1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Makubaliano kuhusu mpango wa kinyuklia wa Iran yafikiwa

13 Januari 2014

Iran imepata makubaliano na mataifa yenye nguvu duniani kuhusu mpango wake wa kinyuklia na makubaliano hayo yataanza kutekelezwa kuanzia tarehe 20 mwezi huu.

https://p.dw.com/p/1ApVX
Picha: Reuters

Tangazo la kuwa Iran imeafikiana na nchi tano wanachama wa kudumu wa baraza la usalama la umoja wa Mataifa pamoja na Ujerumani kwanza lilitangazwa na maafisa wa Iran na baadaye kuthibitishwa na mkuu wa sera za kigeni wa Umoja wa Ulaya Catherine Ashton.

Iran imekubali kusitisha kwa kipindi cha miezi sita urutubishaji wa madini ya Urani ili ilegezewe vikwazo na jumuiya ya Kimatiafa vinavyoathiri pakubwa uchumi wa nchi hiyo.

Iran imekubali kuruhusu shirika la umoja wa Mataifa la kudhibiti kawi ya atomiki kuzuru na kukagua vinu na viwanda vyake vya kinyuklia ili kuhakiki kuwa inazingatia masharti ya makubaliano yaliyofikiwa.

Vikwazo kulegezwa kuanzia Februari 1

Naibu waziri wa mambo ya nje wa Iran Abbas Araghchi amewaambia wanahabari kuwa kiasi cha dola bilioni 4.2 zilizotokana na uuzaji wa mafuta ambazo zilikuwa zinazuiwa sasa zitaachiwa chini ya makubaliano hayo kuanzia tarehe moja mwezi ujao kwa kipindi cha siku 180 zijazo.

Mkuu wa sera za kigeni wa umoja wa Ulaya Bi Catherine Ashton na waziri wa mambo ya nje Javad Zarif
Mkuu wa sera za kigeni wa umoja wa Ulaya Bi Catherine Ashton na waziri wa mambo ya nje Javad ZarifPicha: Reuters

Rais wa Marekani Barrack Obama amekaribisha makubaliano hayo na kusema kuwa yataendeleza lengo lao la kuizuia Iran kuunda silaha za kinyuklia.Obama ameongeza kuwa kwa ajili ya amani na usalama duniani, ni wakati sasa wa kutoa fursa kwa diplomasia kufanya kazi.

Bi Ashton alisifu makubaliano hayo na kusema misingi thabiti na ya kueleweka imewekwa.Waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani Frank Walter Steinmeier ameyataja makubaliano hayo kuwa hatua muafaka ambayo wanaweza kuitegemea.

Mnamo mwezi Novemba mwaka jana,Iran ilikubali kupunguza urutubishaji wa madini ya Urani hadi asilimia tano na kupunguza kiwango ilicho nacho hivi sasa cha kawi ya nyuklia hadi asilimia 20 katika kipindi cha miezi sita.

Makubaliano yakudumu kupatikana

Katika kipindi hicho ambacho pia vikwazo vya kiuchumi dhidi ya Iran vitalegezwa,mashauriano kati ya Iran na nchi zenye nguvu zaidi duniani Marekani,Ufaransa,Uingereza,China,Urusi na Ujerumani yataendelea ili kuwe na makubaliano ya kudumu.

Waziri wa mambo ya nje John Kerry
Waziri wa mambo ya nje John KerryPicha: Reuters

Nchi za magharibi zinahofia kuwa mpango wa kinyuklia wa Iran unaazimia kutengeza silaha za kinyuklia lakini Iran imekuwa ikisisitiza ni kwa lengo la kutoa tu nishati.

Iran sasa itaruhusiwa kufanya biashara kadhaa kama uuzaji na ununuzi wa dhahabu,uuzaji wa bidhaa za petroli na katika masuala ya usafiri wa ndege na reli,kupata mahitaji ya kibinadamu lakini bado haitaweza kutumia benki za Marekani na vikwazo bado vipo.

Makubaliano hayo ni ushindi kwa Rais wa Iran Hassan Rouhani aliyeingia madarakani mwaka jana akiahidi kutafuta suluhu la mzozo huo wa kinyuklia ambao umedumu kwa miaka mingi.

Mwandishi:Caro Robi/afp/ap

Mhariri:Daniel Gakuba