ya uchaguzi imesema Bongo alipata asilimia 49.80 ya kura katika uchaguzi uliofanyika Jumamosi wakati mpizani wake mkubwa Jean Ping akimfuatia kwa karibu kwa kupata asilimia 48.23 ya kura.

Chaguzi za rais huwa zinafanyika kwa duru moja nchini Gabon ambapo mgombea mwenye wingi wa kura moja kwa moja anahesabiwa kuwa mshindi.

Ping anaituhumu serikali kwa kufanya udanganyifu. Katika maandamano yaliofanyika mji mkuu wa Brazaville na mji wa pili kwa ukubwa wa Port- Gentil waandamanaji walikuwa wakipiga mayowe "Ali Bongo lazima ang'oke."

Uharibifu na uporaji

Kwa mujibu wa mashuhuda waandamanaji katika miji mengine kadhaa walifanya uharibifu kwenye duka moja kubwa,waliunguza magari, walipora benki na kuunguza pia majengo zikiwemo mali za naibu waziri mkuu.Vikosi vya usalama vilitumia gesi ya kutowa machozi na maji ya kuwasha kuwatawanya waandamanaji hao.

Hali ilivyokuwa Brazaville.
Hali ilivyokuwa Brazaville.Picha: Getty Images/AFP/M. Longari

Uporaji na makabiliano pia vilitokea wakati wa uchaguzi uliopita mwaka 2009 baada ya Bongo kushinda ambapo alishika madaraka kufuatia kifo cha baba yake Omar Bongo aliyetawala nchi hiyo kwa muda mrefu.

Wawakilishi wa upinzani wanasema kwenye milango ya saa saba za usiku leo hii wanajeshi waliotambuliwa kama ni walinzi wa rais walifyetuwa risasi za moto wakati walipovamia makao makuu ya chama cha upinzani cha Ping na kujeruhi watu 20.

Rene Ndemeze'o Ndiang mkurugenzi wa kampeni wa Ping amesema mtu mmoja ameuwawa lakini Ping mwenyewe alikuwa hayuko katika makao makuu hayo ya chama wakati wa purukushani hizo.

Matokeo ya kila kituo yabainishwe

Mkaazi mmoja amesema vikosi vya serikali pia vilishambulia radio ya upinzani na kituo cha televisheni cha NTV.Televisheni ya taifa imeripoti kwamba mawaziri wanakutana asubuhi hii kujadili hali hiyo.

Polisi wa kutuliza ghasia wakikabiliana na wanaadamanaji wa upinzani.
Polisi wa kutuliza ghasia wakikabiliana na wanaadamanaji wa upinzani.Picha: Getty Images/AFP/M. Longari

Mkoloni wa zamani wa nchi hiyo Ufaransa leo imetowa taarifa ikielezea wasi wasi wake mkubwa kwa yale yanayojiri Gabon kufuatia uchaguzi wa nchi hiyo na imezitaka pande zote mbili kuchukuwa hatua za kujizuwiya kupalilia machafuko.

Umoja wa Ulaya umetaka tume ya uchaguzi nchini humo iweke hadharani kwa kina matokeo ya kila kituo cha uchaguzi ili kuhakikisha amani na utulivu nchini humo. Marekani pia imeitaka serikali kutowa matokeo ya kila kituo cha uchaguzi ili kuwapa matumaini na imani wananchi wa Gabon na Jumuiya Kimataifa kwamba matokeo hayo ya kura yaliyotangazwa ni sahihi.

Mwandishi : Mohamed Dahman /AFP/dpa/

Mhariri : Daniel Gakuba