1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mamea wa miji mikuu kadhaa duniani wakutana

18 Mei 2007

Mamea kutoka miji mikuu mbali mbali ulimwenguni wamekutana mjini NewYork wiki hii pamoja na wafanya biashara wa kimataifa, watalaamu wa mazingira na wawakilishi wa huduma za miji kujadili njia muafaka za kupunguza ongezeko la gesi chafu duniani.

https://p.dw.com/p/CHkt
Meya wa jiji la New York Michael Bloomberg
Meya wa jiji la New York Michael BloombergPicha: AP

Mkutano huo ulilenga kutafuta mbinu zitakazotumiwa ili kupunguza ongezeko la gesi chafu kwa kuanzisha mikakati ya matumizi ya njia safi za usafiri na miundo mbinu inayofaa katika sekta ya nishati.

Zaidi ya mamea 30 walishiriki katika mkutano huo wa siku nne ambao pia ulihudhuriwa na wajumbe kutoka miji mikuu ya mabara sita ulimwenguni.

Rais wa zamani wa Marekani Bill Clinton akitoa mchango wake alisema kundi lake la Clinton linalojishughulisha na maswala ya hali ya hewa litazinduwa mpango wa dunia nzima wa kiasi cha dola bilioni tano utakao isaidia miji 15 mikubwa zaidi ulimwenguni kukarabati majengo yake yaliyochakaa ili yaweze kuokoa matumizi makubwa ya nishati.

Mabadiliko ya hali ya hewa ni tatizo linalo ukabili ulimwengu mzima na linahitaji kushughulikiwa kutoka ngazi za mashinani.

Katika hotuba yake meya wa jiji la New York Michael Bloomberg alisisitiza lengo lake la kupunguza gesi chafu kwa kiwango cha asilimia 30 katika jiji lake la New York kufikia mwaka 2030.

Katika mkutano huo meya wa jiji la Berlin Klaus Wowereit alisema.

“Namnukuu’’..tumejadili hapa kuhusu uwezekano wa kuanzisha malipo maalum kwa magari ili kuingia kati kati ya mji wa New York kama inavyofanyika katika jiji la London, nadhani jijini Berlin watu wangu watanishika koo iwapo nitaanzisha huduma ya aina hiyo lakini hata hivyo maendeleo yanaweza kuafikiwa tu kutokana na maamuzi magumu..“Mwisho wa kumnukuu’’.

Meya wa London Ken Livingston alifanikiwa kuanzisha malipo hayo maalumu mwaka 2003 na kwa mujibu wa meya huyo hayo yalikuwa mapendekezo ya jamii ya wafanya biashara waliozingatia gharama zinazosababishwa na misongamano ya magari.

Meya huyo aliwahakikishia viongozi wa miji mikubwa kuwa hatua kama hiyo haita athiri kuchaguliwa kwao akitoa mfano kuwa yeye mwenyewe umaarufu wake ulizidi baada kuanzisha mpango huo.

Bibi Katie Mandes mkurugenzi wa mawasiliano wa kituo kinachosimamia mabadiliko ya hali ya hewa duniani chenye makao yake nchini Marekani amesema miji mikubwa huenda ikawa ni mfano wa maabara za kujifunzia.

Hata hivyo amesisitiza kuwepo mfumo utakaozihusisha nchi zote duniani zikiwemo Marekani, China na India kupitia katika umoja wa mataifa.

Marekani hadi sasa haiambatani na mkataba wa Kyoto unaozingatia upunguzaji wa gesi chafu.