1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Makubaliano ya Serikali ya Muungano yafikiwa Ujerumani

27 Novemba 2013

Kansela Angela Merkel na muungano wa vyama vyake vya kihafidhina vya CDU, na CSU, wamekamilisha mkataba wa kuunda serikali ya muungano pamoja na SPD miezi miwili baada ya uchaguzi mkuu.

https://p.dw.com/p/1APIK
Kutoka kushoto ni mwenyekiti wa chama cha CDU Angela Merkel,Sigmar Gabriel wa SPd na Horst Seehofer wa chama cha CSUPicha: John Macdougall/AFP/Getty Images

Makubaliano hayo ya kurasa 170 yaliyotangazwa leo alfajiri baada ya majadiliano yaliyodumu zaidi ya saa 17 yatamuwezesha kansela Angela Merkel kuunda serikali yake ya tatu kabla ya siku kuu za Krismasi. Kabla ya hapo lakini wanachama zaidi ya laki nne na 70 elfu wa SPD watabidi watamke kama wanayakubali au la.

Akizungumza na waandishi wa habari mwishoni mwa majadiliano yao katibu mkuu wa chama cha SPD, Andrea Nahles, amechambua mada zilizokubaliwa akisema:"Ni pamoja na kiwango cha chini cha mishahara, Euro 8 na nusu kwa saa moja ya kazi kuanzia mwaka 2015, bila ya shaka umri wa mtu kuweza kustaafu, fedha zaidi kwa serikali za miji na katika sekta ya elimu na tumefanikiwa kweli kwa namna ambayo tunaweza kusema hakuna mtoto aliyezaliwa na kukulia huku atakayelazimishwa tena kuchagua uraia. Haya ni baadhi ya matokeo ya mazungumzo ambayo tunahisi tunaweza kuyafikisha mbele ya wafuasi wetu na tunaweza kuwashauri waseme ndio wameyakubali."

Makubaliano ya Maana kwa Ujerumani

Hata wawakilishi wa vyama vya kihafidhina vya CDU na CSU wameridhika na makubaliano yaliyofikiwa. "Makubaliano yaliyofikiwa ni ya maana kwa nchi yetu," amesema katibu mkuu wa chama cha Christian Democratic Union, Hermann Gröhe, akihoji makubaliano yana muhuri wa kihafidhina; "hakuna kodi ya ziada wala mikopo ya ziada," amesema.

Große Koalition CDU und SPD einigen sich 27. Nov. 2013 Dobrindt und Gröhe
Makatibu wakuu wa vyama ndugu vya CDU na CSU,Alexander Dobrindt (kulia) na Hermann GröhePicha: Reuters

Pindi wanachama wa SPD wakiunga mkono mkataba wa kuunda serikali kuu ya muungano Desemba 14, Angela Merkel atachaguliwa na wabunge Desemba 17 ijayo kuiongoza serikali ya muungano wa vyama vikuu kwa muhula wa tatu wa miaka minne.

Nani atakabidhiwa Wizara Gani?

Wakuu wa vyama vyote hivyo vya kisiasa wanatarajiwa baadaye hii leo kuitisha mkutano na waandishi habari kuzungumzia makubaliano yaliyofikiwa. Suala la nani atakabidhiwa wizara gani litajibiwa pengine baadaye.

Große Koalition CDU und SPD einigen sich 27. Nov. 2013 Kraft und Steinmeier
Frank Walter Steinmeier na waziri mkuu wa jimbo la North Rhine Westphalia bibi Hannelore Kraft.Picha: picture-alliance/dpa

Mwandishi:Hamidou Oummilkheir/dpa/Reuters/AFP

Mhariri: Josephat Charo