1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Malaria yachochea kuenea kwa virusi vya HIV Afrika

Mohamed Dahman8 Desemba 2006

Ugonjwa wa malaria yumkini ukawa unasaidia kuenea kwa virusi vya HIV barani kote Afrika bara ambalo limeathiriwa vibaya sana na gonjwa hilo lisilokuwa na tiba.Timu ya wanasayansi imesema kwenye utafiti wao uliochapishwa kwenye jarida la Sayansi kwamba namna magonjwa hayo mawili yanavyoingiliana kwa kiasi kikubwa huzidisha kutapakaa kwa magonjwa hayo miongoni mwa watu wanaoishi kusini mwa jangwa la Sahara barani Afrika.

https://p.dw.com/p/CHly
Muathirika kwa UKIMWI nchini Afrika Kusini mojawapo ya nchi ilioathirika vibaya na gonjwa hilo ilioko Kusini mwa Jangwa la Sahara barani Afrika.
Muathirika kwa UKIMWI nchini Afrika Kusini mojawapo ya nchi ilioathirika vibaya na gonjwa hilo ilioko Kusini mwa Jangwa la Sahara barani Afrika.Picha: AP

Wanasayansi wanasema malaria ugonjwa unaosabishwa na mbu kwa kiasi kikubwa huupa nguvu kima cha upungufu wa virusi vya kingamaradhi viliomo kwenye damu za waathirika na hiyo kufanya iwe ni jambo linaowezekana sana kuwaambukiza wenza wao katika ngono.

Kiongozi wa utafiti huo Laith Abu-Raddad wa Kituo cha Utafiti wa Kansa cha Fred Hutchinson huko Seattle na katika Chuo Kikuu cha Washington nchini Marekani anasema kiwango kikubwa zaidi cha kasoro ya virusi hivyo vya kingamaradhi husababisha maambukizi zaidi ya virusi vya HIV na malaria husababisha kuwepo kwa kiwango kikubwa cha upungufu wa virusi vya kingamaradhi vyenye HIV.

Abu-Raddad ambaye ni mtafiti wa UKIMWI anakadiria kwamba malaria imesaidia virusi vya HIV kuwaambukiza mamia kwa maelfu pengine hata mamilioni ya watu kusini mwa jangwa la Sahara barani Afrika.UKIMWI uligundulika kwa mara ya kwanza robo karne iliopita.

Watafiti hao wanasema wakati huo huo virusi vya HIV huchochea kuenea kwa malaria kwa sababu watu walioambukizwa virusi hivyo wanakuwa rahisi kuathirika na malaria kutokana na virusi vya HIV kuushambulia na kuudhofisha mfumo wa asili wa kujikinga na maradhi mwilini.

UKIMWI na malaria vimejikita kusini mwa Jangwa la Sahara barani Afrika.Abu- Raddad anasema wanasayansi wameshangazwa wakati walipongamuwa kwamba ngono zembe katika eneo hilo haitoshi kujielezea kuwa ndio sababu ya kuenea kwa haraka kwa virusi vya HIV na kwamba lazima pia kuna sababu nyegine.

Watafiti hao walilenga kazi zao huko Kisumu mji wa Kenya ulioko kandoni mwa Ziwa Viktoria ambapo magonjwa ya malaria na virusi vya HIV ni mengi.Wanasema asilimia 5 ya maambukizi ya HIV yanatokana na kuongezeka kwa kima cha upungufu wa virusi vya kingamaradhi vyenye HIV kulikosababishwa na malaria na asilimia 10 ya kesi za malaria kwa watu wazima zinaweza kuwa zimetokana na virusi vya HIV.

Tokea mwaka 1980 watu 8,500 zaidi waliambukizwa virusi vya HIV na kulikuwa na kesi za malaria zaidi 980,00 .Mtu anaweza kupata malaria zaidi ya mara moja katika mji huo wenye wakaazi 200,000.

Kwa mujibu wa Raddad utafiti huo una faida kwa juhudi za huduma za afya kwa wananchi ambapo kunaonekana umuhimu kwa serikali kuyashughulikia magonjwa hayo kwa pamoja.

Huko nyuma wanasayansi walibaini kwamba kutotahiriwa kwa wanaume na ukeketaji wa wanawake pia kunaharakisha kuenea kwa virusi vya HIV.Abu- Raddad anasema wanaume waliotahiriwa wako katika nafasi ndogo ya kuambukizwa virusi vya HIV na kwamba ukeketaji unafunguwa njia kwa virusi vya HIV kumuambukiza mtu.

Kati ya watu milioni 39 na nusu waliaombukizwa virusi vya HIV milioni 24 wako katika nchi za kimaskini za kusini mwa jangwa la Sahara barani Afrika.Takriban vifo vya watu mlioni mbili na laki tisa kutokana na UKIMWI katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita vimetokea kwenye eneo hilo.

Malaria huuwa zaidi ya watu milioni moja kwa mwaka wengi wao wakiwa ni watoto kusini mwa jangwa la Sahara barani Afrika.

Watafiti wanasema sasa malaria inaweza kuhesabiwa kuwa sababu ya tatu kuu inayochochea kuenea kwa virusi vya HIV.