1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Malalamiko baada ya Hans-George Maaßen kupewa kazi mpya

Zainab Aziz
19 Septemba 2018

Baada ya vuta nikuvute hatimae mkuu wa shirika la ujasusi wa ndani la hapa nchini Ujerumani Hans-Georg Maaßen avuliwa madaraka lakini wakati huohuo apewa wadhifa mwingine hatua iliyozusha kelele.

https://p.dw.com/p/3594I
Hans-Georg Maaßen
Picha: Getty Images/S. Gallup

Baadhi ya wanasiasa wa chama cha Social Democrats (SPD) wamekasirishwa na hatua ya viongozi wao ya kuukubali mpango wa kumbadilisha kazi  Maaßen badala ya kumfuta kazi moja kwa moja. Serikali ya Kansela Angela Merkel imemwondoa mkuu wa idara ya ujasusi wa ndani Hans-George Maaßen na kumhamishia kwenye wizara ya mambo ndani. Merkel alifanya uamuzi huo ili kuumaliza mzozo wa utatanishi mkubwa uliosababishwa na suala la uhamiaji na siasa za mrengo mkali wa kulia.

Mzozo huo uliitikisa serikali hiyo  ya mseto inayoongozwa na Kansela Merkel. Maasen sasa atakuwa naibu waziri kwenye wizara ya mambo ya ndani kama ilivyotangazwa na bibi Merkel pamoja na viongozi wengine wa vyama vinavyounda serikali yake ya mseto baada ya mazungumzo ya kuutatua mgogoro huo.

Kiongozi wa chama cha Waliberali (FDP) Christian Lindner
Kiongozi wa chama cha Waliberali (FDP) Christian LindnerPicha: Getty Images/AFP/O. Messinger

Wanasiasa wa upinzani wameelezea kutoridhishwa kwao na uamuzi wa kumpa bwana Maaßen wadhfa mwingine, Christian Wolfgand Lindner kiongozi wa chama cha Waliberali anayafananisha yale yanayotokea sasa kuwa sawa na suluhisho bandia.

Naibu kiongozi wa chama cha SPD, Ralph Stegner ambacho ni sehemu ya serikali ya mseto ameliambia shirika la habari la hapa Ujerumani dpa kwamba hoja ya kumbadilishia kazi Hans-Georg Maassen ni maafa makubwa na kwamba uvumilivu katika chama chake wa kuendelea kuwemo katika serikali ya mseto unazidi kuyeyuka.

Viongozi wa chama cha SPD pamoja na wale wa vyama vya upinzani wa chama cha Kijani, chama cha Waliberali na chama cha Linke walitaka Maaßes ajiuzulu au afutwe kazi kwa kujiingiza katika masuala ya kisiasa, na pia kwa kufanya mikutano mara kwa mara na viongozi wa chama cha upinzani kinachopinga wahamiaji hapa nchini Ujerumani cha AfD.

Kansela wa Ujerumani Angela Merkel
Kansela wa Ujerumani Angela MerkelPicha: Reuters/H. Hanschke

Kiongozi mwenza wa chama cha  kijani Katrin Goering-Eckardt ameeleza masikitiko yake kwamba mtu ambaye alistahili kuadhibiwa badala yake anapewa cheo kipya. Amesema bwana Maaßen kwa mtazamo wake amepoteza heshima yake.

Mwafaka uliofikiwa umeupa muhula wa nne wa bibi Merkel pumzi nyingine ya uhai baada ya washirika wengine wa serikali yake wa chama cha SPD kusisitiza kuondolewa kwa Maassen kinyume na msimamo wa waziri wa mambo ya ndani Horst Seehofer wa chama ndugu cha Christian Social Union, CSU cha jimbo la Bavaria la kusini mwa Ujerumani.

Mkuu huyo wa zamani wa idara ya ujasusi wa ndani alisababisha mjadala mkali baada ya kuutilia mashaka usahihi wa ripoti juu ya wahuni wa mrengo mkali wa kulia na manazi mamboleo kuwawinda na kuwashambulia kiholela wahamiaji katika mji wa Chemnitz uliopo mashariki mwa Ujerumani mnamo mwezi wa Agosti.

Mwandishi:Zainab Aziz/DPA/AFP

Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman