1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mali ya Libya kuachiwa

31 Agosti 2011

Baraza la usalama la Umoja wa mataifa limeidhinisha kuachiwa euro bilioni 1.8 ya mali ya Libya iliyokuwa imezuiliwa Uingereza.

https://p.dw.com/p/12QFR
Fedha zitatumika kwa misaada ya kibinaadamuPicha: picture alliance/dpa

Ujerumani imeomba pia kuachia kiasi ya euro bilioni moja, huku nayo Ufaransa inataka kuachia kiasi ya euro bilioni tano, kusaidia kununuwa msaada wa kibinaadamu na kuendeleza huduma za kijamii nchini Libya. Ufaransa imeuomba pia Umoja wa Ulaya kutuma waangalizi Libya kusaidia kuijenga upya nchi hiyo.

Sarkozy in China
Rais wa Ufaransa Nicolas SarkozyPicha: dapd

Waziri wa mambo ya nje wa Ufaransa, Allain Juppe, ameliambia gazeti la kila siku la Ujerumani, Frankfurter Algemeine Zeitung, kuwa Ufaransa imetekeleza jukumu lake katika kushinikiza uvamizi wa jeshi la magharibi Libya, na kuwa wengine ikiwemo Ujerumani, inapaswa kuwajibika kwa mengine.

Ujerumani iliwakasirisha washirika wenzake mnamo mwezi Machi kwa kuisusia kura ya baraza la usalama la umoja wa mataifa kuidhinisha usaidizi wa kijeshi na marufuku ya ndege kutoruka katika anga ya Libya. Ufaransa imewakaribisha viongozi duniani mjini Paris hapo kesho Alhamisi kujadili ujenzi upya wa Libya.

Libyen Tripolis Aufständische haben den Stützpunkt Bab al Asasija gestürmt
waasi nchini LibyaPicha: dapd

Wakati huo huo waasi nchini Libya wametoa muda hadi mwisho Jumamosi kwa miji ambayo bado inamtii Muammer Gaddafi, kujisalimisha au ikabiliwe na nguvu za kijeshi. Mkuu wa baraza la kitaifa la waasi nchini humo, Mustafa Abdel Jalil amewaambia waandishi habari katika mji unaodhibitiwa na waasi Benghazi, kuwa mazungumzo yanaendelea ya kujisalimisha miji hiyo, pia katika mji alikozaliwa kiongozi wa nchi hiyo Muammer Gaddafi, Sirte. Kwa mujibu wa msemaji wa Shirika la kujihami NATO, Oana Longescu, waasi hao bado wanaendelea kupokea usaidizi wa angani kutoka ndege za kivita za NATO. Aliongeza kuwa kazi ya NATO bado haijakamilika.

Katibu mkuu wa Umoja wa mataifa, Ban Ki Moon, amekiambia kikao maalum cha baraza la usalama la Umoja wa mataifa kuhusu Libya hapo jana, kuwa sasa anatumai kupatikana suluhisho ya haraka kwa mzozo na mateso yaliopo Libya. Waasi Libya wanasema watu 50,000 wamefariki katika vita hivyo vya wenyewe kwa wenyewe.

Mwandishi: Maryam Abdalla/afpe, rtre, ape
Mhariri:Abdul-Rahman, Mohammed