1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Masaibu yazidi kumwandama Jose Mourinho

17 Agosti 2015

Masaibu yanaendelea kuongezeka na kumkosesha usingizi kocha wa Chelsea Jose Mourinho mapema kabisa katika kampeni yake ya kutetea taji la Ligi Kuu ya Kandanda ya England.

https://p.dw.com/p/1GGke
UEFA Champions League Chelsea vs. Schalke 04
Picha: Reuters/Eddie Keogh

Katika mpambano wa kwanza mzito msimu huu, Chelsea ilizidiwa nguvu jana kwa kufungwa tatu bila katika ngome ya Manchester City kichapo ambacho huenda kikawa na athari ya muda mrefu ya kisaikolojia miongoni mwa mahasimu hao wawili katika kinyang'anyiro cha ubingwa wa ligi. City lipata mabao yake kupitia Sergio Aguero, Vincent Kompany na Fernandinho.

Kasi ya mashambulizi ya Man City ilimfanya Jose kumwondoa uwanjani John Terry – ikiwa ndio mara ya kwanza kabisa kuwahi kumwondoa nahodha wake huyo. Nafasi yake ilichukuliwa na chipukizi Kurt Zouma.

Habari pekee nzuri baada ya kichapo hicho ni kusainiwa kwa beki wa kushoto Abdul Rahman Baba kutoka klabu ya Augsburg ya ligi kuu ya Ujerumani – Bundesliga. Lakini ukweli ni kwamba Chelsea imekuwa na mwanzo mbaya kabisa katika harakati za kutetea ubingwa licha ya kuwa Mourinho aliyataja matokeo hayo kuwa ni “bandia”. Jose alisema "Kwa sababu katika kipindi cha kwanza, timu bora ilikuwa inashinda na katika kipindi cha pili, timu bora ilikuwa Chelsea. Hatukufunga. Ikiwa matokeo ya moja bila baada ya kipindi cha pili, katika maoni yangu yalikuwa si haki, hebu fikiria kama ingekuwa mbili bila au tatu bila. Walikuwa timu bora katika kipindi cha kwanza na kuudhibiti mchezo, wakatengeneza nafasi. Tuliumiliki mpira lakini katika ulinzi tulikuwa dhaifu".

Fußball Manchester City-Manager Manuel Pellegrini
Pellegrini anasema Manchester City itatwaa ubingwa msimu huuPicha: Reuters/Eddie Keogh

Mwenzake wa City Manuel Pellegrini amejigamba akisema kawaida City huwa inaidhibiti Chelsea wakati wote. "Nimeridhika sana kwa sababu siyo rahisi kuwashidna mabingwa. Chelsea walikuwa timu bora, walishinda taji msimu uliopita na nadhani kipindi cha kwanza tulistahili kupata angalau magoli matatu. Katika kipindi cha pili, labda tulikuwa na ugumu kidogo kutokana na kadi za njano, hivyo kasi ikapungua. Lakini Chelsea haikuwa na nafasi zozote na kisha tukafunga magolin mengine mawili ambayo tulistahili kupata katika kipindi cha kwanza"

Katika mchuano mwingine wa jana Arsenal ilipata ushindi wake wa kwanza msimu huu kwa kuifunga Crystal Palace mbili moja matokeo ambayo kocha Arsene Wenger anasema yamerejesha ujasiri wao wa kuwania taji. Hii leo Liverpool itapambana na Bornemouth

Katika michuano ya Jumamosi, Southampton 0 Everton 3, Sunderland 1 Norwich 3, Swansea 2 Newcastle 0, Tottenham 2 Stoke 2, Watford 0 West Brom 0, West Ham 1 Leicester 2. Siku ya Ijumaa, Aston Villa 0 Manchester United 1

Mwandishi: Bruce Amani/AFP/DPA/reuters
Mhariri: Iddi Ssessanga