1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Makaburi ya pamoja yagunduliwa Malaysia

24 Mei 2015

Malaysia imesema Jumapili (25.05.2015) imegunduwa makaburi ya pamoja ya wahamiaji wa Bangladesh na Warohingya ambao ndio kitovu katika mzozo wa kusafirisha binaadamu kwa magendo.

https://p.dw.com/p/1FVql
Wahamiaji wa Rohingya na Bangladesh waliowasili Indonesia.
Wahamiaji wa Rohingya na Bangladesh waliowasili Indonesia.Picha: Reuters/Beawiharta

Waziri wa mambo ya ndani Zahid Hamidi amekaririwa na tovuti ya gazeti la The Star akisema kwamba makaburi hayo yamegunduliwa karibu na kambi zinazowashikilia wahamiaji hao ambazo zinasimamiwa na makundi yanayosafirisha binaadamu kwa magendo.

Zahid amekaririwa akisema " Lakini hatujuwi kuna makambi mangapi na yumkini tukagunduwa miili zaidi."

Kwa mujibu wa gazeti hilo la The Star makambi hayo yalikuwa yametelekezwa wakati polisi ilipoyagunduwa wiki iliopita.

Serikali ya Malaysia huko nyuma ilikuwa iikataa kuwepo kwa makaburi ya pamoja kama hayo au kambi za watumwa katika ardhi yake.

Mifupa ya binaadamu imejaa makaburini

Polisi katika nchi jirani ya Thailand mapema mwezi wa Mei iligunduwa kambi za siri vichakani za kusafirisha binaadamu kwa magendo kwa upande wa pili wa mpaka wao pamoja na makaburi ya kina kifupi.

Wahamiaji wa Rohingya.
Wahamiaji wa Rohingya.Picha: Getty Images/Afp/C. Archambault

Repoti iliomkariri Zahid haikuwa na maelezo ya kina lakini gazeti la lugha ya Malay Utusan Malaysia likikariri duru isizozitaja jina awali lilirepoti kwamba takriban makaburi 30 ya pamoja yamegunduliwa yakiwa na mamia ya mifupa ya binaadamu.

Gazeti la Star pia limekariri duru na kusema kwamba makaburi hayo inaaminika kuwa yalikuwa ya wahamiaji wa jamii ya wachache ya Warohingya wanaofikia 100.

Thailand ilianza msako wa kupambana na makundi yanayosafirisha binaadamu kinyume na sheria kufuatia kugundulika kwa makaburi yake ya pamoja jambo ambalo lilitibuwa njia zinazotumiwa kusafirisha wahamiaji hao katika kanda hiyo.

Wahamiaji hutelekezwa baharini

Wahamiaji wengi huko nyuma walijaribu kuingia Malaysia nchi wanayopendelea kukimbilia kwa kupitia mpaka wake na Thailand.Hivi sasa makundi yanayosafirisha binaadamu kwa magendo yanautelekeza mzigo wao huo wa binaadamu baharini ambapo mashua zilizosheheni mamia ya wahamiaji wanaokufa njaa kutoka nchi hizo mbili zimekuwa zikijaribu kuingia Malaysia,Thailand na Indonesia ambazo nazo zimewakatalia.

Wahamiaji wa Rohingya na Bangladesh.
Wahamiaji wa Rohingya na Bangladesh.Picha: picture-alliance/EPA/Myanmar Information Ministry

Zikikabiliwa na ongezeko la shinikizo la kimataifa Malaysia na Indonesia wiki iliopita zimesema zitawapokea wahamiaji hao ambao baadae itabidi warudishwe makwao au watafutiwe makaazi mapya.

Jeshi la Indonesia limesema Jumapili kwamba Rais Joko Widodo ameiamuru nchi yake ianze msako na operesheni za uokozi kwa mashua za wahamiaji zilizokwama baharini operesheni ambayo imeanza kazi hapo Ijumaa.

Msemaji wa jeshi Fuad Basya ameliambia shirika la habari la AFP kwamba watawaokowa wahamiaji na kuwafikisha fukweni ameongeza kusema kwamba hadi kufikia Jumamosi usiku hakuna mashua mpya zilizoonekana.

Malaysia kushiriki katika uokozi

Huko nyuma wavuvi wa Indonesia wamekuwa wakiwasaidia mamia ya Wabangladeshi na Warohingya waliokwama baharini kufika ufukweni.

Polisi wa Myanmar wakiwasaidia wahamiaji kushuka kwenye mashua.
Polisi wa Myanmar wakiwasaidia wahamiaji kushuka kwenye mashua.Picha: picture-alliance/EPA/Myanmar Information Ministry

Serikali ya Malaysia imetangaza Alhamisi kwamba manowari zake na walinzi wake wa mwambao pia wataandaliwa kwa ajili ya kuwatafuta na kuwaokowa wahamiaji lakini hadi sasa haikurepoti juu ya uokozi wowote ule.

Widodo amedokeza Jumapili kwamba serikali yake ya Indonesia itahitaji msaada wa kimataifa kugharamia makaazi ya maelfu ya wahamiaji hao wa kimaskini.

Zaidi ya wahamiaji 3,500 wameogelea hadi fukweni au wameokolewa kwenye mwambao wa Malaysia, Indonesia,Thailand na Bangladesh tokea kuripuka kwa mzozo huo mapema mwezi huu.

Wakati Wabangladeshi wengi ni wahamiaji wa kiuchumi wanaoukimbia umaskini nchini mwao Warohingya wanaondoka Myanmar kukimbia vitendo vya ubaguzi na ukandamizaji kutoka kwa jamii ya Wabudha walio wengi nchini humo.

Mwandishi : Mohamed Dahman/AFP

Mhariri : Oumilkheir Hamidou