1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Makubaliano ya kusitisha mapigano Syria yavunjika

28 Oktoba 2012

Mapigano yameendelea nchini Syria karibu na mji wa Damascus na upande wa kaskazini Jumamosi(27.10.2012)baada ya kuvunjika kwa hatua ya kusitishwa mapigano iliyotangazwa kwa ajili ya sikukuu ya Kiislamu.

https://p.dw.com/p/16YIA
Source News Feed: EMEA Picture Service ,Germany Picture Service Smoke from what activists say was missile fired by a Syrian Air Force fighter jet loyal to Syria's President Bashar al-Assad is seen at Erbeen, near Damascus October 27, 2012. REUTERS/Maawia Al-Naser/Shaam News Network/Handout (SYRIA - Tags: POLITICS CIVIL UNREST) FOR EDITORIAL USE ONLY. NOT FOR SALE FOR MARKETING OR ADVERTISING CAMPAIGNS. THIS IMAGE HAS BEEN SUPPLIED BY A THIRD PARTY. IT IS DISTRIBUTED, EXACTLY AS RECEIVED BY REUTERS, AS A SERVICE TO CLIENTS
Mashambulizi ya anga ya jeshi la SyriaPicha: Reuters

Makubaliano ya kusitisha mapigano kwa ajili ya sikukuu ya Eid al-Adha ambayo ilianza Ijumaa, kimsingi ilikubaliwa na serikali na waasi wa jeshi linalopigana ili Syria iwe huru, FSA, yalileta uwezekano wa kusitishwa kwa mara ya kwanza kwa mapigano baada ya mzozo uliodumu miezi 19 sasa.

Baada ya kuzuka kwa mapigano hayo mapya siku ya Ijumaa na Jumamosi , waasi pamoja na kundi linaloangalia hali nchini Syria wamesema kuwa makubaliano hayo ya kusitisha mapigano kwa hakika yamekufa.

Ndege zashambulia

Wakati mapigano baina ya majeshi ya serikali ya rais Bashar al-Assad na waasi yakiendelea, ndege za kivita za Syria zilishambulia jengo katika maeneo yanayoshikiliwa na waasi mashariki ya mji mkuu wa Damascus , sehemu ambayo imeshuhudia mapigano makali kwa muda wa wiki kadha, na kusababisha vifo vya watu wanane.

"Haya ni mashambulio ya kwanza ya anga tangu kutangazwa, kusitishwa mapigano kwa muda wa siku nne katika wakati wa sikukuu ", limesema kundi linaloangalia haki za binadamu nchini Syria.

International peace envoy for Syria Lakhdar Brahimi (2nd R) speaks at a news conference at the Arab League headquarters in Cairo October 24, 2012. Syria said on Wednesday its military command was still studying a proposal for a holiday ceasefire with rebels - contradicting international mediator Brahimi's earlier announcement that Damascus had agreed to a truce. Also pictured are former Irish president Mary Robinson (R), former Norwegian prime minister Gro Harlem Brundtland (L) and former U.S. president Jimmy Carter. REUTERS Mohamed Abd El Ghany (EGYPT - Tags: POLITICS CONFLICT)
Mjumbe wa amani wa Syria Lakhdar BrahimiPicha: Reuters

"Makubaliano hayo yamekufa," mkurugenzi wa kundi hilo Rami Abdel Rahman amesema. "Hatuwezi tena kuzungumzia kuhusu kusitishwa mapigano."

Shambulio jingine la anga limefanyika karibu na kituo cha kijeshi cha Wadi Deif katika jimbo la kaskazini magharibi la Idlib, ambako waasi wamekuwa wakipambana katika azma ya kuteka kituo hicho, kundi hilo limesema.

Makubaliano yamekufa

Kamanda wa waasi katika mji wa kaskazini wa Aleppo amesema kuwa hakuna shaka kuwa juhudi za kusitisha mapigano , zilizopendekezwa na mjumbe wa kimataifa wa amani Lakhdar Brahimi , zimevunjika.

"Hii ni kushindwa kwa Brahimi. Juhudi hizi zimekufa kabla hazijaanza," Abdel Jabbar al-Okaidi, mkuu wa baraza la kijeshi la waasi mjini Aleppo , ameliambia shirika la habari la AFP kwa simu.

Amesisitiza kuwa jeshi la waasi la FSA halijavunja makubaliano hayo ya kusitisha mapigano na linachukua tu hatua za kujihami.

"Nimekuwa katika maeneo mbali mbali ya mstari wa mbele wa mapambano jana na jeshi la serikali halijaacha mashambulio yake ya makombora," Okaidi amesema. "Jukumu letu ni kuwalinda raia, na si sisi ambao tunashambulia."

Lakini jeshi la serikali limewashutumu waasi kwa kuendelea kukiuka makubaliano na kuapa kuwa litajibu ukiukaji huo.

"Kwa siku ya pili, makundi ya kigaidi yameendelea kukiuka makubaliano ya kusitisha mapigano yaliyotangazwa na kuheshimiwa na uongozi wa jeshi la serikali," jeshi la Syria limesema katika taarifa iliyosomwa katika televisheni.

"Jeshi litaendelea kufuatilia hatua hii ya ukiukaji wa makubaliano, na kujibu mashambulio dhidi ya vitendo hivi vya wahalifu.

Msemaji wa wizara ya mambo ya kigeni Jihad Maqdisi amesema kuwa jeshi la nchi hiyo linania ya kuendelea kwa hatua ya kusitisha mapigano, na kuwalaumu waasi kwa kuchochea hatua ya kulipiza kisasi kutoka jeshi la serikali.

Mahujaji waandamana

Wakati huo huo, maafisa nchini Saudi Arabia wamewatawanya haraka waandamanaji kadhaa ambao ni mahujaji kutoka Syria wanaotaka kuangushwa kwa rais wa nchi hiyo Bashar al-Assad na kushutumu kile walichokisema kuwa ni kushindwa kwa jumuiya ya kimataifa kuzuwia umwagikaji wa damu nchini Syria.

Kwa mujibu wa shirika la habari la Reuters na watu walioshuhudia waandamanaji walibeba bendera ya waasi na kufanya maandamano kuelekea daraja la Jamarat katika eneo la Mina, mashariki ya mji mtakatifu wa Mecca nchini Saudi Arabia, ambako zaidi ya mahujaji wa Kiislamu milioni 3 walikusanyika kwa ajili ya hija inayofanyika kila mwaka.

Mwandishi: Sekione Kitojo /rtre /afpe

Mhariri: Grace Patricia Kabogo