1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Malaria inauwa maelfu ya watu kuliko Ebola

29 Desemba 2014

Juhudi za kukabiliana na ugonjwa hatari wa Ebola kwenye eneo la Afrika Magharibi, zimekwamisha kampeni dhidi ya Malaria ambao unazuilika na kutibika, lakini umesababisha vifo vya maelfu ya watu kuliko hata Ebola.

https://p.dw.com/p/1EB2K
Aina ya mbu anayesababisha malaria
Aina ya mbu anayesababisha malariaPicha: picture-alliance/dpa

Imeelezwa kuwa madaktari katika eneo la Gueckedou nchini Guinea ambako ugonjwa wa Ebola ulianzia, waliacha kuchukua vipimo vya malaria. Kiwango cha kuuripoti ugonjwa wa malaria kilishuka kwa asilimia 40 nchini Guinea, hatua ambayo Mkurugenzi Msaidizi wa mpango wa rais wa Marekani wa kupambana na malaria, Dokta Bernard Nahlen, anasema siyo nzuri.

Amesema kushuka kwa kiwango cha kuripoti visa vya malaria, kunatokana na watu kuogopa kwenda kwenye vituo vya afya, hivyo hawapati matibabu ya malaria. Takwimu zinaonyesha kuwa nchini Guinea, nusu ya watu milioni 12 hawana uwezo wa kupata huduma za afya na wanafariki bila ya kuhesabiwa.

Kiasi Waguinea 15,000 walikufa kwa malaria mwaka uliopita, 14,000 wakiwa ni watoto wenye chini ya umri wa miaka mitano. Kwa mujibu wa takwimu za Shirika la Afya Duniani-WHO, kiasi watu 1,600 wamekufa kutokana na ugonjwa wa Ebola nchini Guinea.

Shirika la Nets for Life lenye makao yake mjini New York, ambalo limekuwa likitoa msaada wa vyandarua vilivyowekewa dawa ya kuuwa mbu, limesema malaria ni chanzo cha vifo vya watoto wenye chini ya umri wa miaka mitano nchini Guinea na baada ya ugonjwa wa Ukimwi ambao ni chanzo cha vifo vya watu wazima.

Dalili za Ebola na malaria zinafanana

Ebola na malaria zina dalili sawa ikiwemo homa, kizunguzungu pamoja na maumivu ya kichwa na misuli. Takwimu za WHO zinaonyesha kuwa asilimia 24 ya watu wa Gueckedou waliopimwa homa mwezi Oktoba walikutwa na Ebola pamoja na malaria na asilimia 33 kati yao ambao hawakuwa na Ebola, walikuwa na malaria.

Wafanyakazi wa afya wakimhudumia mgonjwa wa Ebola, Sierra Leone
Wafanyakazi wa afya wakimhudumia mgonjwa wa Ebola, Sierra LeonePicha: REUTERS/Baz Ratner

Ugonjwa wa malaria umewaua madaktari 38 wa Cuba waliopelekwa Guinea kusaidia katika mapambano dhidi ya Ebola. Dokta Nahlen amesema shirika lake linafanya utafiti wa kitaifa wa vituo vya afya na kwengineko ili kubaini ni wapi watu wenye malaria wanakwenda kutibiwa.

Anasema kwenye nchi jirani ya Liberia, serikali ilisitisha mpango wa kugawa vyandarua milioni 2. Nako Sierra Leone, nchi ambayo ilishika nafasi ya tatu katika nchi zilizoathiriwa na Ebola, madaktari wasio na mipaka, mwezi huu walichukua hatua isiyokuwa ya kawaida ya kugawa dawa za kujikinga na kutibu malaria kwa watu milioni 1.5.

Patrick Robataille kutoka shirika la madaktari wasio na mipaka mjini Freetown, anasema watu wamekuwa wakimiminika kwenye vituo vya kutibu Ebola, wakidhani wameambukizwa ugonjwa huo, huku ukweli ikiwa ni kwamba wameambukizwa malaria. Imeelezwa kuwa madaktari wamekuwa waoga wa kuchukua sampuli ya damu kwa wagonjwa ili kuwapima malaria.

Mwandishi: Grace Patricia Kabogo/APE
Mhariri:Josephat Charo