1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Makundi ya upinzani Syria yakubali kushiriki mazungumzo

11 Desemba 2015

Makundi makubwa ya upinzani ya Syria yamesema yako tayari kushiriki katika mazungumzo ya kimataifa kwa kuwashirikisha wawakilishi wa Rais Bashar al-Assad, lakini yamesisitiza kwamba Rais Assad aondoke madarakani.

https://p.dw.com/p/1HLju
Picha: Getty Images/AFP/K. Desouki

Wawakilishi wa makundi ya upinzani nchini Syria wamesema ili kuanza mchakato wa kipindi cha mpito wa kisiasa, inambidi Rais Assad aondoke madarakani. Kwa mara ya kwanza makundi kadhaa ya kisiasa na yale yenye silaha yanayohasimiana, yamekutana kwenye mji mkuu wa Saudi Arabia, Riyadh na wamekubaliana kuhusu mfumo wa mazungumzo ambayo mataifa yenye nguvu duniani yamekuwa yakitaka yafanyike.

Katika taarifa yao ya pamoja wawakilishi hao wamesema wako tayari kujadiliana na wawakilishi wa serikali ya Assad katika muda maalum uliopangwa na Umoja wa Mataifa. Hata hivyo, makundi hayo ya upinzani yamesisitiza kwamba Assad na wasaidizi wake inabidi waachie madaraka ili kuanza kipindi cha mpito, kilichowekwa katika mazungumzo ya mwezi uliopita mjini Vienna.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, John Kerry amesema nchi yake imefurahishwa na hatua iliyofikiwa Riyadh, akisema ni matokeo mazuri yaliyopiga hatua katika kufikiwa suluhisho la kisiasa. Msemaji wa wizara hiyo, John Kirby amezishukuru jitihada zilizofanywa na Saudi Arabia.

''Ninapofikisha ujumbe wangu kwa Waziri wa mambo ya nje Al-Jubeir, tunaushukuru uongozi wa Saudi Arabia kwa kuitisha mazungumzo ya wawakilishi wa makundi 116 ambao leo wamekubaliana kuhusu muundo wa chombo cha mazungumzo yao kitakachowawakilisha kwenye mchakato wa kisiasa,'' alisema Kirby

Kundi moja lasusia mazungumzo hayo

Hata hivyo, moja kati ya makundi muhimu ya waasi nchini Syria la Ahrar al-Sham, limesema limeyasusia mazungumzo hayo. Lakini duru za ndani katika mazungumzo hayo na wanadiplomasia wa mataifa ya Magharibi, zimeeleza kuwa kundi hilo lilihudhuria na limesaini makubaliano yaliyofikiwa, ingawa taarifa hizo hazikuweza kuthibitishwa mara moja.

Waziri John Kerry na mwenzake wa Saudi Arabia, Adel al-Jubeir
Waziri John Kerry na mwenzake wa Saudi Arabia, Adel al-JubeirPicha: Reuters/C. Allegri

Kulingana na makubaliano hayo yaliyofikiwa jana mjini Riyadh, makundi ya upinzani yameunda ''kamati kuu ya mazungumzo,'' itakayokuwa na makaazi yake Riyadh. Awali Waziri wa Mambo ya Nje wa Saudi Arabia, Adel al-Jubeir, alisema bila wasiwasi wowote Rais Assad ataondoka madarakani, iwe kwa suluhisho la kisiasa au la kijeshi, kwa sababu watu wa Syria hawamtaki tena.

Wakati huo huo kiasi ya raia 22 wameuawa katika mashambulizi matatu tofauti ya mabomu yaliyotegwa ndani ya gari, kaskazini-mashariki mwa Syria. Shirika linalofuatilia haki za binaadamu nchini Syria, limesema mashambulizi hayo yametokea kwenye mji wa Tal Tamr, jimbo la Hasakeh.

Ama kwa upande mwingine, jeshi la Marekani limesema mkuu wa masuala ya fedha wa kundi lenye itikadi kali la Dola la Kiislamu-IS, Abu Saleh ameuawa katika mashambulizi ya anga yanayofanywa na jeshi la muungano nchini Syria.

Msemaji wa jeshi la Marekani, Kanali Steve Warren amesema Saleh aliuawa mwezi uliopita pamoja na maafisa wengine wawili waandamizi wa IS.

Wakati hayo yakijiri, ndege iliyowabeba wakimbizi 163 wa Syria, imewasili Toronto nchini Canada na kupokelewa na Waziri Mkuu wa nchi hiyo, Justin Trudeau.

Mwandishi: Grace Patricia Kabogo/AFPE,DPAE
Mhariri: Iddi Ssessanga