1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mama Mjerumani afungwa kwa kumchuuza mwanawe kwa wabakaji

Mohammed Khelef
7 Agosti 2018

Mwanamke huyo amehukumiwa kifungo cha miaka 12 jela kwa kumuuza mwanawe wa kiume mwenye miaka 9 kwa wabakaji kupitia mtandao wa intaneti katika moja ya matukio ya kikatili kabisa kuwahi kushuhudiwa.

https://p.dw.com/p/32kbz
Deutschland Freiburg Urteil im Staufener Missbrauchsfall
Picha: picture-alliance/Dpa/P. Seeger

Siku ya Jumanne (7 Agosti 2018), mahakama ya Freiburg, kusini magharibi mwa Ujerumani, ilimtia hatiani mwanamke huyo aliyetambulishwa kwa jina la Berrin T. mwenye umri wa miaka 48 na mpenziwe wa kiume Christian L. mwenye umri wa miaka 39 kwa makosa yapatayo 60, yakiwemo ya kumlazimisha mvulana huyo kuingia kwenye ukahaba, kumtisha kwa maneno na kumtesa, ubakaji na ukatili uliopindukia mipaka.

Jaji Stefan Bürgelin alisema kwenye hukumu yake kwamba dhamira ya mama huyo ni ya kulaaniwa na ushiriki wake kwenye kumdhalilisha mwanawe ulitokana na lengo la kuhakikisha kuwa mpenzi wake mpya hamuachi.

Baadaye, maslahi ya kifedha yaliingia kati, ambapo wawili hao walipata maelfu ya euro kwa kumchuuza kijana wao kwa wabakaji. 

Wawili hao walikuwa ndio watuhumiwa wakuu wa mtandao wa wabakaji wanaopenda kufanya mapenzi na watoto wadogo uliokuwa ukifanya shughuli zake katika mji wa Staufen, kando kigodo ya Freiburg.

Wote wawili walikiri sio tu kumchuuza kijana huyo kwa wanaume kadhaa, bali pia na wao wenyewe kutenda ukatili dhidi yake. 

Hati ya mashitaka inaonesha kuwa mama huyo na mpenziwe waliwaruhusu wanaume wa kigeni na wenyeji wa eneo hilo waliowapata kwenye mtandao kumbaka na kumdhalilisha mvulana huyo wa miaka 9 ndani ya kipindi cha miaka miwili ili wapatiwe fedha.

Ukatili wa kutisha

Deutschland Freiburg Urteil im Staufener Missbrauchsfall
Mmoja wa watuhumiwa wa ubakaji wa mvulana wa miaka 9.Picha: picture-alliance/dpa/P. Seeger

Picha za vidio za uhalifu huo zilikuwa zikiuzwa mtandaoni, huku baadhi yake zikimuonesha mvulana huyo akiwa amezibwa kitambaa usoni na kufungwa kamba mikononi na miguuni. 

Polisi waliugundua mtandao huo wa ubakaji mwezi Septemba 2017 baada ya kupatiwa taarifa na msamaria mwema. Polisi waliwakamata Berrin T., mama wa mtoto huyo, na mpenziwe wa kiume, ambaye alishawahi kutiwa hatiani kwa kudhalilisha watoto. 

Wanaume wengine watatu wa Kijerumani, mmoja wa Uswisi na mwengine raia wa Uhispania wameshahukumiwa vifungo vya miaka kumi kwa kila mmoja kutokana na udhalilishaji huu. Awali waendesha mashitaka walitaka mama mtoto huyo na mpenziwe kufungwa miaka 14 jela.

Kile kinachoitwa mtandao wa giza ni sehemu iliyofichikana kwenye mtandao wa intaneti ambayo inafikiwa tu na watu wenye utaalamu wa programu za kompyuta na hauwezi kuonekana kupitia mashine za kusaka taarifa mtandaoni kama vile Google ama Yahoo. 

Eneo hili lililojificha mara kadhaa huhusishwa na biashara chafu, ingawa pia hutumika kwa malengo mengine, kama vile ujasusi, kama vile ambavyo nyaraka za siri zilivyopenyezwa kuwafikia WikiLeaks, au kama ambavyo mvujisha siri wa Marekani, Edward Snowden, alivyoutumia kuwasiliana na waandishi wa habari.

Mwandishi: Mohammed Khelef/DW English
Mhariri: Iddi Ssessanga