1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mali inataka msaada wa jeshi la kimataifa kuidhibiti sehemu ya kaskazini

25 Septemba 2012

Mali imeuomba Umoja wa Mataifa utoe kibali cha haraka kwa jeshi la kimataifa liisaidie serikali ya nchi hiyo izidhibiti tena sehemu za kaskazini ya nchi hiyo.

https://p.dw.com/p/16DhS
Mkutano wa Umoja wa Mataifa New York
Mkutano wa Umoja wa Mataifa New YorkPicha: picture-alliance/dpa

Habari hiyo imetolewa na waziri wa mambo ya kigeni wa Ufaransa, Laurent Fabius.

Nchi hiyo ya Afrika magharibi ilitumbukia katika michafuko mwezi Machi mwaka huu, pale wanajeshi walipompindua kutoka madarakani rais, hivyo kuweko pengo wazi la madaraka. Hali hiyo iliwawezesha waasi wa Ki-Tuareg kutwaa thuluthi mbili ya nchi hiyo. Lakini makundi ya kiislamu, baadhi yao yakiwa na ushirikiano na mtandao wa Al-Qaeda, yaliuteka nyara uasi huo katika sehemu za kaskazini ya nchi na kuanzisha kutekelezwa sheria za kiislamu.

Akiiashiria barua iliopelekwa na viongozi wa mpito wa Mali kwa katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-moon, hapo Septemba 18, Laurent Fabius alisema Mali imeomba lipitishwe azimio la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa chini ya Ibara ya Saba ya Hati ya Umoja huo ili kutolewe kibali cha kutumiwa jeshi la kimataifa lilisaidie jeshi la Mali kuyateka tena maeneo ya kaskazini mwa Mali. Ibara hiyo ya Saba inaliruhusu baraza la usalama litoe kibali cha kuchukuliwa hatua kutoka zile za kibalozi na za kiuchumi hadi kujiingiza kijeshi.

Waziri wa Mambo ya Kigeni wa Ufaransa Laurent Fabius
Waziri wa Mambo ya Kigeni wa Ufaransa Laurent FabiusPicha: AP

Laurent Fabius, akiisoma barua hiyo, aliwaambia waandishi wa habari kwamba kwa miezi kadha Mali imekuwa ikikabiliwa na mzozo wa usalama usiowahi kuonekana kabla katika maeneo yake ya kaskazini ambayo yametawaliwa na makundi yenye silaha, wakiwemo magaidi, wasafirishaji wa mihadharati na aina zote za wahalifu. Alisema serikali ya Mali inataka jeshi la aina hiyo lipelekwe kwa haraka ili kuyasaidia majeshi ya usalama ya Mali kutekeleza shughuli hiyo.

Msemaji wa katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa amehakikisha kwamba Ban Ki-Moon ameipokea barua hiyo, na akasema inachunguzwa.

Ufaransa yafanya mazungumzo na wanachama wengine

Bwana Fabius alisema ombi la Mali litazungumziwa katika mkutano wa ngazi ya juu utakaozingatia kesho hali ilivyo katika Ukanda wa Sahel barani Afrika wakati wa kikao cha Hadhara Kuu ya Umoja wa Mataifa. Aliongeza kusema kwamba Ufaransa imeanza kufanya mazungumzo na wanachama wengine wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa juu ya namna ya kusonga mbele na jambo hilo.

Julai Tano mwaka huu, Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa lilitoa kibali zichukuliwe juhudi na nchi 15 za Jumuiya ya Kiuchumi ya Afrika Magharibi- ECOWAS- ili kuumaliza mzozo wa Mali, lakini lilijizuia kuunga mkono kujiingiza kijeshi katika nchi hiyo. Japokuwa ombi hilo la Mali ni hatua inayofuata, Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa halifikiriwi kwamba litaipa kibali jumuiya ya ECOWAS kujiingiza kijeshi Mali hadi pale jumuiya hiyo itakapotoa maelezo zaidi juu ya mkakati wake.

Kiongozi wa mpito wa Mali Dioncounda Traore
Kiongozi wa mpito wa Mali Dioncounda TraorePicha: picture-alliance/dpa

Kiongozi wa mpito wa Mali, Dioncounda Traore, alitoa ombi rasmi kwa ECOWAS mwanzoni mwa mwezi huu kutaka msaada wa kijeshi. Umoja huo wa ECOWAS badala yake ulitoa mpango wa operesheni ya hatua tatu ili kuitwaa tena Mali ya Kaskazini, lakini Traore aliomba tu wanajeshi wapelekwe kama hatua ya mwisho, hivyo mabishano baina ya serikali ya Mali na Jumuiya ya ECOWAS juu ya kuwekwa wanajeshi katika mji mkuu wa Mali yaliuzuwia mwenendo huo. Wanabalozi wa nchi za magharibi, faraghani, wana wasiwasi juu ya mipango hiyo ya sasa ya ECOWAS, na pia bado sio wazi kama Urusi italiunga mkono azimio litakaloruhusu kujiingiza kijeshi. Ufaransa, mkoloni wa zamani wa Mali, imeahidi kutoa msaada wa usafiri na kubadilishana taarifa za kijasusi kama sehemu ya mpango wa kujiingiza baadae, lakini imesema haitapeleka moja kwa moja wanajeshi katika nchi hiyo. Sababu ni kwamba tawi la Al-Qaeda katika eneo la Afrika Kaskazini linawashikilia mahabusu wa kifaransa. Serikali za nchi za Afrika Magharibi na zile za nchi za Magharibi zinailinganisha hali ilivyo Mali na katika eneo la Sahel sawa na ile iliyoko Afghanistan.

Mwandishi: Miraji Othman/Reuters

Mhariri: Mohammed Abdulrahman