1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Makubaliano ya amani yasainiwa Ufilipino

27 Machi 2014

Serikali ya Ufilipino na waasi wa kiislamu wamesaini makubaliano ya amani kumaliza uasi na uhasama wa muda mrefu uliosababisha umwagikaji mkubwa wa damu katika taifa hilo.

https://p.dw.com/p/1BWYO
Miriam Coronel-Ferrer kiongozi wa jopo la upatanishi la serikali akipeana mkono na Mohagher Iqbal kiongozi wa upanishi upande wa waasi
Miriam Coronel-Ferrer kiongozi wa jopo la upatanishi la serikali akipeana mkono na Mohagher Iqbal kiongozi wa upanishi upande wa waasi

Makubaliano hayo ya amani yamesainiwa ( 27.03.2014) baada ya miaka 17 ya majadiliano kati ya viongozi wa kundi la wapiganaji wa kiislamu la Moro(milf )na serikali.

Viongozi wa kundi la kiislamu la vuguvugu la Ukombozi la Moro MILF wamesaini makubaliano ya amani kwa sharti la kuchukua udhibiti wa eneo lililopangiwa kujitenga katika eneo la kusini mwa nchi hiyo ya Ufilipino ambayo inakaliwa na idadi kubwa ya waumini wa kikatoliki.Akizungumza kabla ya kusainiwa makubaliano hayo ya kihistoria makamu mwenyekiti wa MILF Ghazali Jaafari ameliambiaa shirika la habari la AFP kwamba kwa miaka mingi wamekuwa wakiongoza harakati za watu wa jamii ya Bangsamoro na wengi wa watu hao wamepitia matatizo mengi na kwahivyo makubaliano haya ni muhimu sana kwa jamii hiyo na hasa kwakuwa yanamaliza mapigano katika eneo la Mindanao.

wanajeshi wa Ufilipino wakibeba masunduku ya maiti za wenzao waliouwawa katika mapigano Kusini
wanajeshi wa Ufilipino wakibeba masunduku ya maiti za wenzao waliouwawa katika mapigano KusiniPicha: AP

.Aidha waziri mkuu wa Malaysia ambaye ni mpatanishi mkuu katika mgogoro huo wa Ufilipino ametoa rai kwa pande zote mbili serikali na waasi kujitahidi kuyazingatia makubaliano hayo ya amani yanayofungua ukurasa mpya katika taifa hilo.

Waasi wakiislamu wamekuwa katika mapambano kwa muda wa zaidi ya miongo minne kwa ajili ya kudai uhuru na kujitenga eneo hilo la kusini la Mindanao ambalo wanalitazama kama eneo lao la jadi.Mamia kwa maelfu ya watu waliuwawa katika mgogoro huo wakati jimbo hilo la Mindanao likiwa ndiilo masikini kabisa na linalokabiliwa na kiwango kikubwa cha rushwa nchini Ufilipino.

Kiongozi wa Ufilipino Benigno Aquino pamoja na mwenyekiti wa kundi la MILF Murad Ebrahim ndio walioshuhudia tukio la kusainiwa kwa makubaliano hayo ya amani katika sherehe zinazoendelea kwenye ikulu ya rais mjini Manila.

Wakimbizi kutoka jimbo la Mindanao
Wakimbizi kutoka jimbo la MindanaoPicha: AP

Makubaliano hayo amani yanatowa mwito wa pande hizo mbili kushirikiana katika kutafuta na kuhakikisha utekelezaji wake.Aidha viongozi wa kundi la waasi la MILF hatimae watahitajika kuwaagiza wapiganaji wake kuweka chini silaha wakati viongozi hao wakijiunga katika siasa na kuliongoza jimbo hilo lililojitenga.Jimbo hilo litajumuisha kiasi asilimia 10 ya ardhi ya Ufilipino pamoja na kuwa na jeshi lake la polisi,bunge la mkoa pamoja na kuwa na mamlaka ya kukusanya kodi.Hata hivyo serikali kuu mjini Manilla itaendelea kudhibiti ulinzi.Bado lakini kuna makundi mengine madogo madogo ambayo yanaendelea na mapigano na hayajaridhika la makubaliano hayo.

Mwandishi:Saumu Mwasimba

Mhariri:Mohammed Abdul-Rahman.